HEADER AD

HEADER AD

WATOTO ZAIDI YA LAKI TANO KUPATA CHANJO YA POLIO

Na Gustaphu Haule, Pwani

WATOTO 587,509 wenye umri chini ya miaka 10 wanatarajia kufikiwa na huduma ya chanjo  ya matone kwa ajili ya kudhibiti ugonjwa wa Polio katika kampeni maalum itakayoanza Agosti 27 hadi Agosti 30 na kisha kurudiwa septemba 29 hadi Oktoba 02,2026.

Mratibu wa huduma za Chanjo Mkoa wa Pwani Dr.Alfred Ngowi ametoa kauli hiyo  Agosti 22/2026  Mjini Kibaha  alipokutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa taarifa kuhusu kampeni ya utoaji wa chanjo hiyo.

        Mratibu wa huduma ya  Chanjo Mkoa wa Pwani Dr.Alfred Ngowi akielezea kuhusu kampeni ya utoaji chanjo ya ugonjwa Polio kwa watoto chini ya umri wa miaka 10 inayotarajia kuanza Agosti 27 hadi Agosti 30 mwaka huu .

Amesema kuwa chanjo ya Polio ya matone(nopv2) inatumika kuzuia maambukizi ya Virusi vya Polio na Tanzania ilianza kutumika mwaka 2023 na Mwaka 2026.

Ngowi amesema chanjo hiyo ni kampeni maalum ambayo haihusiani na ratiba za chanjo za kawaida na kwamba chanjo hiyo itakuwa inatolewa katika vituo na maeneo mbalimbali.

Ngowi amesema kampeni hiyo itawafikia watoto wote waliolengwa katika maeneo yote ikiwemo nyumba kwa nyumba na kwamba hata katika maeneo ya delta tayari zimepangwa timu  za utoaji wa chanjo hiyo.

Pia amesema huduma hiyo itakuwa inatolewa katika Vituo vya afya,Kanisani ,Misikitini , maeneo ya watoto wa Mtaani , hususani katika viwanja vya mpira ,sokoni ,mashuleni ,maeneo ya vituo vya usafiri pamoja na maeneo ya uvuvi.

Amesema katika vituo hivyo kila timu itakuwa na watu watatu akiwemo Mchanjaji ,mhamasishaji na Mtunza takwimu ambapo amewaomba Wazazi na Wananchi kujitokeza kwa ajili ya kuhakikisha watoto wao wanapata huduma hiyo.

Kwa upande wake Afisa wa Wizara ya Afya kitengo cha Mpango wa Kinga na Chanjo Flora Kazoba amesema chanjo hiyo kwa awamu ya kwanza ilianza kutolewa Mikoa ya Kanda ya Ziwa Machi mwaka huu.


     Afisa wa Wizara ya Afya Kitengo cha Mpango wa Kinga na Chanjo Flora Kazoba (pichani) akiwa katika mkutano na Waandishi wa habari Agosti 22/2026 Mjini Kibaha.

Kazoba ,amesema kuwa walianza Kanda ya Ziwa baada ya kuthibitika kuwepo kwa  vimelea vya ugonjwa wa Polio katika Mkoa wa Mwanza na kwamba  kirusi cha Polio kinazalishwa kwenye majitaka na Mkoa wa Mwanza ni moja ya Mikoa yenye mabwawa ya majitaka.

Amesema kuwa Virusi vya ugonjwa wa Polio vipo vya aina tatu lakini aina ya pili iliachwa kutolewa lakini baada ya kugundua kirusi namba mbili kipo kwenye mazingira ya majitaka Serikali imeamua kuchukua hatua ya kudhibiti.

Amesema matone ya ugonjwa wa Polio namba mbili yanatolewa mara mbili ambapo kwa awamu ya kwanza mtoto atapewa matone mawili na awamu ya pili atapewa tena matone mawili na hiyo ni baada ya  wiki nne hadi sita na kwamba wanafanya hivyo ili kuimarisha Kinga kwa mtoto.

"Chanjo hii inatolewa mara mbili kwa mtoto mmoja kwani  awamu ya kwanza itaanza Agosti 27 hadi Agosti 30 lakini awamu ya pili itaanza Septamba 29 hadi Oktoba 02,2026 na watoto waliopata chanjo awamu ya kwanza ndio walewale ambao wanatakiwa kupata chanjo ya awamu ya pili kwakuwa lengo lake ni kuimarisha Kinga kwa mtoto,"amesema Kazoba.

Aidha,Kazoba amesema kuwa kauli mbiu ya kampeni hiyo ni "Mpe Chanjo Mtoto wako ,Linda Tabasamu Zuia Polio" huku akiwaomba Wazazi,walezi na Wananchi kwa ujumla kuhakikisha wanawapeleka watoto kupata chanjo kwakuwa ugonjwa wa Polio hauna tiba.

Amesema kwasasa kampeni ya chanjo ya Polio inakwenda kutolewa katika Mikoa nane ukiwemo Mkoa wa Pwani, Dar es Salam, Manyara, Arusha, Mara, Tanga, Dodoma na Kilimanjaro lakini itabaki Mikoa Sita ambayo itapangiwa ratiba yake.

Hata hivyo, Kazoba amesema kuwa Tanzania kwa mara ya kwanza ilipata mgonjwa wa polio mwaka 1996, na wizara ya afya imekuwa ikitekeleza kampeni ya ugonjwa huo ili kuzuia athari kutokana na kwamba mgonjwa akishapata ugonjwa huo hawezi kupata tiba yake.


No comments