CHUO CHA AFYA NA SAYANSI KIBAHA KINAKABILIWA NA UCHAKAVU WA MAJENGO, MEYA DKT. MAWAZO ASEMA JAMBO

Na Gustaphu Haule, Pwani
MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt. Mawazo Nicas ameahidi kushirikiana na uongozi wa chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha kwa ajili ya kujenga jengo la kisasa la ghorofa Sita ili kuhakikisha chuo hicho kinakuwa na miundombinu mizuri inayoendana na wakati uliopo.
Dkt . Nicas amemuomba Mkuu wa Chuo hicho Tusekile Solile kutafuta timu ya wataalamu ( Technical Team)ambayo watadrafti ramani ya jengo hilo lenye kugharimu kiasi cha Tsh. Bilioni 6 ili liweze kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.
Dkt . Nicas ameuagiza uongozi wa chuo hicho kuandaa harambee maalum kwa ajili ya kupata kiasi cha Tsh. Milioni 150 ili waweze kununua basi la chuo kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wa Chuo hicho usafiri wa kwenda katika masomo ya vitendo katika hospitali mbalimbali.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akikagua miundombinu ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha alipowasili chuoni hapo Julai 24 /2026 .Dkt.Nicas alibainisha hayo Julai 24/2026 wakati akizungumza na uongozi wa chuo hicho na wazazi katika mahafali ya 59 ya Chuo hicho kwa wahitimu wa kozi ya Uuguzi,Ukunga na Utabibu yaliyofanyika katika viwanja vya mpira wa miguu vya Shirika la Elimu Kibaha ( KEC).
Dkt.Nicas alifikia hatua hiyo baada ya kupokea changamoto mbalimbali za Chuo hicho kutoka kwa Mkuu wa Chuo Tusekile Solile ambaye alibainisha kuwa miundombinu ya Chuo hicho ni chakavu kwani hadi sasa imefikia miaka 58 bila ukarabati wowote, ukosefu wa usafiri wa kuwapeleka wanafunzi katika masomo ya vitendo na hata kukosa maji ya uhakika.
Katika hotuba yake Dkt.Nicas amesema kuwa miaka 58 ni mingi kwani miundombinu iliyopo ni dhahiri inapaswa kubadilishwa na kwamba yeye yupo tayari kushiriki katika ujenzi wa miundombinu hiyo ili chuo hicho kipate majengo ya kisasa .
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas wa pili kutoka kushoto akiwa tayari kupokea maandamano ya wahitimu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha katika mahafali ya 59 yaliyofanyika Julai 24/2026 katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha.Amesema yeye ni miongoni mwa wanafunzi waliopita katika Chuo hicho na anawafahamu watu wengi ambao wengine ni Waganga Wakuu na kwamba kwa umoja wao watahakikisha wanapata fedha kiasi cha Sh.bilioni 6 kwa ajili ya kujenga jengo moja kubwa la ghorofa Sita katika Chuo hicho.
Amesema kwa uwingi wa wanafunzi waliopita katika Chuo hicho kama kila mmoja akatoa kiasi cha Sh .100,000 ni wazi kuwa fedha hizo watazipata na jengo litajengwa ambapo hatahivyo amempongeza Mkuu wa Chuo hicho kwakufanyakazi nzuri licha ya kuwa miundombinu yake ni chakavu.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa Chuo hicho na bado inaweka nguvu Katika kuviimarisha vyuo vya Afya na Sayansi hapa nchini lakini lazima waishukuru Serikali ya awamu ya Sita kwa kazi nzuri inayofanya.
Dkt. Nicas amesema katika Serikali za awamu zote hakuna awamu iliyofanya maendeleo kwa kasi kubwa kama Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwani kila mahali pamejengwa Zahanati na Vituo vya afya .
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akiwa katika mahali ya 59 ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha yaliyofanyika Julai 24/2026.Amesema katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kuna vituo vya afya zaidi ya vitano vimejengwa na Zahanati zaidi ya tisa na hayo yamefanyika katika nchi nzima na kwamba hilo ni jambo ambalo linapaswa kumpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anayoifanya .
Dkt Nicas. amewapongeza wahitimu hao na kuwataka waende kuzitendea haki taaluma zao kwa kuzingatia uadilifu,maadili ya kazi kwani wakati mwingine tabasamu la Wauguzi,Wakunga na Matabibu ndio nafuu kwa wagonjwa.
Amewaomba wahitimu hao kwenda kuwa mabalozi wazuri wakukitangaza chuo hicho kwakufanyakazi vizuri huku akiwataka mara wanapoondoka chuoni hapo waanze kuomba nafasi za kujitolea ili waonyeshe ujuzi wao na kupata uzoefu njia ambayo itakuwa rahisi kwao kupata ajira.
Wahitimu wa Kozi ya Uuguzi,Ukunga na Utabibu katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha.Amesema kwa wale ambao wanataka kujiajiri bado Serikali imewapa fursa kwakuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameagiza kuendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa Vijana, Wanawake na Watu wenye ulemavu kwahiyo wao kama vijana wanaweza kutumia fursa hiyo kwa kuunda vikundi ili waweze kuomba mikopo ambayo itawasaidia kununua vifaa vya kutolea huduma.
Naye Mkuu wa Chuo hicho Dkt.Tusekile Solile amesema anaishukuru Serikali kupitia Wizara ya Afya na Baraza la Elimu ya Ufundi na Ufundi Stadi kwa kuendelea kusimamia na kutoa miongozo mbalimbali ya afya na mafunzo.
Dkt.Solile amesema kuwa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha kilianzishwa mwaka 1968 ambapo kilianza na kutoa kozi ya Waganga wasaidizi Vijijini kama sehemu ya kukabiliana na Ujinga,Maladhi na Umaskini .
Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha Tusekile Solile.Amesema kwasasa Chuo kinatoa Kozi ndefu za Uuguzi,Ukunga na Utabibu pamoja na kozi fupi ya miezi mitatu ya Uuguzi ngazi ya Jamii na kwamba katika kozi hizo mwaka huu wamehitimu wanafunzi 192 kati yao Wauguzi na Wakunga 92 na Utabibu wanafunzi 100.
Amesema miongoni mwa mafanikio ya Chuo hicho ni kuzalisha wataalamu wengi zaidi ambao wanatoa huduma katika vituo mbalimbali vya afya na kwamba katika kipindi cha mwaka 2023/2025 zaidi ya wahitimu 2,250 wametoka katika Chuo hicho.
Amesema anaishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwakuwa imefanya mengi makubwa na kwamba katika sekta ya afya wamekuwa wanufaika wakubwa kwani Zahanati na Vituo vya afya vilivyojengwa vimekuwa vikitoa nafasi kwa Wauguzi, Wakunga Matabibu kutoa huduma katika vituo hivyo.
Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas ( katikati) akitembelea chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha Julai 24/2026.Amesema pamoja na mafanikio hayo, lakini zipo changamoto za Chuo hicho ni uchakavu na uhaba wa miundombinu, ukosefu wa vyumba vya kusomea na maabara,na basi la chuo japo wameanza kuzifanyiakazi baadhi ya changamoto ikiwemo ya kujenga chumba cha kompyuta kinachoweza kuingiza wanafunzi 54.
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha( KEC) Khalfan Feruzi amesema fani ya afya ni muhimu kwani bila afya hakuna uzalishaji hivyo amewataka wahitimu hao kwenda kufanyakazi kwa kuzingatia hofu ya Mungu na maadili ya kazi na kuwasihi waepuke rushwa .
Hata hivyo, Feruzi amewapongeza wahitimu wa Chuo hicho,wakufunzi na watumishi wote wa Shirika la Elimu Kibaha na hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa namna ambavyo walitoa ushirikiano kuhakikisha wanafunzi hao wanafanya vizuri katika masomo yao .
Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Khalfan Feruzi ( Kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas (katikati) pamoja na Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha Tusekile Solile.





Post a Comment