MWENYEKITI UWT KIBAHA AWAFUNDA WANAWAKE KATA YA VIZIWAVIZIWA KUTENGENEZA SABUNI, VITENGE, BATIKI,MAFUTA
Na Gustaphu Haule, Pwani
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Kibaha Mjini Elina Mgonja amewafikia Wanawake wa Kata ya Viziwaziwa ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa programu yake ya kutoa elimu na mafunzo kuhusu ujasiriamali.
Mgonja amefika katika Kata hiyo Agosti 11/2026 akiwa ameambatana na Katibu wa UWT Kibaha Mjini Secilia Ndallu pamoja na maafisa kutoka Benki ya Azania tawi la Kibaha.
Akiwa katika Kata hiyo Mgonja amewafundisha Wanawake wa Kata hiyo namna ya kutengeneza Sabuni za aina mbalimbali,Vitenge vya Batiki,Mafuta ya ngozi pamoja na mafuta ya kuoshea nywele( Shampoo).
Somo la utengenezaji wa Sabuni na shampoo kwa Wanawake wa Kata ya Viziwaziwa katika mafunzo yaliyofanyika Agosti 11/2026 katika viwanja vya CCM.
Akizungumza katika mafunzo hayo Mgonja amesema kuwa programu ya mafunzo hayo inalenga kuwapa ujuzi Wanawake wa Kibaha Mjini ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Amesema hadi sasa ametoa mafunzo hayo katika Kata nane ikiwemo Kata ya Msangani,Kata Mkuza,Kata ya Tumbi ,Kata ya Mailimoja,Kata ya Kibaha ,Kata ya Kongowe,Kata ya Misugusugu na leo amekamilisha mafunzo katika Kata ya Viziwaziwa.
Aidha amesema Agosti 12/2026 ziara ya mafunzo hayo itaendelea katika Kata ya Visiga huku akiwaomba Wanawake kuhakikisha wanajitokeza kutumia fursa hiyo ambayo itawasaidia kuinua kipato cha maisha yao.
Wanawake wa Kata ya Viziwaziwa wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumaliza mafunzo ya kutengeneza Sabuni na Vitenge vya Batiki.
Amesema yeye alitumia fedha nyingi kusomea masomo ya ujasiriamali lakini masomo hayo yamemsaidia kumtoa kimaisha na sasa ameamua ujuzi alionao awafundishe Wanawake wenzake bure.
Amesema programu ya kutoa mafunzo hayo kwa Wanawake wa Kibaha Mjini yametumia fedha nyingi kwakuwa vifaa vya kufundishia ni gharama kuwa ambapo amewaomba Wanawake kuona umuhimu wa kuzingatia mafunzo hayo.
"Madhumuni ya UWT ni kuwakomboa Wanawake kifikra, kiuchumi pamoja na kuwatoa katika hali ya umaskini na ndio maana mara zote huwa wanasisitiza suala la Siasa na uchumi lakini katika suala la uchumi yeye ameona awafundishe masomo ya ujasiriamali,",amesema Mgonja
Mgonja amesema kutokana na umuhimu wa UWT ni lazima kuanzia sasa na kuendelea Wanawake washikamane kuimarisha Umoja wao kwakuwa ndio nguzo ambayo inawaunganisha Wanawake wote wa Kibaha Mjini na Taifa kwa ujumla .
Mgonja amempongeza Mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Selina Koka kwa namna ambavyo anajitoa kuwasaidia Wanawake kupata fursa mbalimbali huku akisema kwasasa mama Koka ameamua kuwaletea fursa ya mikopo kutoka Benki ya Azania.
Katibu wa UWT Kibaha Mjini Secilia Ndallu,amesema anampongeza mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini kwa kujitoa kuwafundisha Wanawake hao mafunzo ya ujasiriamali.
Kitenge cha Batiki kilichotengenezwa Agosti 11/2026 na Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja katika Kata ya Viziwaziwa.
Ndallu,amesema wakati huu sio wakati wa kukaa magenge wala kupanga safu za uongozi bali ni wakati sahihi wa kufanyakazi za kujiletea maendeleo ambapo amewaomba Wanawake kuchangamkia fursa hiyo muhimu.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Mkazi wa Kata ya Viziwaziwa Salome Lusikya , amemshukuru mwenyekiti wa UWT kufundisha masuala ya ujasiriamali kwa Wanawake wa Kata hiyo.
Hata hivyo Lusikya amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwakuwa yatawasaidia kupata ujuzi wa kuzalisha bidhaa zao na kisha kuziuza katika masoko mbalimbali na hivyo kupata kipato cha kuendesha maisha ya familia zao.




Post a Comment