MCHENGERWA AKABIDHI GARI LA KUBEBA WAGONJWA WILAYA YA KIBAHA LENYE THAMANI YA TSH. MILIONI 100

Na Gustaphu Haule, Pwani
WAZIRI wa Afya Mohamed Mchengerwa amekabidhi gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) lenye thamani ya sh .milioni 100.5 kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kwa ajili ya kutolewa huduma za dharula kwa Wananchi waliopo katika Halmashauri hiyo.
Mchengerwa amekabidhi gari hilo Agosti 24/2026 katika hafla iliyofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani iliyopo katika Mji mdogo wa Mlandizi hafla ambayo ilishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali pamoja na Wananchi wa Kibaha Vijijini.
Gari jipya la Wagonjwa lililokabidhiwa Agosti 24/2026 na Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa kwa ajili ya kutoa huduma ya dharula kwa Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha .Miongoni mwa viongozi walioshuhudia hafla hiyo ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa,Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge,Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon na baadhi ya viongozi wa CCM katika Wilaya hiyo akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkali Kanusu.
Kupatikana kwa gari hilo ni jitihada za Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa ( Mzee wa Sambusa) ambaye alipeleka maombi kwa Waziri wa Afya miezi michache iliyopita na kumueleza changamoto ya ukosefu wa magari ya wagonjwa katika Jimbo lake.
Akizungumza katika hafla hiyo Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa ( Mzee wa Sambusa) amesema kuwa gari hilo halikuja hivihivi kwani zipo juhudi alizifanya hadi kuweza kupata gari hilo .
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa (Mzee wa Sambusa) akizungumza katika hafla ya mapokezi ya gari jipya la Wagonjwa kutoka kwa Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa.Jumaa ,amesema kuwa siku chache zilizopita alipata nafasi ya kukutana na Waziri Mchengerwa na ndipo akamueleza shida ya ukosefu wa gari la Wagonjwa katika Jimbo lake na akakubali kulifanyiakazi jambo hilo.
Jumaa amesema anamshukuru Waziri Mchengerwa kwa kukubali ombi lake na kisha kulifanyiakazi na hatimaye kufanikisha kupata gari hilo ambalo litakwenda kuwasaidia Wananchi wa Jimbo la Kibaha Vijijini katika kusafirisha wagonjwa pale wanapougua.
Jumaa katika hafla hiyo mbali na kukabidhiwa gari hilo lakini pia ametumia nafasi hiyo kumuomba Waziri huyo kusaidia katika ujenzi wa uzio katika hospitali ya Wilaya pamoja na kujenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mlandizi - Ruvu hadi Mzenga.
Jumaa amemshukuru Rais wa awamu ya Sita Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya katika Taifa na kwamba wakati anaingia madarakani watu wengi walidhani hatoweza lakini kwa muda wote huo ameonyesha kwa vitendo kuwa anaweza na kazi zinafanyika.
Jumaa amesema kuwa moja ya historia aliyoiandika Rais Samia ni ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Mwalimu Nyerere kilichopo Rufiji Mkoani Pwani (JNHPP) mradi ambao ulianzishwa na mtangulizi wake Hayyat John Magufuli.
Amesema wengi wakisema mradi huo utakwama lakini Rais Samia Suluhu Hassan ameusimamia vyema hadi kukamilika na hatimaye kuzinduliwa Agosti 22/2026 ukiwa umetumia fedha za ndani kiasi cha Tsh .Trilioni 7.4.
Jumaa ameongeza kuwa si tu Rais Samia amekamilisha kituo hicho cha umeme lakini amefanikiwa kikamilifu reli ya Mwendokasi ( SGR) na kuanzisha ujenzi mwingine wa SGR kutoka Tabora hadi Kigoma sambamba na kukamilisha mradi mkubwa wa daraja la Bugongo - Busisi.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa amemshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa iliyotukuka kwa kuwaletea Wananchi maendeleo huku akisema Mkoa wa Pwani umepokea fedha kiasi cha Trilioni 1.7 .
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika hafla ya mapokezi ya gari jipya la Wagonjwa la Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha.Kunenge amesema fedha hizo zimesaidia kujenga miundombinu ya kutolea huduma za afya 635 ikiwemo hospitali ya Rufaa 1,hospitali za Wilaya 14,vituo vya afya 62, Zahanati 442,kliniki 18,wodi za Wazazi 07, maabara 106 huku upatikanaji wa dawa ukifikia asilimia 89.
Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa amesema kuwa kukabidhi gari hilo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi kupitia sekta ya afya lakini wanatekeleza dira ya 2050 iliyoanzishwa chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Mchengerwa amesema kuwa dhamira ya Rais Samia ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora ya matibabu na ndio maana kila siku kumekuwa na mipango ya kuhakikisha miundombinu inajengwa sambamba na kuweka dawa pamoja na vifaa tiba vya kutosha .
Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa akizungumza katika hafla ya kukabidhi gari la Wagonjwa la Halmashauri ya Kibaha Vijijini Agosti 24/2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani Mlandizi Pwani Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge (katikati) akimpokea Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa katika hafla ya mapokezi ya gari jipya la wagonjwa iliyofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani Halmashauri ya Kibaha Vijijini na watatu mwenye shati nyeupe ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa.Mchengerwa amesema kuwa awamu hii yametoka magari 10 ya wagonjwa lakini aliona gari moja likabidhiwe Kibaha Vijijini kutokana na maombi ya Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa.
Ameomba gari hilo litumike kwa kazi iliyokusudiwa na lisitumike kwa shughuli nyingine za kiutawala huku akimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani kuhakikisha anaitisha magari yote mabovu ya kubebea wagonjwa na kisha kuyafanyia tathmini ili kujua mahitaji yake.
Amesema amepokea changamoto ya uhitaji mkubwa wa magari ya wagonjwa katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini na kwamba jambo hilo litafanyiwa kazi huku akisema awamu ijayo ataona namna ya kuwaongezea magari .
"Nimepokea changamoto ya ukosefu wa magari ya wagonjwa katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini lakini nataka niseme magari mengine yakiongezeka Kibaha Vijijini itaangaliwa zaidi kwani Rais amejenga vituo vya afya sio majengo bali ni kutaka huduma itolewe,"Amesema Mchengerwa.
Hata hivyo, Mchengerwa anatambua Kibaha Vijijini wanahitaji vituo vya afya vinne lakini amesema fedha za ujenzi wa vituo vya afya zinatoka Wizara ya Afya kwenda Tamisemi ambapo amemuagiza Mkurugenzi wa afya Dr .Erasto Sylvanus kuhakikisha fedha hizo zinakwenda kwa maelekezo ili kusudi Kibaha Vijijini hipate vituo viwili vya afya.





Post a Comment