MWENYEKITI UWT KIBAHA ATOA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KWA WANAWAKE KATA YA PICHA YA NDEGE, SOFU
>>Elina Mgonja awahimiza Wanawake kuongeza bidii katika kufanya shughuli za kiuchumi
Na Gustaphu Haule,Pwani
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Kibaha Mjini Elina Mgonja amewapa mafunzo ya ujasiriamali Wanawake wa Kata ya Picha ya Ndege pamoja na Kata ya Sofu huku akiwataka Wanawake hao kuongeza bidii katika kufanya shughuli za kiuchumi.
Mgonja, ametoa wito huo Agosti 13/2026 katika mafunzo ya kuwajengea uwezo Wanawake kuhusu masuala mbalimbali ya ujasiriamali yaliyofanyika katika Kata ya Picha ya Ndege na Kata ya Sofu zilizopo katika Manispaa ya Kibaha .
Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja (pichani).Mgonja anaendelea na ziara yake ya kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa Wanawake wa Kibaha Mjini ambapo hadi sasa tayari amefanikiwa kuwafikia Wanawake zaidi ya 900 katika Kata 11 kati ya Kata 14 za Manispaa ya Kibaha.
Kata alizofanikiwa kupita hadi sasa ni pamoja na Kata ya Msangani,Kata ya Mkuza,Kata ya Mailimoja,Kata ya Tumbi,Kata ya Kongowe, Misugusugu,Visiga ,Viziwaziwa ,Sofu,Picha ya Ndege, Kibaha na ambapo Agosti 14 atapita katika Kata ya Tangini na baadae kumalizia katika Kata ya Mbwawa na Pangani.
Mafunzo ya ujasiriamali yakifanyika Kata ya Sofu Agosti 13/2026 chini ya Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja.Akizungumza wakati akitoa mafunzo hayo Mgonja amesema kuwa Mwanamke anapaswa kujituma katika kufanya shughuli ambazo zitasaidia familia kuongeza kipato .
Amesema wapo Wanawake wengine wanabweteka kwa kukaa nyumbani kwasababu tu mume wake anafanyakazi na anauhakika wa kula na kuishi vizuri jambo ambalo sio sawa kwa maisha ya sasa.
Mgonja amesema kuwa maisha yanabadilika na kwamba hata huyo mwanaume unayemtegemea kuna siku atastaafu kazi na kubaki nyumbani hali ambayo itapelekea kutumia pensheni ambayo haiwezi kutosheleza kukidhi mahitaji yote ya nyumbani.
Amesema hatua hiyo inasababisha migogoro ya ndani ya nyumba kila siku kwakuwa tu Mwanamke huna chakufanya lakini kama utakuwa umezoea kujishughulisha ni wazi kuwa hata Wanaume zao mambo yakiwaendea vibaya wao wanachukua nafasi ya kusaidia familia.
Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja aliyekaa kwenye kiti akiwafundisha Wanawake wa Kata ya Sofu kutengeneza Sabuni za aina mbalimbali Agosti 13/2026.Ameongeza kuwa ,kama umejitoa kujishughulisha na masuala ya ujasiriamali halafu Mwanaume akaona unafanya kitu nyumbani kwa ajili ya familia ni wazi kuwa hakutakuwa na ugomvi na badala yake Mwanaume atakuwa na amani ya kuwaruhusu kufanya shughuli hizo bila vipingamizi.
"Mimi mume wangu amestaafu miaka mingi lakini nilianza kuwa mjasiriamali kipindi ambacho yeye anafanyakazi na wakati huo aliona namna ambavyo ninachangia majukumu ya nyumbani na akaona bora aniruhusu niendelea kuwa mjasiriamali lakini leo amestaafu na anakula matunda ya Mke wake ,"amesema Mgonja .
Mgonja , amesema kama kuna mwanamke alikuwa wakukaa nyumbani basi kuanza sasa waanze waamke na kuchangamkia fursa na fursa mojawapo ni kuhakikisha wanakwenda kuyatumia vizuri mafunzo ya ujasiriamali anayoyatoa.
Wanawake wa Kata ya Sofu wakishangalia mara baada ya kumaliza kutengeneza Vitenge vya Batiki katika mafunzo yaliyotolewa Agosti 13/2026 na Mwenyekiti wa UWT Elina Mgonja.Mgonja amesema kuwa anafanya hivyo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwakuwa amekuwa akiweka mipango mbalimbali ya kuwakomboa Wanawake hapa nchini.
Amewapongeza Wanawake wa UWT Kata ya Picha ya Ndege na Kata ya Sofu kwa kujitoa kwa wingi kushiriki mafunzo hayo huku akiahidi kuwa atarudi tena katika Kata hizo kwa ajili ya kuwaongezea ujuzi zaidi wa masuala ya ujasiriamali.
Diwani wa Kata ya Sofu Mashaka Mahande ,amemshukuru mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja kwa kazi kubwa anayoifanya hususani kwa kuwapa mafunzo Wanawake waliopo katika Kata yake.
Diwani wa Kata ya Sofu katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Mashaka Mahande akizungumza na Wanawake katika mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika ndani ya Kata hiyo Agosti 13/2026.Mahande amesema anaamini kupitia mafunzo hayo Wanawake wengi watakuwa wamepata shughuli za kufanya ambazo kwa kiasi kikubwa zitawasaidia kuongeza kipato katika familia zao.
Amesema Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha inatoa mikopo ya asilimia 10 na Wanawake ni wanufaika namba moja kwahiyo baada ya mafunzo hayo wajitahidi kuchangamkia fursa hiyo kwakuwa tayari watakuwa na jambo la kufanya .
Amesema,mikopo ya Halmashauri inatolewa kwa njia ya vikundi lakini kwa watu wenye ulemavu hata mtu mmoja anapata na kwamba wahakikishe wanaunda vikundi ili wawe na sifa ya kukopesheka.
Washiriki wa mafunzo ya ujasiriamali wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kutengeneza Vitenge vya Batiki Agosti 13/2026 katika Kata ya Picha ya Ndege."Undeni vikundi lakini hakikisheni mnajuana kwani kuna vikundi vinaundwa na watu ambao hawafahamiani halafu mwisho wa siku wanapopata fedha za mkopo wengine wanakimbia na kuwaachia wenzao matatizo,"amesema Mahande.
Hata hivyo,Mahande amesema kuwa yeye yupo tayari kutoa ushirikiano kwa Mwanamke au vikundi vya Wanawake ambavyo vitakuwa vinajishughulisha na masuala ya ujasiriamali ikiwa kwa kuwapa nguvu katika kuendeleza shughuli zao.
Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja aliyechuchumaa kushoto akishangilia baada ya kutengeneza Vitenge vya Batiki katika mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika Kata ya Sofu Agosti 13/2026.






Post a Comment