DKT. DAVID MRAMBA AWAASA VIJANA KUACHA KUTUMIKA KWA MASLAHI YA WENGINE

Na Gustaphu Haule , Pwani
KATIBU wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani Dkt. David Mramba amewaasa vijana kuacha kutumika kwa maslahi ya watu wengine kwa kufanya vitendo vitakavyowaingiza katika matatizo.
Dkt. Mramba amesema vijana wajikite katika masuala ya elimu, kazi, ubunifu na hata fursa za kilimo kwani ndiyo njia salama ya kujenga maisha yao.
Dkt.Mramba ametoa kauli hiyo Julai 1, 2026 wakati akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu kulinda amani na utulivu wa nchi.
Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM)Mkoa wa Pwani Dkt.David Mramba akizungumza n Waandishi wa habari ofisini kwake Julai 1/2026.
Amesema katika nyakati ambazo kuna tofauti za kisiasa ni muhimu kila mmoja kutumia busara kwani Katiba na Sheria za nchi zimeweka njia mbalimbali za kutoa maoni ,kushiriki katika siasa na kueleza mitazamo .
Amesema tofauti za kisiasa zisiwe chanzo cha chuki,vurugu au uhasama kati ya Watanzania kwahiyo amewasihi Wananchi wa Mkoa wa Pwani kuacha kushawishiwa kufanya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa maisha,mali na uchumi.
Mramba, ameongeza kuwa kila mzazi amlinde mtoto wake,kila kijana afikirie mustakabali wake na kila mwananchi alinde amani ambayo imegharimu juhudi kubwa kuijenga.
",Tusikubali tofauti za kisiasa zitugawanye kwakuwa baada ya uchaguzi au mijadala ya kisiasa sisi sote tunabaki kuwa Watanzania, majirani,ndugu na marafiki na Taifa letu lina nguvu pale tunapoweka mbele maslahi ya nchi kuliko tofauti zetu,"amesema Mramba.
Amesema mkoa wa Pwani umebarikiwa kuwa na lango muhimu la uchumi wa Taifa kwani kuna Wakulima ,Wafugaji,wavuvi wafanyabiashara na wawekezaji na kwamba wote hao wanahitaji mazingira ya amani ili waendelee kuzalisha na kuchangia maendeleo ya nchi.
Mramba amewaomba Wananchi wa Mkoa wa Pwani kuendelea kuwa walinzi wa amani, kuheshimu Sheria ,kushirikiana na vyombo vya dola katika kulinda usalama na kujenga Tanzania yenye umoja na mshikamano.
Hata hivyo, Mramba amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kinampongeza na kumuunga mkono Dkt.Samia Suluhu Hassan mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anafanyakazi kubwa ya kuwatumikia Wananchi na kuendelea kudumisha hali ya amani na utulivu katika Taifa.

Post a Comment