SHILINGI YA TANZANIA , NI VYEMA IHESHIMIWE
SHILINGI ya Tanzania, ni vema iheshimiwe,
Jinsi tunavyotumia, kwa uzuri itumiwe,
Sifa kuiharibia, ni vema kulaaniwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Pesa kwa Uchumi wetu, ukue tuinuliwe,
Biashara ada zetu, huko kote itumiwe,
Shilingi maisha yetu, hufanya tuhudumiwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Tumetangaziwa sana, Shilingi iheshimiwe,
Vile tunavyoiona, vema sana itumiwe,
Kurusharusha Hapana, hufanya ichafuliwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Huwa tunazo sherehe, na watuwashangiliwe,
Cha kwetu kimuhemuhe, watu pesa wapatiwe,
Wachungaji na Mashehe, na wao tusaidiwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Unazionesha pesa, wengine wakuelewe,
Tayarisha chombo hasa, humo ndimo zitupiwe,
Hili la bure darasa, ni vema litambuliwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Vema watu kuwatunza, chombo na kiandaliwe,
TanTrade napongeza, na Kibati waenziwe,
Kuweka chombo liweza, watu pesa wapatiwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Shilingi heshima yetu, vema sana ienziwe,
Hata matumizi yetu, na isidharauliwe,
Iwe ni wajibu wetu, isifike tukemewe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Kwa wote washereheshaji, hili budi muelewe,
Mdomo wenu mtaji, wateja na waambiwe,
Mtakuwa wakosaji, kesho tusilaumiwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Onesha unazo pesa, kitaka ushangiliwe,
Unapoziweka pesa, vema sana paelewe,
Kutupatupa ni kosa, singoje ushitakiwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Kwenye cherekochereko, ninyi nyote muelewe,
Acheni hivi vituko, ifike mtambuliwe,
Mara ufike mkoko, na nyie mnyakuliwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Viongozi wa jamii, hata dini muelewe,
Eleza watu watii, kesho wasiadhibiwe,
Bila shuruti utii, vema sana uenziwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Haya mambo ya Katoro, ni vema yalaaniwe,
Hiyo ni kubwa kasoro, wenye huku muelewe,
Ni makosa tena kero, kokote yasirudiwe,
Kuzitupatupa noti, wala siyo jambo jema.
Na Lwaga Mwambande (KiMPAB)

Post a Comment