HEADER AD

HEADER AD

WANANCHI PWANI WAIPONGEZA TARURA KWA UTEKELEZAJI BARABARA YA KIROMO- CHAMBEZI


Na Gustaphu Haule, Pwani 

WANANCHI wa Kata ya Kiromo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani wamepongeza juhudi za Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) kwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Kiromo -Chambezi hadi Buma kwa kiwango cha lami.

Wakizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali waliotembelea mradi huo Septemba 11,2026 baadhi ya Wananchi hao walisema kuwa ujenzi wa barabara hiyo ni mkombozi mkubwa kwa Wananchi wanaopitiwa na barabara hiyo.

       Meneja TARURA Wilaya ya Bagamoyo Bupe Angetile( Kulia) akiwa na Mhandisi wa J.P Traders Ltd Paulo Nang'omwiu pamoja na Mhandisi Mbaraka Seseme kutoka  Tarura Bagamoyo wakikagua ujenzi wa daraja katika Barabara ya Kiromo - Chambezi hadi Buma.

Mohamed Fundi Mkazi wa Kitonga "A"amesema kuwa  barabara hiyo wakati wa mvua magari wala bodaboda yalikuwa hayapiti na kwamba kutokana na hali hiyo uzalishaji uliokuwa unategemea barabara hiyo ulikuwa unakwama.

Fundi amesema kuwa anaishukuru Serikali kupitia TARURA kwani kutokana na matengenezo hayo anaamini changamoto waliyokuwa wanaipata itakwisha na Wananchi wa Kiromo pamoja na wale wanaopitiwa na barabara watakuwa wanafanya uzalishaji pasipokuwa na shida ya barabara.

"Mimi naishukuru sana TARURA kwa maamuzi yao mazuri ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara hii kwani itasaidia Wananchi wa Bagamoyo hususani wakazi wa Kata ya Kiromo maeneo ya Kitonga "A "na Kitonga "B" pamoja na Makondeko kusaidia katika kusafirisha bidhaa zao," amesema Fundi.

Fundi ameiomba TARURA kuangalia kama kuna uwezekano barabara hiyo ifike hadi katika Shule ya Sekondari na hata katika maeneo ya Buma sambamba na kuunganisha barabara ya Makofia -Mlandizi ambapo hatahivyo ameahidi kushirikiana na wakazi wenzake kuitunza miundombinu ya barabara hiyo.

        Mwananchi wa Kiromo ambaye ni dereva Bodaboda  Mohammed Fundi.

Nae Salehe Rashid amesema kuwa barabara hiyo ilikuwa na madimbwi makubwa na mashimo makubwa na wakati ukipita na gari aina ya Kenta lazima lizame jambo ambalo lilikuwa linakwamisha mzunguko wa kibiashara na hivyo kupelekea uchumi kwa Wananchi kushuka.

Rashid amesema kwasasa shughuli za kijasiriamali zitakuwa zinakwenda vizuri kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo ambapo ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kupitia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara hiyo kwa kiwango lami .

Meriana Mjeri Mkazi wa Kiromo amesema kuwa anaishukuru Tarura pamoja na Serikali kwa ujumla kwa namna ambavyo wamejitoa na kuwekeza nguvu ya kuhakikisha wanajenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami .

Mjeri,amesema wakati wa mvua maji yalikuwa yanajaa kiasi ambacho kilikuwa kinapelekea mama wajawazito kushindwa kufika hospitali na hata  wanafunzi kushindwa kuvuka na kwenda shule lakini kwasasa anafurahia kuona changamoto hiyo inakwenda kumalizika.

Meneja Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA )Wilaya ya Bagamoyo Bupe Angetile amesema mradi wa barabara hiyo unajulikana kwa jina la Kiromo - Chambezi - Buma yenye Kilomita 11.

       Meneja Tarura Wilaya ya Bagamoyo Bupe Angetile akiwaonyesha Waandishi wa habari namna ambavyo mradi wa ujenzi wa barabara ya Kiromo - Chambezi - Buma kwa kiwango cha lami unaovyotekelezwa.

Angetile amesema ujenzi wa mradi huo unatekelezwa kwa kiwango cha lami Kilomita 2 na kuimarisha maeneo korofi kwa kuchonga sambamba na kuweka changarawe katika maeneo yote korofi.

Amesema kuwa mradi huo unatekelezwa kupitia mkandarasi mzawa JP Traders Limited kwa gharama ya Sh.bilioni 3.22  na ujenzi wake utachukua miezi 12 ikiwa ni kuanzia Julai 28 ,2026 hadi Julai 27 ,2027 ambapo kiwango cha lami itakayowekwa itakuwa lami ngumu.

Angetile ameongeza kuwa awali barabara hiyo ilikuwa na changamoto kubwa kwani wakati wa mvua Wananchi walikuwa wanashindwa kupita hususani wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kiromo na Shule ya Msingi .

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha Wananchi wa Kata ya Kiromo na maeneo mengine ya jirani kwani utasaidia kuongeza uchumi na kuwafanya waendelee vizuri katika Shughuli zao za uzalishaji.

        Ujenzi wa barabara wa Kiromo- Chambezi - Buma Wilaya ya Bagamoyo ukiwa unaendelea.

Angetile ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita kupitia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ambapo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 30.

Angetile ametoa wito kwa mkandarasi wa ujenzi wa barabara hiyo kuhakikisha anaongeza spidi ya utekelezaji wa mradi huo hasa katika kuelekea kipindi cha mvua na kwamba maeneo ambayo yataathirika ajitahidi kuweka tabaka ngumu ambalo haliathiri barabara hiyo.

     Ujenzi wa daraja katika barabara ya Kiromo -Chambezi - Buma ukiwa unaendelea, barabara hiyo inawekewa lami ngumu Kilomita mbili chini ya TARURA.

Msimamizi wa ujenzi wa barabara hiyo kutoka katika kampuni ya J.P Traders Ltd Mhandisi Paulo Nang'omwiu amesema kuwa kwa namna ambayo wameanza kasi yao ni nzuri kwani walipofikia anaimani kabla ya mvua kubwa zilizotabiriwa kunyesha ( El-Nino) watakuwa wamefikia katika tabaka ambalo halitaweza kuathiriwa na mvua hizo.

Nang'omwiu amesema kuwa sehemu nyingi ambazo zimekuwa na changamoto katika kipindi cha mvua tayari wamedhibiti kwa kutengeneza karavati kwa ajili ya kupitisha maji ambapo amewatoa wasiwasi Wananchi kuwa barabara yao itapitika vizuri kipindi chote cha mvua.

Hata hivyo, Nang'omwiu amesema kuwa anaimani kabla mwaka wa kimkataba haujaisha watakuwa wamemaliza kazi kwakuwa malengo yao ifikapo Machi hadi Aprili 2027 wawe wamekabidhi mradi huo kwa TARURA ikiwa tofauti ya miezi mitatu mbele.

       Meneja Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Bagamoyo Bupe Angetile (Kulia) akiwa na Mhandisi wa ujenzi wa barabara ya Kiromo - Chambezi - Buma walipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara Septemba 11,2026.


No comments