Home
/
MAKUNDI MAALUM
/
FAMILIA YA JOSEPHATI MWITA WATOA MSAADA WA VIFAA WEZESHI KWA WATU WENYE ULEMAVU WA VIUNGO
FAMILIA YA JOSEPHATI MWITA WATOA MSAADA WA VIFAA WEZESHI KWA WATU WENYE ULEMAVU WA VIUNGO
DIMA ONLINE, Tarime
Josephati Mwita na mkewe Ester Josephati wakazi wa Nyamongo, wilayani Tarime mkoa wa Mara , wamekabidhi vifaa mbalimbali wezeshi yakiwemo Magongo, Kiti mwendo, Baiskeri za magurudumu matatu, mikongojo, nguo aina ya kanga vyenye jumla ya shilingi Milioni 2.2 .
Wamekabidhi vifaa hivyo Septemba, 11, 2026 mbele ya Wachungaji waKanisa la Waadventista Wasabato,Jimbo la Mara Kaskazini kwenye makambi ya watu wenye ulemavu yaliyofanyika katika viwanja vya chuo cha Mwera Vision, mjini Tarime , kambi linalohitimishwa leo Jumamosi lililodumu kwa siku saba.
Josephati amesema kuwa familia imeguswa kutoa msaada huo kwani watu wenye uhitaji maalum wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hivyo ni vyema wakapata msaada wezeshi.
" Bhoke Orindo mwenye ulemavu wa macho alituomba kuja kuwashika mkono watu wenye ulemavu . Zawadi hizi zitasaidia katika kupata huduma ya Kikristo" amesema Josephati .
Ester mke wa Josephati amesema familia inawapenda wenye ulemavu hivyo wasijione wanyonge huku akiwaombea baraka watu wenye ulemavu wa viungo na kuwaomba kutokata tamaa na wamtumikie mwenyezi Mungu.
Josephati Mwita na mkewe Ester wakizungumza baada ya kukabidhi msaada wa vifaa wezeshi kwa watu wenye ulemavu wa viungo.
Katibu wa Chama cha Wachungaji ambaye pia ni Mkurugenzi wa familia , Mkurugenzi wa uamsho na matengenezo kanisa la Waadventista Wasabato, Jimbo la Mara Kaskazini , Mch. Adili Ndimangwa ameishukuru familia ya Josephati Mwita na kusema kwamba imeleta uamsho kwa watu wenye uhitaji maalum .
Ametoa wito kwa watu wengine kuwasaidia watu mwenye ulemavu wa viungo kwani ni kundi linalokabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za kijamii na kiuchumi.
Akikabidhi kiti mwendo cha Prisca Mahende kwa mama yake mzazi Maria Stephano, kilichotolewa na familia ya Josephati Mwita, Mchungaji wa mtaa wa Sabasaba Mch. Boniface Nassari , amesema kanisa la Waadventista Wasabato wanawatambua watu wenye uhitaji maalum na kwamba litaendelea kushirikiana na watu wenye ulemavu wa viungo .
Mchungaji wa mtaa wa Sabasaba Mch. Boniface Nassari akisalimiana na Maria Stephano, mama mzazi wa Prisca Mahende mwenye ulemavu wa viungo baada ya kufika nyumbani kwako mtaa wa Kogete , Kata ya Kenyamanyori, mjini Tarime, kukabidhi Kiti Mwendo kilichotolewa na familia ya Josephati Mwita.
Mratibu wa makambi hayo ya watu wenye ulemavu wa viungo , Bhoke Orindo ameishukuru familia hiyo kwa msaada wa vifaa wezeshi huku akiwaombea na watu wengine kujitokeza kuwezesha watu wenye uhitaji maalum .
Wakati huo huo , Mkuu wa wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele amefika na kuzungumza na watu wenye ulemavu wa viungo katika kambi hilo na kutoa katoni 10 za maji .













Post a Comment