HEADER AD

HEADER AD

WAZIRI ULEGA AWATAKA WAKURUGENZI BIHARAMULO, NGARA KUSHIRIKIANA NA TANROADS


Na Alodia Dominick, Kagera

WAZIRI wa ujenzi Abdallah Ulega amewataka wakurugenzi wa halmashauri za Biharamulo na Ngara kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Kagera pamoja na mkandarasi anayetekeleza ujenzi wa barabara ya rami ya Rusahunga- Rusumo mkoani Kagera kujenga maegesho ya maroli ili kuongeza uchumi wa wilaya hizo.

Waziri Ulega ameyasema hayo wakati akiwa mkoani Kagera akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya rami yenye urefu wa kilomita 92 inayotoka Rusahunga wilaya ya Biharamlo hadi Rusumo wilaya ya Ngara ambayom ujenzi wake umefikia asilimia 77 na itagharimu zaidi ya Tsh. Bilioni 200.

         Waziri Ulega akizungunza na Mkandarasi wa ujenzi wa barabara, wataalamu wa Tanroads na wakurugenzi wa halmadhsuri za Ngara na Biharamlo.

"Nawaagiza wakurugenzi wa halmashauri hizi mbili na wataalamu wetu wa TANROADS pamoja na mkandarasi anayejenga barabara hii kujenga maegesho ya magari makubwa ya mizigo ili wajasiliamali wetu wanaouza bidhaa mbalimbali katika senta zote waone faida ya uwepo wa barabara hii ya rami na halmashauri ziongeze mapato" amesema Waziri Ulega

Amesema barabara hiyo itakapokamilika ziwekwe taa katika senta zote ili kuwapa fursa wajasiliamali kufanya biashara zao hata majira ya usiku.

       Mbunge wa jimbo la Ngara Dotto Bahemu akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo.

Ameongeza kuwa, mradi huo unatarajia kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa watu na bidhaa ndani na nje ya nchi na kuwa ni sehemu ya mtandao wa barabara unaounganisha Tanzania na nchi jirani za Afrika Mashariki, 

Ameeleza  kuwa, Serikali ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imetoa tabasamu kwa wananchi wa mkoa wa Kagera kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya barabara kwa dhumuni la kuchochea ukuaji wa uchumi, kupunguza gharama za usafiri na kuongeza fursa za uwekezaji.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Hamza Faisary, amesema, mradi wa Rusahunga–Rusumo ni kati ya miradi saba inayotekelezwa katika Programu ya Tanzania Transport Integration Project (TanTIP), ikiwemo miradi minne ya barabara na mitatu ya viwanja vya ndege yenye thamani ya dola za Marekani milioni 550, sawa na fedha za kitanzania Sh trilioni 1.5.

        Kaimu mtendaji mkuu wa Tanroads Mhandisi  Hamza Faisary kulia kwake ni kaimu meneja wa Tanroads mkoa wa Kagera Mhandisi Festo  Julius.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Ramadhan Kido, ametoa shukrani kwa  Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuidhinisha zaidi ya Sh bilioni 500 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya  barabara mkoani humo.

Mbunge viti maalumu mkoa wa Kagera Devotha Daniel amesisitiza wananchi kuwa na amani kwani bila amani hakuna miradi ya maendeleo inayoweza kutekelezwa.

Amesema wananchi wanapaswa kuendelee kuitunza amani ya nchi hii kwani maendeleo yanayoonekana leo yanatokana na utulivu uliopo, bila amani, miradi mikubwa ya maendeleo isingeweza kutekelezwa kwa ufanisi 

Mbunge wa Jimbo la Ngara, Dotto Bahemu, amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutamaliza adha ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wananchi kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

        Mbunge wa jimbo la Ngara Dotto Bahemu akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo.

Bahemu amesema kuwa, kipande cha kilomita 60 kutoka Rusahunga hadi Ziroziro walikuwa wanasafiri zaidi ya masaa manne hadi sita, wapo wazee ambao wanaishi Dar es salaam walikuwa wanalazimika kusafiri kwa ndege hadi Rwanda alafu wanatoka Rwanda hadi Ngara zaidi ya kilomita 100 ili kukwepa kipande hicho amabacho kilikuwa kinapitika kwa shida.

Kaimu Meneja wa  Wakala wa Barabara Tanzania  (TANROADS) Mkoa wa Kagera, Mhandisi Festo Julius, amesema, mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo ulisainiwa Februari 18, 2023, na utekelezaji wake ulianza Julai 5 mwaka 2023, mradi umefikia asilimia 77 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika Desemba 10 mwaka huu.

       Devotha Daniel mbunge viti maalumu mkoa wa Kagera akizungumza na wananchi na kuwasisitiza kutunza amani.

No comments