MCH. BONIFACE NASARI: USITUMIE ULEMAVU WAKO KUITESA JAMII
>> Asema dhambi ni dhambi haijalishi una hali gani
>> Awasisitiza waumini kutojiona wa maana
Na Mwandishi Wetu, Tarime
MCHUNGAJI wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Mtaa wa Sabasaba, Jimbo la Mara Kaskazini, Mch. Boniface Nasari, amewaasa watu wenye ulemavu wa viungo kutotumia hali zao kuwatesa au kuwakandamiza watu wengine katika jamii.
Amesema baadhi ya watu wenye ulemavu wamekuwa wakitumia hali zao kuwanyanyasa wengine, wakiwemo wenzao wenye ulemavu wa viungo akisisitiza kuwa hali hiyo haimpendezi Mungu.
Mch. Nasari ameyasema hayo Jumamosi, Septemba 12, 2026, akiwa mhudumu mkuu katika ibada ya kuhitimisha makambi ya watu wenye ulemavu wa viungo ya Jimbo la Mara Kaskazini, yaliyofanyika kwa siku saba katika Chuo cha Mwera Vision, mjini Tarime.
Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), Mtaa wa Sabasaba, Jimbo la Mara Kaskazini, Mch. Boniface Nasari akihubiri wakati wa Sabato ya kuhitimisha makambi ya Watu wenye ulemavu wa viungo.
Amesema dhambi haiangalii mtu ana macho au hana macho, bali dhambi hubaki kuwa dhambi bila kujali hali ya mtu, hivyo amewataka watu kuishi kwa kupendana, kusaidiana na kutumia fursa wanazopata kwa njia sahihi.
“Watu wenye ulemavu msitumie ulemavu wenu kuitesa jamii, msitumie ulemavu wenu kukandamiza baadhi ya watu kwenye jamii. Tumia ulemavu wako kupata fursa na haki unayopaswa kupata, maana kuna walemavu wengine ni wa manung’uniko kila pakicha.
“Wapo walemavu wameajiriwa ni wahasibu lakini wamekuwa wezi, wananyanyasa hata walemavu wenzao. Pesa inatoka awapatie wenzake yeye anachukua kiasi kikubwa na kuwadhulumu wenzake.
“Usije ukasema kwamba kwa hali niliyonayo Yesu atanionea huruma. Dhambi ni dhambi tu, haijalishi una kiungo kimoja au hauna, kwa sababu Mungu hajatunyima vyote,” amesema Nasari .
Pia amesema wapo baadhi ya wasio walemavu kuwatumia walemavu kwa faida zao wenyewe jambo ambalo si sahihi .
Akomalia suala la uzinzi
Mch. Nasari pia amekemea vitendo vya uzinzi miongoni mwa watu wenye ulemavu, akisema kila mtu atasimama mbele ya hukumu na kutoa hesabu ya matendo yake bila kujali hali yake ya kiafya au ulemavu alionao.
“Kuna wengine ni walemavu lakini nao ni wahuni kweli, wanatongozana hapa hapa kwenye kambi. Najua mnasema, ‘Pasta unahubiri nini?’ Nataka niwaambie, dhambi ni dhambi.
“Niwatie moyo mnapoenda kwenye jamii mnayoishi mkafanyike baraka kwa jina la Yesu. Kama ulikuwa na tabia ya kutafuna tafuna vitoto vya watu ukisingizia ulemavu, utashindwa kwa jina la Yesu.
“Kuna mlemavu anaenda anamtafuta mke wa mtu, anamuuliza, ‘Hivi ndiyo wewe?’ Anaanza kumshikashika kifuani na kusema, ‘Hivi ni weweeee.’ Zingatieni mliyojifunza hapa, hakuna mlemavu ambaye hajasikia,” amesema Nasari.
‘Usijione ni wa maana’
Mch. Nasari amewataka waumini kutokujiona kuwa ni bora au wa maana kuliko wengine, akisema kila mwanadamu anaweza kukumbwa na ulemavu wakati wowote wa maisha.
Waumini wakiwemo watu wenye ulemavu wa viungo wakiwa kwenye ibada siku ya jumamosi, Septemba, 12, 2026.
Amesema hali hiyo inapaswa kuwa sababu ya watu kumtukuza Mungu kwa jinsi walivyoumbwa na kuthamini utu wa kila mmoja.
“Sisi ni walemavu watarajiwa. Unaweza kushangaa unamuona mtu analingalinga, anajiona ni wa maana sana kuliko wengine. Ungekaa na hawa watu wenye ulemavu usingejiona wa maana.
“Wakati unadhani wewe ni wa maana, kumbuka hapa kuna watu ambao wameumbwa kwa mfano wa Mungu. Kwanini nasema sisi ni walemavu watarajiwa?
“Kuna watu walikuwa na viungo vyote lakini leo ni walemavu, hawana mikono. Akitaka kwenda chooni mpaka apate usaidizi, akitaka kukaa mpaka apate msaada. Wengine hapa walizaliwa vizuri, wakakua vizuri, wakafika mahala macho yakafa, wanasoma kwa shida,” amesema Mch. Nasari .
Mungu amewabariki wenye ulemavu
Mchungaji huyo amesema watu wenye ulemavu wamebarikiwa kwa kuwa wana vipaji na uwezo mbalimbali, hivyo amewataka kutumia vipaji hivyo kumtumikia Mungu na kujikwamua kiuchumi.
“Kuna wengine hapa hawaongei ila wanajua kushona. Kuna mtafsiri wa lugha ya alama hapa ni bubu, ni fundi ujenzi, anajenga vizuri mno kuliko hata watu wanaoona.”
‘Chuma kimechomoka’
Katika ibada hiyo, Mch. Boniface alitoa somo lililopewa jina “Chuma Kimechomoka”, akilitumia kufundisha kuhusu vipaji, karama na uwezo ambao Mungu amempa kila mwanadamu.
Somo hilo lilijikita katika vifungu mbalimbali vya Biblia, vikiwemo 2 Wafalme 6:1-7, Yeremia 51: 20 , 2 Wafalme 7:3-5, 2 Wafalme 5:1-3, Yohana 15:5
Amesema “chuma chenye mpini” kinawakilisha talanta, vipaji na uwezo ambao Mungu amempa mtu, akisisitiza kuwa ulemavu haumzuii mtu kuwa na karama au uwezo wa kufanya jambo la maana.
“Chuma chenye mpini ni talanta zako, vipaji vyako. Ni uwezo ambao Bwana amekupa hata kama wewe ni mlemavu. Walemavu hawajanyimwa vyote.
“Unaweza ukawa mlemavu au mzima, ila chuma kikichomoka unabaki mpini ambao hauwezi kufanya chochote kwenye maisha yako. Kama chuma chako kimechomoka, endelea kumwambia Bwana akirejeshe mahali pake,” amesema.
Ameongeza " Watoto wa walemavu wana akili kuliko watoto wa watu wazima. Ni kwa sababu Bwana hajawanyima vyote. Mzima na mlemavu, chuma kikitoka mahali pake wote wanafanya madudu.
“Mwenye ulemavu akitumia vibaya karama ambayo Mungu amempa atakuwa fisadi kama mafisadi wengine. Atakuwa mwizi kama wezi wengine, atakuwa mzinzi kama wazinzi wengine na atafungwa gerezani ” amesema Mch. Nasari .



















Post a Comment