ZAIDI YA BILIONI MOJA ZATUMIKA KUJENGA STENDI BUKOBA, YAANZA KUTUMIKA
Na Alodia Dominick, Bukoba
ZAIDI ya Tsh. Bilioni moja zimetumika kujenga stendi mpya ya Bukoba ambayo imekuwa mkombozi kwa watumiaji wa stendi hiyo kwani kabla ya kujengwa kipindi cha mvua palikuwa panajaa tope.
Stendi hiyo ambayo ilianza kujengwa mwaka 2023 imefunguliwa jana na inatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi katika Manispaa ya Bukoba kwa kuboresha huduma za usafiri, kurahisisha shughuli za biashara na kuongeza mapato ya halmashauri kupitia matumizi ya miundombinu hiyo.
Baadhi ya wananchi, wamesema kufunguliwa kwa stendi mpya ya mabasi madogo iliyopo katika Manispaa ya Bukoba kutarahisisha usafiri na kuwawezesha kutekeleza shughuli zao kwa wakati huku wakisema stendi hiyo imeongeza hadhi na kuboresha mandhari ya Manispaa hiyo.
Wakazi hao wameyasema hayo wakati stendi hiyo ikifunguliwa na kuanza kutoa huduma rasmi ambapo wamesema uwepo wa stendi hiyo utapunguza msongamano na kuongeza ufanisi katika huduma za usafiri wa umma.
Edson Simoni dreva anayeendesha gari la abiria kutoka Bukoba mjini kwenda Mutukula amesema, kipindi cha nyuma stendi hiyo ilikuwa mbovu ila kwa sasa wanaishukuru serikali kwa kukamilisha stendi hiyo hakuna vumbi tena na hata mvua ikinyesha hapatakuwepo na matope.
Marius Stephano dreva wa haice itokayo Bukoba mjini kwenda Buyango amesema kuwa, anashukuru serikali kwa kuboresha stendi hiyo.
"Tulizoea stendi hii ilikuwa na tope wakati wa mvua na wakati wa kiangazi palijaa vumbi lakini kwa sasa adha zote hizo zimeisha tunaishukuru serikali kwa kujenga stendi hii maana ndiyo mlango wa mkoa wa Kagera" amesema Stephano.
Naye Asumpta Mushama amemshukru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa stendi hiyo na kuwa, kwao ilikuwa kilio kikubwa wakati wa kusafiri walikuwa wanapata shida lakini leo wamepata recodi mpya.
"Awali ya yote nashukuru kwa dizaini waliyojenga kwani ndani na nje yamewekwa maduka hivyo abiria watapata huduma mbalimbali"amesema Mushama
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Jacob Nkwera, amesema zaidi ya Tsh. Bilioni 1.5 zimetumika katika ujenzi wa stendi hiyo, ambayo inalenga kuboresha huduma mbalimbali za wananchi.
"Maduka 34 yamejengwa katika stendi hii, kuna sehemu za vinywaji, sehemu za vyakula na eneo ya kupumzika abiria wakiwa wanasubili usafiri"amesema Nkwera.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, amewataka watumiaji wa stendi hiyo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha huduma zinatolewa kwa utaratibu, usalama na ufanisi.

Post a Comment