HEADER AD

HEADER AD

MEYA KIBAHA ATOA SIKU SABA KWA DAWASA WANANCHI MTAA WA MUHEZA WAWE WAMEPATA MAJI


Na Gustaphu Haule, Pwani

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas amempa siku Saba Mhandisi wa maji wa DAWASA Kibaha Betha George kuhakikisha wakazi wa Mtaa wa Muheza katika Kata ya Mailimoja wawe wamepata  maji.

Dr.Nicas ametoa wito huo Septemba 11,2026 wakati akizungumza na Wananchi wa Mtaa wa Muheza katika mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi ulioandaliwa na diwani wa Kata ya Mailimoja Ramadhani Lutambi.

       Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akizungumza na Wananchi wa Mtaa wa Muheza katika mkutano ulioandaliwa na diwani wa Kata ya Mailimoja Ramadhani Lutambi kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo.

Dr.Nicas amefikia hatua hiyo baada ya Wananchi wa Mtaa wa Muheza kutoa malalamiko juu ya ukosefu wa maji katika mkutano huo wakisema hadi sasa ni miaka mitatu hawana maji na wanatumia maji machafu ya visima vifupi ambayo sio salama kwa afya zao.

Kutokana na malalamiko ya Wananchi hao mhandisi wa maji wa Dawasa Kibaha Betha George aliwaeleza Wananchi hao kuwa anatambua changamoto ya eneo la Muheza juu ya ukosefu wa maji lakini katika kukabiliana na hali hiyo wameanzisha mradi mkubwa wa kimkakati Kata ya Pangani na mara ukikamilika Wananchi wa Muheza watapata maji ya kutosha.

Majibu ya Mhandisi huyo hayakumridhisha Meya wa Manispaa ya Kibaha ambapo alimuagiza mhandisi huyo kufanyakazi ya ziada kuhakikisha Wananchi wa Mtaa wa Muheza wanapata maji ndani ya wiki moja na endapo akishindwa kufanya hivyo basi Septemba 18/2026 siku ya Ijumaa wakutane ofisi kwake.

       Mhandisi wa maji kutoka Dawasa Kibaha Betha George akizungumza na Wananchi wa Mtaa wa Muheza katika mkutano uliofanyika Septemba 11,2026.

Dr.Nicas amesema kuwa suala la maji Mtaa wa Muheza limekuwa sugu kwani amekuja meneja mpya na wakamuita na meneja huyo aliomba kupewa wiki mbili ili kuleta maji Muheza lakini wiki mbili zikapita maji hakuna .

"Mimi nimekuja hapa kwa jambo  hili la maji maana watu hawa hawana maji kwa muda mrefu meneja aliomba wiki mbili zimekwisha, sasa wewe unatupiga stori na stori sisi hatutaki ,yaani tumekupeni wiki mbili hadi leo halafu unasema tuvumilie,sasa tuvumilie hadi lini na tuvumilie nini? amehoji Dr.Nicas

Dr.Nicas amesema yeye anataka maji yafike Muheza hakuna mjadala mwingine na kwamba ifikapo siku ya Alhamis ahakikishe maji yanatoka kwa wakazi wa Mtaa wa Muheza na endapo maji hayatapatikana basi siku ya Ijumaa wakutane ofisini kwake.

       Wananchi wa Mtaa wa Muheza katika Kata ya Mailimoja Manispaa ya Kibaha wakimsikiliza diwani wa Kata ya Mailimoja Ramadhani Lutambi katika mkutano uliofanyika Septemba 11,2026.

"Mhandisi tunakupeni hadi Alhamis ijayo maji yawe yamefika hapa na ikifika siku ya Alhamis kama utafika hapa kutambia maji hayajafika hapa basi ufike ofisini kwangu siku ya Ijumaa tuonane lakini naimani Muheza mtapata maji," amesema Dr.Nicas.

Amesema Rais Dr.Samia Suluhu Hassan anatamani kuona Watanzania wanapata tabasamu katika nchi yao huku akisema ukweli ni kwamba Rais Samia anafanyakazi kubwa ukilinganisha na awamu nyingine zilizopita.

Amesema zamani watu walikuwa wanapanga foleni kwa ajili ya kununua sukari katika duka moja na hata barabara ilikuwa kutoka Mwanza hadi kufikia Dar es Salaam ni wiki mbili lakini sasa hivi kila kitu kimerahisishwa.

Amesema hata hili la maji Rais hataki kuliona tena  bali anataka kuona maji yanapatikana kwa Wananchi kwahiyo watendaji wa ngazi za chini lazima wamsaidie Rais kutimiza malengo yake.

Amesema kero ndogo ndogo sio kazi ya Rais bali ni kazi ya watendaji wa ngazi ya chini kwahiyo pale ambapo kuna uwezekano wa kuondosha kero hizo basi ziondoshwe maramoja ili Wananchi wapate huduma stahiki.

Amesema anashangaa wakati mwingine maji hayatoki lakini utakuta Wananchi wanaletewa bili jambo ambalo sio sawa na kwamba kwa changamoto ya Muheza wameichkua kwa uzito na Wananchi watapata maji.

Diwani wa Kata ya Mailimoja Ramadhani Lutambi amemshukuru Meya wa Manispaa ya Kibaha kwa kusimamia jambo hilo kwakuwa Wananchi wa Muheza wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji kwa miaka mingi.

         Diwani wa Kata ya Mailimoja katika Manispaa ya Kibaha Ramadhani Lutambi akizungumza na Wananchi wa Mtaa wa Muheza katika mkutano wake uliofanyika Septemba 11,2026.

Lutambi amesema kuwa Mtaa wa Muheza una wakazi zaidi ya 12000 lakini watu zaidi ya 8000 hawapati maji licha ya kuwa wamekuwa na miundombinu ya maji kwa muda mrefu.

Amesema awali walikuwa wanapata maji lakini kutokana na bomba lililokuwa linatumika kupeleka maji katika Mtaa wa Muheza kuzidiwa na ndio maana spidi imekuwa ndogo na yanashindwa kwenda Muheza kwakuwa kutoka Mailimoja kwenda Muheza kumekuwa na mwinuko mkubwa.

Lutambi amesema Agosti ,2024 Wananchi walipeleka maombi ya kuunganishiwa maji na ombi hilo lilitolewa mbele ya Mkuu wa Wilaya lakini hadi leo maji hakuna  na Wananchi wanazidi kuteseka.

Lutambi ,amewaomba Wananchi wa Mtaa wa Muheza kuendelea kuwa wavumilivu kwakuwa jambo hilo lipo mikononi mwa Meya na tayari ametoa maelekezo kwa mhandisi wa maji basi ni vyema wakatoa muda wa kuhakikisha Mhandisi huyo analeta maji .

          Wananchi wa Mtaa wa Muheza katika Kata ya Mailimoja Manispaa ya Kibaha wakimsikiliza kwa makini diwani wa Kata ya Mailimoja Ramadhani Lutambi ( hayupo pichani).

Lutambi amesema mbali na changamoto ya maji lakini anatambua Muheza kuna changamoto ya barabara ambapo hadi sasa Halmashauri ya Manispaa wameliwekea mkakati kuhakikisha changamoto hiyo inakwisha.

Amesema barabara ya Sheli - Muheza ipo katika mkakati wa kujengwa kwa kiwango cha lami kupitia mradi wa Tactic ambapo kinachosubiriwa ni kulipa fidia kwa Wananchi 65 mpango ambao utaanza hivi karibuni.

Amesema baada ya kumaliza kulipa fidia hiyo Wananchi watapewa siku 90 kuhakikisha wanahamisha na kuvunja nyumba zao na baada ya kufanyika kwa mchakato huo ndipo barabara itaanza kujengwa kwahiyo amewaomba Wananchi wa Mtaa huo kuwa wavumilivu wakati jitihada mbalimbali zikiendelea kufanyika.

No comments