HEADER AD

HEADER AD

MENEJA KIWANDA CHA KINGLION AIOMBA SERIKALI KUTENGENEZA BARABARA


Na Gustaphu Haule, Pwani

MENEJA wa kiwanda cha Kinglion kinachojishughulisha na uzalishaji wa bati za aina mbalimbali kilichopo Mtaa wa Zegereni Kata ya Misugusugu Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Kelvin Richard ameiomba Serikali kuwatengenezea barabara inayoingia kiwandani hapo ili waweze kusafirisha bidhaa zao kirahisi.

Richard, amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilomita mbili ni ya vumbi na imekuwa ni changamoto kubwa kwani  wakati wa mvua haipitiki na hivyo kushindwa kusafirisha bidhaa zao.

Richard, ametoa ombi hilo mwishoni mwa wiki iliyopita mbele ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas aliyetembeleea kiwandani hapo kwa ajili ya kutaka kujua changamoto zinazowakabili.

Amesema hitaji lao kubwa ni kuona barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami kwakuwa wamekuwa wakikumbana na changamoto ya magari kunasa wakati wa mvua hali ambayo wakati mwingine inapelekea kusimamisha uzalishaji .

Richard amesema kama barabara hiyo itajengwa vizuri itakuwa mkombozi mkubwa kwa wawekezaji wa viwanda wanaotumia barabara hiyo lakini hata mapato ya Serikali yataongezeka.

     Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akifanya kikao na viongozi wa Kiwanda cha Kinglion mwishoni mwa wiki alipotembelea kiwanda hicho kwa ajili ya kujua changamoto zinazowakabili.

"Mstahiki Meya sisi tunafurahi kuja hapa kututembelea lakini kilio chetu kikubwa ni barabara hii tunayoitumia kwani imekuwa ni changamoto kubwa kwetu, kwahiyo tunaomba mtusaidie kuijenga ili iweze kupitika muda wote,"amesema Richard.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas amesema barabara hiyo inajulikana kwa jina la Zegereni Industrial five ambayo kwa mujibu wa Tarura imebainika kuwa endapo wakijenga kwa kiwango cha changarawe bado haitasaidia.

        Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akizungumza  katika kikao cha pamoja na viongozi wa kiwanda cha Kinglion pamoja na wataalam mbalimbali wa Manispaa ya Kibaha.

Dr.Nicas amesema Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini(TARURA) wameshauri barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami na Manispaa imekubali ushauri huo ili kuwasaidia wawekezaji wanaotumia barabara hiyo.

Aidha, Dr Nicas amesema hadi sasa tayari mipango ya kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami imekamilika na itajengwa haraka iwezekanavyo na haitachukua muda kuanza kujengwa kwakuwa umuhimu wake ni mkubwa kwani inahudumia viwanda vikubwa tisa ambavyo vinalipa kodi kubwa.

"Nimekuja hapa kuwatia moyo na leo nawaambia Manispaa ya Kibaha ipo katika mpango maalum wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kwani mchoro upo tayari na sasa majadiliano yaliyopo ni namna ya kujenga kwamba wasubiri mvua za El-nino zipite au waanze sasa? amesema Nicas.

Dr.Nicas amesema kuwa Manispaa ya Kibaha ipo pamoja na wawekezaji  na inataka kuona wawekezaji wanafanya shughuli zao katika mazingira mazuri na kama kuna sehemu zipo changamoto lazima zitatuliwe.

Amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kuhakikisha kila mwekezaji anayeingia nchini anavutiwa kuwekeza na kwamba Manispaa ya Kibaha inafuata miongozo ya Rais ili kuhakikisha malengo yanatimia.

Amesema uwekezaji uliofanywa Kibaha umesaidia kwa kiasi kikubwa kuzalisha ajira za vijana na hata kuongeza mapato ya Taifa kupitia kodi wanazolipa lakini amewaomba wawekezaji hao kutunza mazingira kwa kujenga miundombinu mizuri ya kutolea maji machafu.

No comments