HEADER AD

HEADER AD

MWENYEKITI UWT KIBAHA ATOA MAFUNZO BURE YA KUTENGENEZA BIDHAA MBALIMBALI KWA WANAWAKE


>> Elina Mgonja ni mtaalam na mkufunzi wa masuala ya ujasiriamali

Na Gustaphu Haule, Pwani 

MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi ( UWT) Wilaya ya Kibaha Mjini Elina Mgonja ameanza kuwapa tabasamu Wanawake wa UWT Kibaha Mjini kwa kuwafundisha bure  masuala ujasiriamali wa kutengeneza bidhaa mbalimbali.

Mgonja ambaye mbali na kuwa mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini lakini pia ni mtaalamu na mkufunzi wa masuala ya ujasiriamali anayetambulika Kitaifa na Kimataifa kwa kutengeneza bidhaa zake mwenyewe.




Mgonja ameanza kutoa elimu hiyo Agosti 4,2026 katika Kata ya Msangani na Kata ya Mkuza ambapo miongoni mwa mafunzo anayotoa ni pamoja na kutengeneza Vitenge vya Batiki,Sabuni na mafuta mbalimbali ya ngozi ( Lotion).

Elina anatoa mafunzo hayo bure ikiwa ni sehemu ya kuimarisha Umoja wa UWT ili kusudi Wanawake waliopo katika Umoja huo waweze kujikwamua kiuchumi na hivyo kupunguza utegemezi kwa wanaume zao.

Akizungumza wakati akitoa mafunzo hayo kwa Wanawake  wa Kata ya Msangani na Kata ya Mkuza Mgonja amesema anawapongeza Wanawake hao kwa kazi kubwa waliyoifanya katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ambao ulisaidia kumpata Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, Mbunge Silvestry Koka pamoja na madiwani.

Amesema wakati alipokuwa akichaguliwa kuwa mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini aliahidi kutoa bure elimu ya ujasiriamali kwa Wanawake wa Kibaha Mjini na alifanikiwa kufanya hivyo katika ukumbi wa CCM japo waliohudhuria walikuwa wachache wapatao watu 600.

     Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja wa kwanza kushoto akionyesha Kitenge cha Batiki mara baada ya kuwafundisha Wanawake wa Kata ya Msangani Agosti 04,2026.

Pia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 alipita kufanya kampeni na kuomba kura katika Kata mbalimbali na kuahidi endapo CCM ikishinda atapita tena kila Kata kwa ajili ya kutoa bure elimu ya ujasiriamali.

Amesema anashukuru uchaguzi umekwisha na CCM imeshinda kwa kishindo kuanzia ngazi ya Urais,Ubunge na udiwani lakini kwa Kibaha Mjini Wanawake ndio walioongoza kwa kupiga kura na kukichagua Chama Cha Mapinduzi ( CCM).

Mgonja amesema kutokana na hali hiyo ,alikaa na kamati yake ya utekelezaji na kujadili namna ya kuwashukuru Wanawake hao na hatimaye kupanga kufanya ziara ya kuwashukuru Wanawake hao kwa kuwapa elimu bure ya ujasiriamali.

     Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi ( UWT) Kibaha Mjini Elina Mgonja akitoa mafunzo ya ujasiriamali kwa Wanawake Agosti 04 2026.

Amesema anataka kuona Wanawake wa UWT Kibaha Mjini wanasimama imara ili waweze kujitegemea kiuchumi kwani wanapokuwa imara hawata subiri kupewa fedha kiasi cha Sh. 100,000 kutoka kwa wagombea ili waweze kuwachagua.

"Mimi sitaki kusikia Wanawake wanatumika tu wakati wa uchaguzi kwa kupewa Sh.100,000  ili wakapige kura lakini nataka wasimame imara kiuchumi ili waweze kufanya maamuzi ya bila kulazimishwa na mtu na ndio maana nawafundisha namna ya kujitegemea",amesema Mgonja 

Mgonja amesema kuwa atahakikisha  anatoa mafunzo hayo katika Kata zote na baada ya kutoa mafunzo hayo anaamini kila mwanamke atakuwa imara na amepata ujuzi ambao utawasaidia katika maisha yao.

       Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Kibaha Mjini Elina Mgonja ( Kulia) akiwafundisha Wanawake kutengeneza vitenge vya Batiki katika mafunzo yaliyofanyika Agosti 04,2026 katika Kata ya Msangani na Mkuza.

Amesema yeye yupo tayari kuendelea kuwasaidia Wanawake kwa namna yoyote anayoweza ambapo amewapa fursa akina mama hao kwa yeyote anayetaka ushauri wakijasiriamali wafike nyumbani kwake ili aweze kuwasaidia.

Amewashauri Wanawake hao baada ya kupata mafunzo hayo wajiunge kwenye vikundi na ikiwezekana wasajiliwe ili wapate fursa ya kwenda Halmashauri kwa ajili ya kupata mikopo itakayowaweza kupata mitaji ya kukuza bidhaa zao.

"Nataka mkitoka hapa muende mkawe walimu kwa wenzenu lakini nendeni mkatengeneze bidhaa bora na zenye mvuto ili ziweze kupata masoko ya ndani na nje ya nchi kwani naamini bidhaa zikiwa bora masoko yanapatikana," amesema Mgonja .

Katibu wa UWT Kibaha Mjini Secilia Ndallu,amesema wanataka Wanawake wa UWT Kibaha Mjini wajitegemee kwa kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi hali ambayo itawaondoa katika masimango.

         Katibu wa UWT Kibaha  Mjini Secilia Ndallu katika mafunzo ya ujasiriamali katika Kata ya Msangani na Kata ya Mkuza Agosti 04,2026.

Ndallu amemshukuru mwenyekiti wa UWT kwa namna ambavyo amejitoa  kuwafundisha Wanawake hao masuala ya ujasiriamali ambapo ametumia nafasi hiyo kuwaomba Wanawake kuhakikisha wanatumia fursa ya mafunzo hayo kwa ajili ya kujiendeleza kijasiriamali.

Amesema kuwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan hataki kuona Wanawake wanateseka kwahiyo kwa kufuata nyanyo za Rais UWT Kibaha Mjini  imeona sasa iende kwa vitendo zaidi .

Amesema sasa hivi hakuna uchaguzi bali wanafanyakazi kwa ajili ya kuimarisha Chama na Jumuiya zake na ndio maana mwenyekiti wa UWT anapita kuhakikisha ahadi zake zinatekelezwa na wanachama wake wanaimarika kiuchumi.

"Kiongozi mzuri ni yule anayeshauri, kuwapenda watu na kufanyakazi lakini mwenyekiti mama Mgonja anafanyakazi nzuri ndio maana leo amejitoa kuwaletea elimu na mafunzo ya ujasiriamali kwahiyo natamani kuona UWT inayojitegemea na sio ombaomba,"amesema Ndallu.

Mjumbe wa Kamati ya utekelezaji ya UWT Kibaha Mjini Dr.Zainabu Gama amesema  wanatoa mafunzo ya ujasiriamali ili Wanawake wainuke kiuchumi.

Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja akionyesha Sabuni aliyoitengeneza katika mafunzo yaliyofanyika Agosti 04,2026 katika Kata ya Msangani.

Dr.Gama amesema kama Wanawake hawana nguvu ya kiuchumi mwisho wa siku watakuwa wananunuliwa katika uchaguzi lakini anaamini wakipata elimu hiyo wataweza kutengeneza bidhaa na kuziuza na hivyo kukuza uchumi wao.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo ambaye pia mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msangani Mwajuma Abdallah, amemshukuru Mwenyekiti wa UWT kwa namna alivyojitoa kuwasaidia kwani wanakwenda kuyatumia mafunzo hayo katika kukiimarisha kiuchumi.

Hata hivyo,siku ya kwanza ya mafunzo hayo katika Kata ya Msangani na Kata ya Mkuza zaidi ya wanufaika 100 wamefikiwa lakini Agosti 5,2026 mafunzo hayo yataendelea katika Kata ya Tumbi na Kata ya Mailimoja.

      Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini Elina Mgonja ( aliyekaa kwenye kiti) na Mjumbe wake Dr.Zainabu Gama wakitoa elimu ya ujasiriamali kwa Wanawake wa UWT Kata ya Msangani Agosti 04 2026.

No comments