HEADER AD

HEADER AD

HALMASHAURI KIBAHA YAWAHAKIKISHIA WAFANYABIASHARA KUTATUA KERO ZAO


Na Gustaphu Haule, Pwani

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kibaha imewahakikishia wafanyabiashara waliopo ndani ya Manispaa hiyo kuwa changamoto na kero zote za kibiashara zinazowakabili zinakwenda kupata ufumbuzi ili waweze kufanya biashara zao katika mazingira mazuri zaidi.

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon amewahakikishia wafanyabiashara hao  wakati akifungua  mkutano wa pamoja baina ya wafanyabiashara na viongozi wa Manispaa ya Kibaha uliofanyika Julai 15,2026 katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha kwa Mfipa.

         Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon akifungua Mkutano wa wafanyabiashara uliofanyika Julai 15,2026 chini ya maandalizi ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.

Mkutano huo wa siku moja uliandaliwa na Manispaa ya Kibaha kwa ajili ya kufanya tathmini ya ukuaji wa biashara katika kipindi cha mwaka 2025/ 2026 pamoja kueleza fursa mbalimbali za kibiashara zilizopo katika Manispaa ya Kibaha.

Katika Mkutano huo Saimoni amesema sekta binafsi ndio sekta mama katika Manispaa hiyo hivyo ni kazi ya serikali kuhakikisha wazalishaji wanakuwa katika mazingira mazuri ya shughuli zao.

        Wafanyabiashara wa Manispaa ya Kibaha wakiwa katika mkutano wa pamoja na viongozi wa Halmashauri hiyo uliolenga kujadili changamoto mbalimbali za kibiashara.

Amesema kuwa bajeti ya Serikali ipo chini ya sekta binafsi na hata katika mapato sekta binafsi ndio zinachangia mapato makubwa zaidi kwahiyo kazi kubwa iliyopo mbele ni kuhakikisha wafanyabiashara wa sekta binafsi wanakuwa katika mazingira mazuri.

Amesema kuwa sekta binafsi ni ndio moyo wa Tanzania na kwenye uchumi ndio wachangiaji wakubwa kwahiyo Serikali imekuwa ikitoa nafasi kwa  wafanyabiashara ili waweze kuzalisha zaidi.

       Wafanyabiashara wa Manispaa ya Kibaha katika mkutano wao maalum ulioandaliwa na Halmashauri ya Manispaa Julai 15,2026 katika  Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha kwa Mfipa.

Amesema msingi ni kuhakikisha sekta binafsi inakuzwa ili iweze kunufaisha Watanzania hususani katika uchumi,ajira na kuongeza pato la Taifa ndio maana Serikali imekuwa ikiwekeza nguvu kubwa sekta binafsi kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara.

"Asilimia kubwa ya mapato yetu yanatoka kwa wafanyabiashara na sekta binafsi inaibeba Kibaha, ni jukumu letu Serikali ambao ni walezi wa sekta binafsi kuhakikisha tunaweka mazingira mazuri ya kufanyia biashara ambayo yatakuza mapato yetu,"amesema Saimon

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt. Mawazo Nicas amesema kukutana na wafanyabiashara hao ni sehemu ya kujadili kwa pamoja  mafanikio na vikwazo vyao kwani kundi hilo ndio wachangiaji wakubwa wa pato la Taifa.

        Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akizungumza na wafanyabiashara wa Manispaa hiyo katika mkutano uliofanyika Julai 15,2026.

"Wafanyabiashara ndio wadau wakubwa wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha na leo tumekutana hapa  kusikiliza kero na changamoto zao ili nasisi kama Manispaa tuone namna ya kuzitatua ili  tunapoanza mwaka huu wa fedha  tuendelee kuinua mapato yetu," amesema Dk.Nicas.

Amesema Halmashauri hiyo inakwenda kupeleka miundombinu wezeshe kwenye maeneo ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji huku wakiwa na mkakati wa kusimamia kipaumbele cha vijana wa Manispaa hiyo kupata ajira.

"Huu uwekezaji unatakiwa uwanufaishe wakazi wa Kibaha, tumekubaliana kukaa na wawekezaji na kujadiliana nao ili vijana wazawa waweze kupewa kipaumbele cha ajira na tuangalie fani zinazohitajika zaidi ili tuwaandae vijana wetu," amesisitiza.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa amewashukuru wafanyabiashara hao kwa namna wanavyochangia ukuaji wa mapato ya Manispaa hiyo.

        Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Rogers Shemwelekwa akizungumza na wafanyabiashara katika mkutano uliofanyika Julai 15,2026 katika Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha kwa Mfipa.

Dk.Shemwelekwa  amesema mapato yanayokusanywa yamekuwa yakitumika kujenga shule, zahanati na kupeleka huduma nyingine kwa wananchi ikiwemo maji kuwaondolea wananchi kero pamoja na kulipa fidia.

Shemwelekwa amewataka wafanyabiashara hao kuboresha biashara zao sambamba na kuwa wabunifu ili bidhaa zao ziingie kwenye ushindani wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo baadhi ya  wafanyabiashara hao akiwemo Henry Mgala ameomba Manispaa hiyo kuwaboreshea barabara za kwenye mitaa yao ili wateja wafike kwa urahisi.

Pia Mgala ameomba maboresho kufanyika kwenye eneo la Nishati ya umeme kwani baadhi ya maeneo umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara na kusababisha hasara ya vifaa vya kufanyia biashara.


No comments