HEADER AD

HEADER AD

MWENYEKITI UWT KIBAHA AWATAKA WANAWAKE KUWA WABUNIFU NA KUJIFUNZA MBINU ZA UJASIRIAMALI

  


Na Gustaphu Haule, Pwani

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Kibaha Mjini Elina Mgonja amewataka Wanawake wa Kata ya Visiga kuwa wabunifu pamoja na kupenda kujifunza mbinu mbalimbali za ujasiriamali ili ziweze kuwasaidia katika kujikwamua kiuchumi.

Mgonja, ametoa wito huo Agosti 12/2026 wakati akizungumza na Wanawake hao katika mkutano uliofanyika Visiga Kati ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuwafundisha Wanawake mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali.

Amesema kuwa,Mwenyezi Mungu alimuumba Adam  lakini akaona ni vyema amtafutie msaidizi ambaye ni Hawa na kwamba Wanawake wapo kwa makusudi ya kuwasaidia Wanaume zao.

      Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja akionyesha kitenge cha Batiki alichokitengeneza katika mafunzo ya ujasiriamali yaliyokuwa yakifanyika katika Kata ya Visiga Agosti 12/2026.

Amesema kuolewa ni wajibu na sio kazi kwahiyo lazima Mwanamke awe na kitu cha kujishughulisha ili kusudi apate kipato ambacho kitakuwa kinamsaidia mume wake katika kutekeleza masuala mbalimbali yanayohusu familia.

Amesema ili kupata kipato hicho ni vyema Mwanamke akawa na ujuzi wa kufanya jambo lolote na ikiwezekana wajifunze mbinu mbalimbali za kijasiriamali ambazo zitakuwa nguzo ya kupata kipato.

"Tunatakiwa tuwe wasaidizi wazuri kwa waume zetu sio kila kitu unaomba kwa mume kwani wakati mwingine huwa tunaomba hela ya chumvi na hata kiberiti jambo ambalo sio sahihi",amesema Mgonja .

Mgonja ameongeza kuwa ndoa nyingi zinavunjika kutokana na mgogoro wa kipato na mara nyingi mgogoro huo unaanzia kwa Mwanamke kwakuwa hana kazi ya kufanya na badala yake anaomba kila kitu kutoka kwa mume wake.

      Wanawake wa Kata ya Visiga wakishiriki mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika Agosti 12/2026 kwa ufadhili wa mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja.

Amesema Mwanaume anapaswa kuombwa vitu vikubwa vinavyohitaji fedha nyingi ikiwemo ada ya Shule lakini sio kumsumbua mume kwa fedha ya Kiberiti jambo ambalo ni aibu kwa Mwanamke.

Mgonja ameongeza kuwa kwa kutambua umuhimu wa Wanawake katika masuala ya uchumi ameamua kujitoa na kuanza kuwasaidia Wanawake juu ya kuwapa elimu na mafunzo ya namna ya kutengeneza Vitenge vya Batiki pamoja na Sabuni ujuzi ambao utawasaidia katika maisha yao.

Mgonja amesema kuwa anafanya hivyo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwakuwa amekuwa akiweka mipango mbalimbali ya kuwakomboa Wanawake hapa nchini.

Amewapongeza Wanawake wa UWT Kata ya Visiga pamoja na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Kata hiyo kwa ushirikiano na mshikamano walionao ambapo amewaomba waendelee kushirikiana katika kudumisha na kulinda amani .

Mwenyekiti wa UWT Kata ya Visiga Fatuma Omary amempongeza mwenyekiti huyo wa UWT kwa namna ambavyo amejipanga kuwasaidia Wanawake hasa katika masuala ya kuwakomboa kiuchumi.

       Mwenyekiti wa UWT Kata ya Visiga Fatuma Omary akizungumza katika mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika Agosti 12/2026 katika Kata hiyo.

Omary ,amemuomba mwenyekiti huyo kuendelea kutoa mafunzo hayo bila kuchoka huku akiahidi kuendelea kuyatumia mafunzo hayo pamoja na kuwafundisha Wanawake wenzao ili waweze kujikomboa na umaskini.

Naye Salma Hamad Mkazi wa Kata ya Tangini ambaye ni mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ameeleza kufurahishwa mafunzo hayo huku akisema awali hakuwa na ujuzi huo lakini kwasasa anaamini anakwenda kutumia ujuzi huo kuanzia miradi mbalimbali ikiwemo kutengeneza vitenge vya Batiki, Sabuni na mafuta ya shampoo.

           Diwani wa Kata ya Visiga Mohamed Mpaki( aliyesimama Kulia) akishuhudia mafunzo ya ujasiriamali ya utengenezaji wa vitenge vya Batiki na Sabuni yaliyofanyika Agosti 12/2026 chini ya Mwenyekiti wa UWT Elina Mgonja.

No comments