HEADER AD

HEADER AD

RAS PWANI AWAOMBA WANANCHI KUSHIRIKIANA NA TRA ILI KUKUSANYA KODI STAHIKI


Na Gustaphu Haule, Pwani 

KATIBU  Tawala wa Mkoa wa Pwani Pili Mnyema amewaomba wadau wa Mkoa huo kuendelea kushirikiana na Mamlaka ya Mapato ( TRA) ili kuhakikisha wanakusanya kodi stahiki kwa ajili ya maendeleo ya Mkoa na Taifa.

Mnyema  ametoa wito huo Julai 1, 2026 wakati akizungumza na wadau hao katika hafla ya maadhimisho ya miaka 30 ya kuanzishwa wa TRA yaliyofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.

         Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Pili Mnyema wa kwanza kulia akikata keki katika hafla ya maadhimisho ya miaka 30 ya TRA yaliyofanyika katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani Julai 1/2026.

Katika maadhimisho hayo yaliambatana na utoaji wa tuzo za Rais za Mlipakodi bora na kwamba zaidi ya tuzo 30 zilitolewa ambapo waliotoa tuzo hizo ni Kamishna wa TRA nchini Yusuf Mwenda, Waziri wa Fedha Khamis Omary pamoja na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuwa kodi iliyokuwa inakusanywa katika kipindi cha Miaka 30 ni kielelezo cha maendeleo ya Taifa ambapo imesaidia Serikali kujenga miundombinu mbalimbali ya Elimu,Afya ,Maji , Barabara na huduma nyingine za kijamii.

Amesema wanapoanza Julai 1,2026 Serikali imeanza utekelezaji wa dira ya Taifa ya 2020/2050  ambapo dira hiyo imetoa kipaumbele kwa sekta binafsi katika kuchangia uchumi wa nchi.

Mnyema amesema kuwa Serikali na TRA wamepewa jukumu la kukusanya kodi na kuhakikisha Wanawake mazingira mazuri ya sekta binafsi ili hiweze kuchangia mapato ya nchi kwa asilimia 70.

Amewataka watumishi wa TRA Mkoa wa Pwani kuongeza juhudi na maarifa katika ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu bila kumuonea mfanyabiashara au mdau yeyote.

         Baadhi ya wadau walioshiriki maadhimisho ya miaka 30 ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika ukumbi wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.

",Nawapongeza watumishi wa TRA Mkoa wa Pwani kwakufanya kazi nzuri ya ukusanyaji mapato kwani hadi sasa imevuka malengo kutoka Sh.bilioni 27 ya Mwaka  2015/2016 hadi kufikia Sh.bilioni 266 ya  mwaka 2025/2026  ,"amesema Mnyema.

Mwakilishi wa meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Salim Makame amesema kuwa anawashukuru wadau kwa kujitokeza kushiriki katika maadhimisho hayo kwakuwa walikuwa pamoja katika kufuatilia maagizo ya Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan.

              Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Pili Mnyema ( katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa TRA Mkoa wa Pwani katika hafla ya maadhimisho ya miaka 30 ya TRA yaliyofanyika Julai 1,2026 katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.

Amesema kuwa TRA imeanza mwaka mpya wa fedha wa 2026/2027 na kwamba ameomba ushirikiano kutoka kwa wadau hao ili kuweza kufikia malengo ya ukusanyaji.

Hata hivyo, Makame amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan anatamani kuiona TRA inafanya vizuri pale anapomaliza muda wake kwahiyo ni vyema ushirikiano huo ukawa endelevu ili kufikia malengo ya Mwaka mpya wa fedha.


No comments