DC KIBAHA AZINDUA CHANJO KWA WATOTO CHINI YA MIAKA 10 ILI KUJIKINGA NA UGONJWA WA POLIO
Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amezindua kampeni ya utoaji wa chanjo ya matone kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10 ikiwa ni kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa wa Polio aina ya pili.
John amezindua kampeni hiyo Agosti 27/2026 katika kituo cha afya Mkoani kilichopo Kata ya Tumbi Manispaa ya Kibaha uzinduzi ambao uliwashirikisha wanafunzi 1,208 kutoka shule mbalimbali za Msingi.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John akizindua kampeni ya chanjo ya Polio kwa watoto chini ya umri wa miaka 10 uliofanyika katika kituo cha afya Mkoani Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani Agosti 27/2026.Wanafunzi walioshiriki uzinduzi huo wametoka katika Shule ya Msingi Mkoani , Shule ya Msingi Kambarage na Shule ya Msingi Kibaha Independent ambao wote walipata chanjo hiyo.
Akizungumza wakati akizindua kampeni hiyo John amesema kampeni ya kutoa chanjo hiyo itafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inaanza Agosti 27 hadi Agosti 30 na awamu ya pili itaanza Septamba 29 hadi Oktoba 02/2026.
Utoaji wa chanjo ya Polio kwa watoto uliofanyika katika kituo cha afya Mkoani Kata ya Tumbi Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani Agosti 27/2026.Amesema malengo ni chanjo kuwafikia watoto wote waliopangwa kufikiwa huku lengo lingine ni kuhakikisha jamii inashirikiana katika kampeni hiyo.
John amesema katika uzinduzi wa kampeni hiyo watoto 1,208 wamepewa chanjo hiyo na hiyo ni ishara kwamba Mkoa wa Pwani unakwenda kufanikiwa kwa kuwapatia chanjo watoto wote.
Muuguzi wa kituo cha Afya Mkoani katika Manispaa ya Kibaha akitoa chanjo ya Polio kwa mtoto mara baada ya uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika chini ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John."Malengo ya Mkoa wa Pwani ni kutoa chanjo kwa watoto zaidi ya 587,509 na Chanjo hiyo inatolewa kwa awamu mbili na ishara zote zinaonyesha kuwa wanakwenda kufanikiwa kama ilivyopangwa ," amesema John.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Kusirye Ukio amesema kuwa maandalizi ya utoaji wa chanjo hiyo yalianza Agosti 17/2026 ambapo kazi iliyopo mbele ni ndogo kwakuwa walishirikisha jamii.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Kusirye Ukio wa kwanza kushoto katika uzinduzi wa kampeni ya utoaji wa chanjo ya Polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka 10 iliyofanyika Agosti 27/2026 katika kituo cha afya Mkoani Kata ya Tumbi Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani.Ukio amesema kuwa anawashukuru Wakuu wa Wilaya,Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani,Wizara ya Afya pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Amesema anawashukuru viongozi hao kwasababu ya maandalizi na umuhimu wa chanjo hiyo kwa Taifa kwa ajili ya kuwakinga watoto dhidi ugonjwa wa Polio ambayo itatolewa kwa awamu mbili .
Afisa kutoka Wizara ya Afya Kitengo cha Chanjo Juma Fadhili amesema kuwa kwa awamu ya kwanza chanjo hiyo ilianza kutolewa katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa Machi mwaka huu.
Afisa kutoka Wizara ya Afya Kitengo cha Chanjo Fadhili Juma akizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya chanjo ya Polio uliofanyika Agosti 27/2026 Kibaha Mkoani Pwani.Fadhili amesema kwasasa chanjo hiyo inatolewa kwa Mikoa nane ukiwemo Mkoa wa Pwani, Mkoa wa Dar es Salaam,Mkoa wa Manyara, Kilimanjaro, Arusha,Mara,Tanga ,Dodoma na baadae kumalizia Mikoa mingine sita iliyobaki.
Hata hivyo, Fadhili amewaomba Wazazi,walezi , Wananchi na jamii kiujumla kujitokeza kwa wingi katika kuhakikisha wanawapeleka watoto wao kupata chanjo hiyo ili kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa Polio ambao hauna tiba pale ambapo mtoto anaupata.







Post a Comment