HEADER AD

HEADER AD

RAIS DKT. SAMIA SULUHU KUANDIKA HISTORIA UZINDUZI BWAWA LA KUFUA UMEME RUFIJI


Na Gustaphu Haule, Pwani 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan Agosti 22/2026 ataweka historia na kishindo kikubwa katika uzinduzi wa Bwawa la kufua Umeme la Mwalimu Nyerere lililopo Rufiji mkoani Pwani.

Rais Samia ataweka kishindo hicho  kwa kufanikiwa kukamilisha ujenzi wa Bwawa hilo jambo ambalo limekuwa na mvuto mkubwa kwa Watanzania hasa katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa umeme hapa nchini.

Rais Samia atazindua Bwawa hilo huku mataifa makubwa duniani yakipigwa na butwaa kwa namna ambavyo Tanzania imeweza kukamilisha Bwawa hilo chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Bwawa la kufuata Umeme la Mwalimu Nyerere (JNHPP) ni uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Tanzania kwa kutumia fedha zake za ndani  kiasi cha Sh.Trilioni 7.452 ambapo ujenzi wake ulianzishwa na Rais wa awamu ya tano Hayyat John Magufuli mwaka 2019.

Imeelezwa kwamba Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kukamilisha bwawa hilo kwani wakati anaingia madarakani alikuta ujenzi wa Bwawa hilo umefikia asilimia 35 lakini alihakikisha anatoa fedha ili kusudi kukamilisha malengo ya Serikali ya ujenzi wa Bwawa hilo.

Kukamilika kwa Bwawa hilo ni mafanikio makubwa kwa Taifa kwani linakwenda kuzalisha Megawati za umeme 2115 na kuweza kuchangia takribani asilimia 45  kwenye gridi ya Taifa hivyo kuwafanya Watanzania kuwa na umeme wa kutosha.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza katika mkutano wake na Waandishi wa habari uliofanyika Agosti 20/2026 Mjini Kibaha amepongeza juhudi kubwa zilizofanywa na Rais Samia kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa Bwawa hilo.

           Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake Agosti 20/2026  kuhusu uzinduzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere linalotarajia kuzinduliwa Agosti 22/2026 na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Amesema umeme unaotoka katika Bwawa hilo tayari umeanza kuwa na faida kwa upande wa Mkoa wa Pwani kwani mwaka 2022 Mkoa wa Pwani ulikuwa ukipata umeme Megawati 118 lakini mwaka huu Mkoa unapata umeme Megawati 356 .

Amesema licha ya kuongezeka kwa Megawati hizo lakini pia Mkoa wa Pwani umepata bahati kwani kituo cha kupoza umeme kimejengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze na maeneo mengine mbalimbali ya Mkoa huo.

Amesema ujenzi wa vituo hivyo ndani ya Mkoa wa Pwani vinakwenda kumaliza changamoto na kilio cha umeme kwa wawekezaji wa viwanda ambao mara kwa mara walikuwa wakilia juu ya ukosefu wa umeme.

Amesema Mkoa wa Pwani ni Mkoa wa viwanda na Serikali ya awamu ya Sita imekuwa ikiwekeza nguvu katika kuimarisha viwanda na miongoni mwa maeneo ambayo yamekuwa na mafanikio makubwa ni katika suala la umeme.

Ameongeza kuwa viwanda ambavyo vimejengwa katika utawala wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan tangu aingie madarakani ni 495 na viwanda vipya vikubwa ni 395 kwahiyo suala la umeme limekuwa na mafanikio makubwa .

Amesema Serikali imefanyakazi ya kusambaza umeme katika Vitongoji 1,220 na Vijiji vyote isipokuwa Vijiji 8 ambavyo vinapatikana visiwani lakini kukamilika kwa Bwawa hilo ndio suluhisho la kuvifikia Vijiji hivyo.

Bwawa la kufua umeme asilimia 60 lipo Mkoa wa Pwani na asilimia 40  lipo Mkoa wa Morogoro na kwamba amewahakikishia Wananchi wa Morogoro kuwa wapo tayari kulitunza Bwawa hilo kwa faida ya Watanzania wote.

        Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na Waandishi habari Agosti 20/2026.

"Nampongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukamilisha mradi huo mkubwa kwani wakati anaingia alikuta mradi umefikia asilimia 35 lakini alihakikisha mradi unakamilika na sasa anakwenda kuuzindua,",amesema Kunenge .

Hata hivyo, Kunenge amesema uzinduzi wa Bwawa hilo  unakwenda kutimiza ndoto ya Watanzania na Taifa kwa ujumla lakini ni historia kubwa ambayo haijawai kutokea hapa nchini kwakuwa watu mbalimbali watahudhuria kutoka ndani na nje ya nchi.


No comments