HEADER AD

HEADER AD

MWENYEKITI UWT WILAYA YA KIBAHA AWAFUNDA UJASIRIAMALI WANAWAKE KATA YA MAILIMOJA, TUMBI

Na Gustaphu Haule, Pwani

WANAWAKE wa Kata ya Mailimoja na Kata ya Tumbi waliopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wamenufaika na mafunzo ya ujasiriamali yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Kibaha Mjini Elina Mgonja.

Mafunzo hayo yametolewa Agosti 05/2026 katika viwanja vya Chama Cha Mapinduzi( CCM) Mkoa wa Pwani ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa mafunzo hayo yaliyoanza kutolewa na Mwenyekiti huyo Agosti 04 katika Kata ya Msangani na Mkuza.

Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja ( aliyekaa kwenye kiti) akiwafundisha Wanawake wa Kata ya Mailimoja na Tumbi kutengeneza Sabuni za aina mbalimbali katika mafunzo yaliyofanyika Agosti 05/2026 katika viwanja vya CCM Mkoa wa Pwani.

Mgonja yupo katika ziara  ya kuwatembelea Wanawake wa Kata 14 za Kibaha Mjini kwa ajili ya kuwashukuru juu ya kufanikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi wa mwaka 2025 akienda sambamba na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa Wanawake hao.

Wakizungumza mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo katika viwanja vya CCM Mkoa wa Pwani baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo akiwemo  Asha Mloli kutoka Kata ya Mailimoja amesema wanamshukuru mwenyekiti wao kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali bila kulipia chochote.

Mloli amesema kuwa hatua ya mwenyekiti wao kujitoa na kuwafundisha elimu ya ujasiriamali kwa vitendo ni sehemu ya kuwasaidia katika kuwakuza kibiashara na hivyo kuwakwamua akina mama kiuchumi.

        Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja (kushoto) akiwafundisha Wanawake wa Kata ya Mailimoja na Tumbi kutengeneza vitenge vya Batiki mafunzo ambayo yamefanyika Agosti 05,2026 katika viwanja vya CCM Mkoa wa Pwani.

Amesema mafunzo hayo kwao ni muhimu na kwamba yatawasaidia kuanzisha biashara zao kupitia utengenezaji wa vitenge vya Batiki,Sabuni za aina mbalimbali pamoja na mafuta ya ngozi (lotion).

"Kwakweli nina mshukuru mwenyekiti wetu wa UWT Wilaya Kibaha Mjini Elina Mgonja kwa kuona umuhimu wa kuwainua Wanawake kiuchumi kwa kutufundisha masomo ya ujasiriamali kwani leo tumepata ujuzi ambao wengi wetu hatukuwanao", amesema Mloli.

Amemuomba mwenyekiti huyo kuendelea kutoa elimu hiyo kwa Wanawake kwakuwa elimu hiyo ni muhimu na itakuwa mkombozi kwa akina mama wengi katika kufanya shughuli zao za kiuchumi.

Nae Fatuma Mngoma mstaafu kutoka  Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) amesema kuwa amefurahishwa kupata mafunzo hayo kwani mafunzo hayo ni mwanzo wa yeye kuwa mjasiriamali mkubwa .

       Mafunzo ya kutengeneza Sabuni na Vitenge vya Batiki yaliyofanyika Agosti 05/2026 chini ya mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja.

Mngoma amesema kuwa hakuwai kupata mafunzo hayo sehemu yoyote lakini kwasasa anamshukuru mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Kibaha Mjini Elina Mgonja kwa kutoa mafunzo hayo bure bila kuchangia jambo ambalo ni bahati kwake.

"Mimi ni mstaafu kutoka Tughe na katika maisha yangu  sikuwai kupata elimu kuhusu mafunzo ya ujasiriamali lakini leo nimepata mafunzo haya bure kutoka kwa Mwenyekiti wa UWT Elina Mgonja kwahiyo nachukua nafasi hii kumpongeza mwenyekiti wetu pamoja na kumuunga mkono kwa hiki anachokifanya ", amesema Mngoma .

Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja amesema kuwa yeye mtaalamu wa masuala ya ujasiriamali akiwa anatengeneza bidhaa mbalimbali kupitia malighafi za asili ikiwemo matunda ya Parachichi yanayotumika kutengeneza mafuta ya kupaka ya ngozi.

Mafunzo ya ujasiriamali yaliyotolewa Agosti 05,2026 na Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja (kushoto).

Mngoja amesema kwa kipindi kirefu amekuwa akifundisha watu mbalimbali kwa kulipwa fedha nyingi lakini ameona kwasasa asogeze ujuzi huo kwa Wanawake wenzake wa Kibaha Mjini ili na wao wapate kujishughulisha katika masuala ya kuongeza kipato katika familia .

Amesema miaka ya nyuma alitoa mafunzo kwa Wanawake wa Kibaha japo kwa watu wachache lakini ameona kuna haja ya kuendelee kufanya hivyo ili kuwakomboa kiuchumi Wanawake wenzake.

",Mimi nimeamua kujitolea kuwafundisha Wanawake wa UWT namna ya kutengeneza Sabuni,Vitenge vya Batiki,mafuta ya aina mbalimbali na mambo mengine ya kijasiriamali kwakuwa nataka kuona kila mwanamke anakuwa bize katika shughuli zake za kujitafutia kipato,"amesema Mgonja.

Mgonja amesema ameanza kutoa mafunzo hayo kwa Wanawake wa Kata ya Msangani na Mkuza, Tumbi na Mailimoja  lakini lengo lake ni kuhakikisha anapita katika Kata zote kuwapa fursa Wanawake kujikita katika Shughuli za kijasiriamali.

        Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja wa kwanza kulia akionyesha Kitenge cha Batiki mara baada ya kumaliza kukitengeneza katika mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika katika viwanja cha CCM Mkoa wa Pwani Agosti 05/2026.

Mgonja amewaomba Wanawake wa UWT Kibaha Mjini kuhakikisha wanajitokeza kushiriki katika fursa mbalimbali zinazotolewa hususani za kijasiriamali ili waweze kupata elimu  ambayo itawasaidia kuwakomboa kiuchumi.

Katibu wa UWT Kibaha Mjini Secilia Ndallu amewaomba Wanawake wa UWT kujitokeza kushiriki mafunzo hayo kwakuwa yanatolewa bure bila gharama yoyote lakini pia ni kwa ajili ya faida ya maisha yao.

Ndallu amesema kipindi hiki ni kipindi cha kufanyakazi na hakuna uchaguzi wowote na kwamba kama kuna mtu anawaza uchaguzi ni wazi kuwa anajipotezea muda ambapo amewaomba Wanawake kuungana na Mwenyekiti katika mafunzo hayo.

        Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini akionyesha Sabuni aliyoitengeneza katika mafunzo ya ujasiriamali yaliyofanyika Agosti 05/2026 viwanja vya CCM Mkoa wa Pwani.


No comments