MEYA KIBAHA AWATAKA WENYEVITI WA BODI ZA SHULE KUAINISHA CHANGAMOTO ZA UKOSOFU WA MABWENI

Na Gustaphu Haule, Pwani
MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas amewataka wenyeviti wa bodi za Shule za Sekondari zilizopo katika Manispaa hiyo kuainisha changamoto ya ukosefu wa mabweni kama hitaji muhimu katika Shule zao.
Dkt.Nicas amesema endapo wenyeviti hao wataliweka jambo hilo katika kipaumbele litasaidia Manispaa ya Kibaha kupitia mkurugenzi wake kulisimamia jambo hilo na hivyo kuweka mkakati wa pamoja wa kuhakikisha kila Shule ya Sekondari yenye uhitaji wa mabweni hayo yanajengwa.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akizungumza na Wazazi, walimu, wanafunzi na Wananchi katika hafla ya kukabidhi mashine ya kutolea kopi kwa Shule ya Sekondari Mwambisi iliyopo Kata ya Kongowe.
Dkt .Nicas ametoa wito huo Septemba 08/2026 wakati akizungumza na Wazazi,walimu,wenyeviti wa bodi za Shule ,wanafunzi na wadau mbalimbali wa elimu katika hafla fupi ya kukabidhi mashine ya kutolea kopi( Photocopy Mashine) kwa Shule ya Sekondari Mwambisi iliyopo Kata ya Kongowe.
Amesema kuwa yeye amepita moja ya Mkoa amekuta kila Shule ya Sekondari ina mabweni na kwamba hata Manispaa ya Kibaha ikijipanga vizuri inaweza kufikia malengo ya kutatua changamoto ya ukosefu wa mabweni katika Shule zake.
Dr.Nicas amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt .Samia Suluhu Hassan amefanyakazi kubwa ya kujenga Shule nchi nzima kwani ametaka kila mwanafunzi hapate elimu.
Amesema Rais Samia ndio shujaa wa masuala ya afya ,elimu na mazingira na ndio maana mambo yote mazuri yamefanyika katika kipindi cha uongozi wake na hata kama miundombinu Rais amejenga madaraja na barabara nchi nzima.
Amewataka wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwambisi na Shule nyingine zilizopo ndani ya Manispaa ya Kibaha kupuuza habari za mitandaoni zinazomvunja nguvu Rais Samia na badala yake waipongeze Serikali kwa kazi kubwa inayofanyika.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwambisi iliyopo Kata ya Kongowe Manispaa ya Kibaha wakishiriki katika zoezi la kupokea mashine ya kutolea Kopi kutoka kwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas.
Dr.Nicas ameongeza kuwa miaka ya zamani wanafunzi waliokuwa wanaenda Sekondari ni wawili hadi watatu lakini siku hizi wanafunzi wote wanafaulu na wanapata nafasi ya kwenda Sekondari.
"Kwakweli huyu Rais apewe haki yake na ikiwezekana wazazi , wanafunzi na Wananchi kwa ujumla waeleze mambo ambayo yamefanywa na Rais kwani wote tunaona kwa macho yetu jinsi ambavyo nchi inapiga hatua kimaendeleo ,"amesema Nicas
Dkt.Nicas amewapongeza walimu wa Shule Sekondari Mwambisi kwa kutokomeza utoro na kufuta ziro katika matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2025 ambapo amewataka walimu wa shule nyingine kutumia mbinu za walimu wa Mwambisi kuhakikisha katika Shule zao wanafanikiwa kutokomeza utoro na kufuta ziro.
Wananchi wa Kata ya Kongowe wakishiriki hafla ya kukabidhi mashine ya kutolea kopi katika Shule ya Sekondari Mwambisi , mashine hiyo imetolewa na Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas.
Katika hatua nyingine Dr.Nicas amemuagiza Afisa Elimu wa Sekondari wa Manispaa ya Kibaha Theresia Charles kuhakikisha anayachukua majina yote ya
walimu wanaofundisha kwa kujitolea ili Manispaa ione namna ya kuwapa mikataba mifupi huku wakiendelea kuona namna ya kuwatafutia ajira ya kudumu.
Kuhusu mashine ya kutolea kopi aliyoikabidhi Shuleni hapo Dr.Nicas amesema kuwa ametoa mashine hiyo ili kupunguza mzigo kwa walimu na Wazazi kuchangia fedha za mitihani katika shule hiyo.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akikata utepe ikiwa ni ishara ya kukabidhi Mashine ya kutolea kopi kwa Shule ya Sekondari Mwambisi hafla ambayo imefanyika Septemba 08/2026 Shuleni hapo.
Afisa Elimu wa Sekondari katika Manispaa ya Kibaha Theresia Charles amesema kuwa malengo ya Manispaa ya Kibaha ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaomaliza kidato cha nne wanaishi kupata daraja la pili pekee ( Division two).
Charles amesema anaipongeza Shule ya Sekondari Mwambisi kwa kuhakikisha wanafuta ziro katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2025 ambapo amewaomba wenyeviti wa bodi waende katika shule zao kuweka msisitizo ili kuondoa utoro kwa baadhi ya wanafunzi hatua ambayo itasaidia wanafunzi kufanya vizuri darasani.
Mwenyekiti wa kamati ya shule Hamza Duruge amesema mafanikio ya Shule ya Sekondari Mwambisi yametokana na ushirikiano kati ya Walimu ,Wazazi na Wananchi kwani awali watoto wengi walikuwa wakiingia katika vitendo vya uhalifu ikiwemo kuvutia bangi.
Duruge amesema anawashukuru Wazazi kwa kutoa ushirikiano juu ya kutokomeza vitendo vya uhalifu Shuleni hapo huku akimshukuru Mkuu wa Shule hiyo kwa uwazi katika matumizi ya fedha za ruzuku zinazotolewa na Serikali.
Duruge amemshukuru Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas kwa kukubali kutoa fedha kiasi cha Sh.milioni 1.6 kwa ajili ya kuchangia katika ununuzi wa mashine hiyo.
Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akiwa na baadhi ya madiwani pamoja na viongozi mbalimbali wakati akikabidhi mashine ya kopi kwa Shule ya Sekondari Mwambisi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Kibaha Mjini Yahaya Mtonda amempongeza Meya wa Manispaa ya Kibaha kwa kuonyesha dhamiri njema ya ujenzi wa mabweni katika Shule za Sekondari .
Mtonda amesema pamoja na kujenga mabweni hayo lakini pia amemuomba Meya huyo kuweka msisitizo juu ya ujenzi wa kidato cha tano na Sita katika Sekondari ya Mwambisi.
Hata hivyo,Mtonda amesema kitendo cha kuipandisha hadhi Shule hiyo hadi kufikia kidato cha tano kutasaidia wanafunzi wengi hasa wanaoishi katika Kata ya Kongowe kupata nafasi ya kupangiwa katika Shule hiyo.





Post a Comment