RC PWANI AWATAKA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII KUZINGATIA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050

Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amefungua kikao kazi cha Maafisa Maendeleo ya Jamii waliopo ndani ya Mkoa huo kwa kuwataka wafanye kazi kwa kuzingatia mwongozo wa Dira ya Taifa ya maendeleo ya 2050.
Kunenge amefungua kikao hicho Julai 29/2026 kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo kwa kuwashirikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii,Wakuu wa divisheni na vitengo ,Wakuu wa idara,Wakuu wa taasisi za Serikali na binafsi.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akifungua kikao kazi cha Maafisa Maendeleo ya Jamii kilichofanyika Julai 29/2026 Kibaha .
Kunenge amesema kuwa kinachotakiwa ni kuhakikisha wanafanyakazi kuzingatia matarajio ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais anatamani kuona anapomaliza muda wake wa utumishi hasiache tu majengo bali aache tabasamu kwa Wananchi.
Amesema ili kufikia malengo yake ni lazima kila afisa Maendeleo ya Jamii ahakikishe anafanyakazi kupitia utekelezaji wa dira ya Taifa ya 2050.
Amesema kuwa maafisa Maendeleo ya Jamii wanatakiwa kuonyesha kiwango cha utendaji wao wa kazi katika maeneo yao kwakuwa wao ndio wanazijua changamoto zilizopo katika maeneo yao.
"Kwa nafasi mliyonayo lazima mbainishe changamoto na kueleza mmefanya nini na kwa kiasi gani japo hamuwezi kufanya vyote lakini jambo kubwa ni lazima mjue Wananchi wenu wanataka nini,"amesema Kunenge.
Amesema kikao cha kuwakutanisha maafisa Maendeleo ya Jamii ndio cha kwanza Tanzania kufanyika Mkoa wa Pwani na Pwani haitaki kuwa ya pili kwani mara zote wanataka kuona yale ambayo Rais Samia anatamani yatokee basi yanatokea.
Amesema anatambua maafisa Maendeleo ya Jamii wanafanyakazi nzuri lakini kama wanafanyakazi vizuri basi haitakiwi kuona kiongozi anapokuja Wananchi wananyanyua mambo kwani kitendo cha kunyanyua mabango hayo ni ishara kuwa watu hawawajibiki katika maeneo yao.
Amesema kitu pekee ni kuhakikisha lazima kila wanachokifanya kiwe ndani ya dira ya 2050 ndio maana dira hiyo imetumia makundi mbalimbali kutoka ngazi ya chini hadi juu na endapo wanafanya kinyume na dira hiyo basi wanaopoteza muda na fedha.
Amesema anawaomba Makatibu wakuu wakae na kujadili changamoto zao zilizopo katika Wizara zao kwakuwa majukumu yanaingilia ambayo kwa kiasi kikubwa yanawachanganya maafisa hao.
Amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alisema kila Wizara ipitie Sheria na Sera zake ili ziweze kuendana jambo ambalo litawapa wepesi wa kufanyakazi lakini yote kwa yote lazima wahakikishe wanaacha tabasamu kwa Wananchi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Pili Mnyema amesema kuwa malengo ya kikao kazi hicho ni kukumbushana wajibu wao ,kupeana uzoefu pamoja na kupeana taarifa za mafanikio.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Pili Mnyema akizungumza na maafisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Pwani katika kikao kilichofanyika Julai 29/2026.
Amesema maafisa Maendeleo ya Jamii ni eneo muhimu kati ya Wananchi na Serikali na wamekuwa wakifanya kazi kubwa huku akiwapongeza na kuwaomba waendelee kushirikiana zaidi na Wananchi ili kuweza kufikia malengo.
Mwakilishi kutoka ofisi ya Waziri Mkuu , Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI )Jeremiah Mwambange ,amewaagiza Maafisa ya Maendeleo ya Jamii hao kuhakikisha kila mmoja anakuwa na Kijiji chake cha mfano.
Mwambange ,amesema kuwa lengo ni kuhakikisha wanakwenda sambamba na dira ya 2020/2050 kwa kutekeleza nguzo kwa jamii ambapo kufuatia hali hiyo Tamisemi itaanzisha utaratibu wa kukutana kila septemba ili kila afisa Maendeleo ya Jamii aweze kutoa mrejesho..
Mwambange amesema maagizo mengine ni pamoja na kuhakikisha kila Halmashauri wanatekeleza suala la utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa Wananchi pamoja na kuandaa dokumentari fupi kwa vikundi vilivyofanya vizuri ili viweze kurushwa katika vyombo vya habari.
Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kikao kazi kilichofanyika Julai 29/2026 katika ukumbi wa jengo la Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Pamoja na hayo lakini pia Mwambange amewaomba maafisa Maendeleo hao kuhakikisha wanafanyakazi kwa kuzingatia takwimu halisi katika maeneo yao ili pale panapotokea na changamoto hiwe kutatua.
Hata hivyo afisa Maendeleo ya Jamii wa Mkoa wa Pwani Grace Tete amesema kuwa kikao hicho kinafanyika kwa siku mbili ikiwa ni sehemu ya kukumbusha wajibu na kupeana miongozo ya utekelezaji wa majukumu.




Post a Comment