KATIBU UVCCM KATA YA TANGINI AWASHIKA MKONO WAJASIRIAMALI , ELINA MGONJA ATIA NENO
Na Gustaphu Haule, Pwani
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi ( UWT) Kibaha Mjini Elina Mgonja amelazimika kutoa machozi ya furaha baada ya Katibu wa Umoja wa Vijana( UVCCM) Kata ya Tangini Lazaro Benjamini kuwachangia fedha Tsh.100,000 Wanawake wajasiriamali ili waweze nunua malighafi za kutengenezea Vitenge vya Batiki,Sabuni na bidhaa nyingine.
Mbali na Benjamin kutoa fedha hizo Lakini pia amemkabidhi mwenyekiti huyo treyi mbili za Mayai ikiwa sehemu ya zawadi kwa ajili ya kujitoa kwake na kuwafundisha bure Wanawake hao masuala ya ujasiriamali.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Kata ya Tangini (kulia) akimkabidhi mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja treyi mbili za Mayai hafla iliyofanyika Agosti 14/2026.
Benjamini amekabidhi fedha na Mayai kwa Mwenyekiti huyo Agosti 14, 2026 mbele ya Wanawake wa Kata ya Tangini katika mafunzo ya ujasiriamali ambayo yalikuwa yakifanyika katika ukumbi wa ofisi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Tangini Manispaa ya Kibaha.
Awali akizungumza kabla ya makabidhiano hayo Benjamini amesema kuwa amefurahishwa na hatua ya mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini kujitoa katika kuhakikisha anawapa ujuzi Wanawake wa Kata ya Tangini kupitia mafunzo ya ujasiriamali.
Benjamini amesema tangu ameingia katika Siasa amekuwa akimuona mwenyekiti huyo akifanyakazi kwa vitendo akipita kila Kata kuwafundisha Wanawake mafunzo ya ujasiriamali jambo ambalo ndio msingi wa kuwainua kiuchumi.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM Kata ya Tangini Lazaro Benjamin akiangalia Sabuni iliyotengenezwa na Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja alipokuwa anawafundisha Wanawake wa Kata hiyo Agosti 14/2026.
Amesema ameona baada ya kumaliza mafunzo hayo Wanawake wanapaswa kuendeleza ujuzi waliohupata lakini ni vyema wakapata kianzio cha kununua malighafi au kununua vitabu vya kujisomea zaidi ujuzi huo.
Amesema kwa kutambua juhudi za mwenyekiti huyo ameona atoe kiasi cha Sh ,100,000 kwa ajili kuwachangia Wanawake hao lakini pia ni sehemu ya kumtia nguvu mwenyekiti katika kuendeleza moyo wa uzalendo wa kufundisha zaidi.
Mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika Agosti 14 kwa Wanawake wa Kata ya Tangini chini mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja.
"Niliona nipite hapa kuangalia namna mafunzo yanavyoendelea lakini kiukweli nimefurahi kuona mafunzo haya ni mazuri na mimi nataka Wanawake waendelee kuyatumia mafunzo haya na leo nawachangia Sh.100,000 ili mkanunue malighafi au vitabu ,"amesema Benjamini.
Benjamini amesema amewiwa sana na Wanawake wa UWT Kata ya Tangini waliojitokeza katika jambo hilo ambapo amewaomba waende kuyatumia kwa vitendo mafunzo hayo na kama kuna changamoto yoyote ya kupata malighafi basi ni vyema wakamshirikisha.
Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja amemshukuru Benjamini kwa moyo wake wa kujitolea hususani katika kuwasaidia Wanawake wa UWT Kata ya Tangini.
Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja akiwafundisha Wanawake wa Kata ya Tangini kutengeneza Sabuni, mafunzo hayo yaliyofanyika Agosti 14/2026 katika ofisi za CCM za Kata hiyo.
Amesema kijana huyo ameonyesha moyo wa upendo na uzalendo kwani licha ya kutoa Mayai lakini ametoa fedha huku akisema fedha kipindi ni ngumu lakini kijana huyo amekubali kujitoa.
Mgonja ameahidi kumpa ushirikiano Katibu huyo kwa jambo lolote na hata kama kuna suala la kutoa elimu ya ujasiriamali kwa vijana yeye atakuwa tayari kujitoa kwa ajili yake.
Ameongeza kuwa, kutokana na hali hiyo ameahidi kurudi tena Kata ya Tangini kwa ajili ya kuwafundisha zaidi Wanawake hao kuhusu utengenezaji wa vitenge vya Batiki na bidhaa nyingine mbalimbali.





Post a Comment