KIWANDA CHA KUTENGENEZA KARATASI KILICHOPO SAENI CHATOA MSAADA SHULE YA MSINGI ZOGOWALE
>> Shule hiyo imepokea misaada mbalimbali yenye thamani ya Tsh. Milioni 8
>> Meneja biashara kiwanda cha Fortune Paper Colin Yang aishukuru serikali
Na Gustaphu Haule, Pwani
KIWANDA cha kutengeneza karatasi cha Fortune Paper kilichopo Mtaa wa Saeni Kata ya Misugusugu katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kimetoa misaada mbalimbali katika shule ya msingi Zogowale yenye thamani zaidi ya Tsh. Milioni 8.
Msaada huo ni pamoja na unga wa sembe kwa ajili ya chakula cha wanafunzi wa shule hiyo uliogharimu kiasi cha Sh.milioni 2,pampu ya kuvutia maji katika kisima kilichopo shuleni hapo iliyogharimu kiasi cha Tsh.milioni 1:1 pamoja na steshenari zenye gharama ya Tsh. Milioni 5.
Meneja wa kiwanda cha Fortune Paper kilichopo Mtaa wa Saeni Kata ya Misugusugu Manispaa ya Kibaha Weiwei Zhou ( Kulia)akikabidhi vifaa vya steshenari kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John (katikati)kwa ajili ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Zogowale na kushoto ni diwani wa Kata ya Misugusugu Ally Simba.
Mbali na msaada huo kiwanda hicho kimewasaidia wananchi wa Mtaa wa Saeni kupata maji kwa kuwaunganishia mabomba ya maji kutoka kiwandani humo na kuyapeleka katika maeneo ya Wananchi ikiwa ni umbali wa Kilomita 3.
Maji hayo watakuwa wanayatumia bure bila malipo na yatatumika kwa kuoga,kuoshea vyombo na matumizi mbalimbali ya kilimo ambapo zaidi ya Kaya 20 zitakuwa zinanufaika na uwepo wa maji hayo.
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika shuleni hapo Agosti 19/2026 baina ya meneja wa kiwanda hicho Weiwei Zhou pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon huku ikishuhudiwa na walimu, wanafunzi, viongozi wa Kata na Wananchi.
Meneja wa kiwanda cha kutengeneza karatasi cha Fortune Paper kilichopo Mtaa wa Saeni Kata ya Misugusugu Manispaa ya Kibaha Colin Yang ( Kulia) akizindua mradi wa maji waliojenga kwa Wananchi wa Mtaa huo kwa kumtwisha Ndoo kichwani Mkazi wa Mtaa huo Pili Nassoro ( kushoto).
Awali akizungumza kabla ya makabidhiano hayo Meneja biashara wa kiwanda cha Fortune Paper Colin Yang,amesema anaishukuru Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikitoa ushirikiano katika uwekezaji wa kiwanda hicho.
Yang amesema kuwa mbali na kuishukuru Serikali lakini pia ameishukuru jamii inayozunguka kiwanda hicho kwakuwa wamekuwa na mchango mkubwa wa kuhakikisha kiwanda kinaimarika na kuzalisha bidhaa zake.
Amesema Fortune Paper ni kiwanda cha kwanza katika eneo hilo katika kuwafikia jamii kwani licha ya kutoa ajira kwa vijana wa eneo hilo lakini pia kinagusa jamii na kwamba lengo lao ni kuhakikisha Wananchi wananufaika na uwekezaji huo.
"Kiwanda chetu kimekuwa cha kwanza kuchangia jamii inayoishi eneo hili na tunaomba viwanda vingine vijitokeze kuiga mfano wetu ili kusudi jamii inufaike na uwekezaji unaofanyika katika maeneo yao,"amesema Yang
Ameongeza kuwa kiwanda cha Fortune Paper kinaamini mafanikio yake yanatokana na kufanya mambo ya kimaendeleo kwa jamii na ndio maana licha ya kuchangia katika ukuaji wa uchumi,ajira na maendeleo ya Jamii lakini pia wanawajibika moja kwa moja kwa jamii inayowazunguka.
Wananchi wa Mtaa wa Zogowale pamoja na wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza karatasi cha Fortune Paper wakishuhudia hafla ya kukabidhi vyakula na vifaa mbalimbali vya steshenari kwa Shule ya Msingi Zogowale Agosti 19/2026.
Diwani wa Kata ya Misugusugu Ally Simba amekishukuru kiwanda hicho kwa kuchangia vitu muhimu katika Shule hiyo kwani vinakwenda kuwasaidia wanafunzi katika kuhakikisha wanakuwa imara na kuweza kuzingatia masomo yao.
Simba ,amesema kuwa kilichofanywa na kiwanda hicho ni jambo la kipekee kwani ameonyesha namna anavyotambua umuhimu wa Jamii wanayoishinayo huku akisema Serikali ipo pamoja kufanyakazi nao kwani wanategemea kupata mengi kutoka kwao.
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo amewashukuru wawekezaji wa kiwanda hicho kwa kutoa msaada wa chakula Shuleni hapo.
Hafla ya kukabidhi vifaa vya steshenari katika Shule ya Msingi Zogowale iliyofanywa na kiwanda cha karatasi cha Fortune Paper kilichopo Kata ya Misugusugu Manispaa ya Kibaha.
Amesema kilichofanywa na kiwanda hicho ni kusapoti mpango wa Serikali katika suala la lishe mashuleni na kwamba msaada huo utakuwa endelevu ili kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kupata chakula jambo ambalo litasaidia kusoma katika mazingira mazuri.
Amewataka viongozi wa ngazi ya Mtaa,Kata na Tarafa kuhakikisha wanawatumia wawekezaji waliopo katika maeneo yao ili kusukuma gurudumu la maendeleo.
Nae Mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Zogowale Irene Didas akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa Shule hiyo ameushukuru uongozi wa kiwanda hicho kwa kuwapa msaada huo.
Didas amesema pamoja na msaada huo lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya uhaba wa mashine ya fotokopi ambapo amewaomba wawekezaji hao kuona namna ya kuwasaidia mashine hiyo ili waweze kufanya mitihani yao kwa urahisi.
Hata hivyo ,Mkazi wa Mtaa wa Saeni Pili Nassoro amekishukuru kiwanda hicho kwa kuwapelekea mradi wa maji katika maeneo yao kwani awali walikuwa wanasafiri umbali mrefu kufuata maji .
Meneja wa Kiwanda cha Fortune Paper kilichopo Mtaa wa Saeni Kata ya Misugusugu Manispaa ya Kibaha Weiwei Zhou ( kulia) alikabidhi unga wa sembe kwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John ( Mwenye koti) na wa kwanza aliyeshika mfuko huo ni diwani wa Kata ya Misugusugu Ally Simba.






Post a Comment