RC PWANI AHIMIZA JAMII KUWAPELEKA WATOTO CHINI YA MIAKA 10 KUPATA CHANJO YA POLIO
Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameyaomba makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo Wazazi,walezi ,viongozi wa Serikali, viongozi wa dini, viongozi wa kijamii na wadau wengine kushirikiana kwa pamoja katika kuhamasisha Wananchi juu ya kampeni ya utoaji wa Chanjo ya Polio kwa watoto chini ya umri wa miaka 10.
Kunenge ametoa wito huo Agosti 24/2026 wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika mkutano maalum uliofanyika ofisini kwake kuhusu kampeni ya utoaji wa chanjo hiyo inayotarajia kuanza Agosti 27 hadi Agosti 30,2026.
Kunenge amesema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizofanikiwa kutokomeza ugonjwa wa Polio unaosababishwa na Kirusi Pori cha Polio aina ya kwanza (Wild Poliovirus Type 1).
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu kampeni ya chanjo inayotarajia kuanza Agosti 27 hadi Agosti 30,2026.Amesema kufuatia mafanikio hayo ,Shirika la Afya Duniani (WHO)lilitangaza Tanzania kuwa nchi isiyo na maambukizi ya Polio Mwezi Novemba 2025.
Kunenge amesema hatahivyo,kutokana na kubaini kwa uwepo wa Kirusi cha Polio katika mazingira, ikiwemo majitaka katika baadhi ya maeneo hapa nchini Serikali imeandaa kampeni maalum ya utoaji wa chanjo ya matone ya Polio aina mpya ya Novel Oral Polio Vaccine Type 2(nOPV2).
Amesema chanjo hiyo ni kwa ajili ya watoto wote waliopo chini ya umri wa miaka 10 ambapo dozi yake itatolewa mara mbili ambapo dozi ya kwanza itatolewa kuanzia Agosti 27 hadi Agosti 30,2026 na dozi ya pili itatolewa kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 02,2026.
Mikoa inayohusika na kampeni hiyo ni Mkoa wa Pwani,Dar es salaam,Tanga, Dodoma,Manyara , Kilimanjaro,Arusha na Mara ambapo lengo kubwa ni kuwakinga watoto dhidi ya Kirusi cha Polio aina ya pili ambacho kinaweza kusababisha ugonjwa wa kupooza na ulemavu wa kudumu.
Kunenge amesema kuwa katika kampeni hiyo Mkoa wa Pwani unalenga kuwafikia jumla ya watoto 587,509 walio chini ya umri wa miaka 10 katika Halmashauri zote ambapo Halmashauri ya Bagamoyo watoto 57,336, Chalinze 94,424,Kibaha Vijijini 32,849, Kibaha Manispaa 73,019,Kibiti 59,984,Kisarawe 43,491,Mafia 17,553, Mkuranga 161,103 na Rufiji ni 47,750.
Kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge na Waandishi wa habari kilichofanyika Agosti 24,2026 kwa ajili ya kuhamasisha Wananchi juu ya kampeni ya chanjo ya Polio kwa watoto chini ya umri wa miaka 10 itakayoanza Agosti 27,2026.Kunenge amewahakikishia Wananchi kuwa maandalizi juu ya kampeni hiyo yamekamilika na kwamba timu za afya zitafika katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha kila mtoto anafikiwa na kupata chanjo.
Amesema huduma ya chanjo hiyo zitatolewa nyumba kwa nyumba ,Shuleni,katika maeneo ya mikusanyiko,nyumba za Ibada,vituo vya mabasi ,masoko pamoja na maeneo magumu kufikika yakiwemo yale ya delta na visiwani.
Kunenge,ameongeza kuwa Mkoa wa Pwani unaendelea kufanya vizuri katika utoaji wa huduma za chanjo kwani mwaka 2025 Halmashauri zote zilifikisha kiwango cha utoaji wa chanjo zaidi ya asilimia 99 na hivyo kuvuka lengo la Kitaifa la asilimia 95.
"Nawahakikishia Wananchi kuwa chanjo zinazotolewa nchini zinazingatia viwango vya usalama na ubora na zimeidhinishwa na Mamlaka husika za afya na zinatolewa kwa kuzingatia miongozo ya Kitaifa na Kimataifa," amesema Kunenge .
Hata hivyo, Kunenge ameipongeza Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka kipaumbele katika afya na ustawi wa Watanzania ikiwemo kuhakikisha upatikanaji wa chanjo,dawa vifaa tiba na vitendanishi.



Post a Comment