HEADER AD

HEADER AD

MEYA KIBAHA AWAFUNDA WAZAZI NA WALEZI WA WANAFUNZI SHULE YA MSINGI LULANZI

Na Gustaphu Haule,Pwani 

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas amewafunda Wazazi na walezi wa wanafunzi wa Shule ya Msingi Lulanzi iliyopo Kata ya Picha ya Ndege kuwekeza elimu kwa watoto wao kwakuwa ndio urithi pekee utakaoweza kuwasaidia katika maisha yao.

Dr.Nicas ameeleza kusikitishwa na baadhi ya Wazazi ambao wamekuwa na tabia ya  kuwatelekeza watoto wao hasa pale linapokuja suala la kuchangia katika elimu na kusema wengi wao wanakuwa nyuma kwa madai ya kuwa na kipato kidogo.

        Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Nicas Mawazo akizungumza katika mahafali ya 16 ya  darasa la Saba katika Shule ya Msingi Lulanzi Kata ya Picha ya Ndege yaliyofanyika Septemba 18/2026.

Dr.Nicas amewafunda Wazazi na walezi hao kwenye mahafali ya 16  ya wanafunzi wa darasa la Saba wa Shule ya Msingi Lulanzi yaliyofanyika Shuleni hapo Septemba 18/2026 yakiwa yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali,walimu ,wanafunzi na Wananchi.

Amesema Wazazi wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza watoto wao juu ya umuhimu wa elimu pamoja na kuhakikisha wanachangia kikamilifu masuala ya elimu katika Shule zao.

      Wanafunzi wa darasa la Saba katika Shule ya Msingi Lulanzi iliyopo Kata ya Picha ya Ndege wakifurahi kwa kucheza katika mahafali yao yaliyofanyika Shuleni hapo Septemba 18/2026.

Amesema yapo mambo makubwa ambayo yamefanywa na Serikali hususani katika kujenga miundombinu ya madarasa,na vifaa vingine vya kufundishia lakini yapo mambo madogo ambayo hayapaswi kusubiri Serikali.

"Tukitaka tusongembele katika elimu lazima wazazi tujitoe katika kuchangia kwani yapo mambo madogo ambayo kama Wazazi tukikubaliana tunaweza kufanya kwa faida ya watoto wetu ,hivyo niwaombe linapokuja suala la kuchangia mahali fulani basi kwa pamoja tushiriki,"amesema Dr .Nicas 

Dr .Nicas amesema Wazazi wasijaribu kutelekeza watoto katika suala la elimu kwakuwa elimu ndio urithi pekee wa watoto ambao utawasaidia katika maisha yao kuliko kuwarithisha nyumba na magari ya kifahari.

     Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Nicas Mawazo akivishwa skafu mara baada ya kuwasili katika Shule ya Msingi Lulanzi iliyopo Kata ya Picha ya Ndege kwa ajili ya mahafali ya darasa la Saba ya Shule hiyo

Amesema kumrithisha mtoto nyumba na magari hakutamsaidia kimaisha badala yake umemuongezea ugumu katika maisha yake kwani hatojui mali hizo zimepatikanaje na mwisho wake mtoto kubaki maskini.

Dr.Nicas ameahidi kuendelea kushirikiana na Wazazi hao ili kuleta mabadiliko chanya ya kuboresha elimu katika Shule mbalimbali zilizopo ndani ya Manispaa ya Kibaha ili kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira mazuri na hata walimu pia.

         Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Nicas Mawazo ( Kulia mwenye skafu) akizungumza na viongozi wa Shule ya Msingi Lulanzi.

Mkuu wa Shule ya Msingi Lulanzi Bakari Salum ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya elimu katika Shule hiyo hususani kwa kujenga vyumba vya madarasa na vifaa vya kufundishia.

Salum amesema kuwa pamoja na mafanikio makubwa ya Shule hiyo lakini kwasasa wanakabiliwa na changamoto ya uzio wa Shule ambapo ameiomba Serikali kuwasaidia kupata uzio ili wanafunzi na Walimu wawe katika mazingira yenye usalama .

     Wanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Lulanzi wakiwa katika mahafali yao yaliyofanyika Shuleni hapo Septemba 18/2026.

Akisoma risala kwa mgeni rasmi mwanafunzi wa darasa la Saba Janeth Mwangi ,amesema Shule hiyo ilianzishwa  mwaka 2007 lakini hadi sasa imepiga hatua kubwa ikiwemo ongezeko la miundombinu ya madarasa.

Hatahivyo,Mwangi ameiomba Serikali kupitia wadau mbalimbali waone namna ya kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili Shule hiyo ikiwemo ujenzi wa uzio pamoja na jengo la utawala .


No comments