WATUMISHI WA AFYA KAGERA WAFANYA TUKIO LA UTAYARI KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO
Alodia Dominick, Bukoba
Kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa ebora ambao umeendelea kushambulia wananchi nchini Congo, watumishi wa afya mkoani Kagera wamepatiwa mafunzo ya utayari kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Ebora ili ikitokea hapa nchini wawe na uelewa mpana.
Mafunzo hayo ya utayari yamefanyika Augosti 26, 2026 katika hospital ya wilaya halmashauri ya Bukoba ambapo wamefanya tukio la utayari na wataalamu wa afya wameelezwa maswala mbalimbali ikiwemo mapokezi ya mhisiwa au mgonjwa endapo akitokea katika vituo vyao.
Madaktari wakijifunza jinsi ya kuvua mavazi baada ya kumuhudumia mhisiwa wa Ebora.Mafunzo ya utayari yaliyotolewa kwa wataalamu wa afya ni pamoja na jinsi ya kupokea mhisiwa wa mlipuko wa ebora na wataalamu wanapopokea mhisiwa jinsi ya kumpatia matibabu/vipimo na baada ya kutoa huduma namna ya kuvua mavazi.
Baada ya kutoa mafunzo ya utayari baadhi ya wataalamu kutoka wizara ya afya na wadau wengine wa afya wamezungumza na waandishi wa habari na kueleza maelengo ya mafunzo hayo.
Afisa Muuguzi wizara ya afya na mratibu wa magonjwa ya mlipuko Theresia Haule ametaja lengo la kuwa Kagera ni kujenga uwezo kwa watumishi, kuangalia ni namna gani wenzao wana utayari wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.
"Katika kipindi cha wiki mbili ambacho tumekuwa Kagera kuanzia Augosti 17 hadi Augosti 28,2026 tumetembelea na tutaendelea kutembelea hospitali zote za mkoa wa Kagera lakini hii yote ni kuonyesha kwamba ni namna gani watumishi wa afya wameweza kujiandaa na magonjwa ya mlipuko" amesema Haule
Amesema kuwa, mlipuko wa ebora haujaingia nchini Tanzania lakini kutokana na mkoa wa Kagera kuwa mpakani serikali imeona ni vyema kuwapatia mafunzo ya utayari watumishi wa afya ili wawe tayari ikitokea mlipuko wawe na uelewa mpana.
Mwakilishi wa mganga mkuu wa mkoa Kagera Dr Pascal Peter ameeleza kuwa, mkoa kwa kushirikiana na Wizara ya afya wameendelea kuwajengea uwezo watumishi wa afya katika halmashauri zote nane za mkoa huo ikijumuisha timu za afya za mkoa katika mapambano ya magonjwa ya mlipuko .
Tukio la mafunzo ya utayari madaktari wakipokea mhisiwa kutoka katika gari la wagonjwaDr Peter ameeleza kuwa, kutokana na mkoa wa Kagera kuwa mpakani walikuwa na uhitaji mkubwa wa mafunzo kwa watumishi wa afya kwani wamepata uelewa jinsi ya kujikinga endapo atapatikana mgonjwa wa ebora na jinsi ya kutoa huduma kwa mgonjwa au mhisiwa.
Mmoja wa waliopata mafunzo hayo mganga mfawidhi hospitali ya wilaya Kyerwa Dr Richard Protas Sangu ameeleza kuwa, mafunzo yamewajengea uwezo maeneo tofauti ikiwemo jinsi ya kumpokea mhisiwa, jinsi ya kujikinga mtumishi wa afya na baada ya kutoa huduma kwa mhisiwa jinsi ya kuvua mavazi.
"Mbali na sisi kujengewa uwezo pia tutatoa mafunzo haya kwa wataalamu wa afya ambao wako kwenye hospitali zetu jinsi ya kumpokea mhisiwa wa ebora na magonjwa mengine ya mlipuko na namna mtaalamu anavyopaswa kujikinga yeye mwenyewe" amesema Dr.Sangu
Meneja IPC, Mradi wa Usalama wa Afya Duniani, unaotekelezwa na CIHEB- Tanzania kupitia serikali ya Marekani Christina Mmasa amesema kuwa, wataalamu wa afya waliopata mafunzo kwa vitendo wazingatie mafunzo hayo.



Post a Comment