HEADER AD

HEADER AD

TAKUKURU PWANI KUFIKA KATA KWA KATA KUTOA ELIMU KWA WANANCHI USIMAMIZI WA MIRADI YA MAENDELEO

 


Na Gustaphu Haule,Pwani 

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imeanza  kupita Kata kwa Kata kwa ajili ya kutoa elimu juu ya usimamizi wa miradi ya maendeleo kwa viongozi, Wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Mbali na elimu kuhusu usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo lakini pia TAKUKURU katika programu hiyo  inatoa elimu dhidi ya mapambano ya rushwa pamoja na kufanya vikao vya TAKUKURU Rafiki.
     Viongozi mbalimbali wa Kata ya Kibaha katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wakishiriki mafunzo maalum yaliyokuwa yakitolewa na TAKUKURU Mkoa wa Pwani Septemba 07/2026.

TAKUKURU tayari imeanza kutoa elimu hiyo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha na hadi sasa Takukuru imewafikia viongozi na Wananchi wa Kata ya Visiga, Misugusugu, Kongowe, Viziwaziwa na  Kibaha ambapo Septemba 08/2026 itaendelea katika Kata ya Msangani.

Akizungumza kuhusu matumizi ya fedha za miradi ya umma (PETS) katika mafunzo yaliyofanyika Septemba 07/2026 katika Kata ya Kibaha afisa ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo TAKUKURU Mkoa wa Pwani Juliana Bulinda amesema Takukuru Mkoa wa Pwani kwasasa imeshuka  katika kutoa elimu kwa jamii.

      Afisa ufuatiliaji wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani Juliana Bulinda akizungumza wakati akitoa elimu kwa viongozi wa Kata ya Kibaha , Wananchi na Wajasiriamali.

Bulinda amesema kuwa TAKUKURU imekuja na programu maalum ya ufuatiliaji wa fedha za  miradi ya maendeleo (PETS) ambapo kazi ya programu hiyo ni kuangalia ushirikishwaji wa Wananchi katika mradi husika iliyopo ndani ya maeneo yao na kuangalia wajibu wa wataalam juu ya kuitisha vikao  kuhusu kupitisha mradi husika.

Amesema jambo lingine ni kuangalia ucheleweshaji wa mradi nani alihusika,fedha za mradi zimetoka wapi,zilifika lini na nani alizipokea ,pamoja na kuangalia thamani ya fedha za  mradi( Value for Money).

      Mafunzo maalum yaliyokuwa yakitolewa na Takukuru Mkoa wa Pwani Septemba 07/2026 kwa viongozi wa Kata ya Kibaha.

Amesema kwenye thamani ya fedha za mradi wanaangalia ubora wa mradi,vifaa vilivyotumika kama vinalingana na fedha iliyotumika, mradi ulitakiwa kukamilika lini na ulianza lini,kujua kama utaratibu wa mradi ulikuwa wa wazi,kujua mfumo  wa manunuzi, uvujaji wa fedha za mradi na mambo mengine mbalimbali.

"Utakuta kitasa cha mlango kinauzwa Sh.elfu 50,000 lakini kwakuwa ni mradi wa Serikali basi utakuta mtu anakuambia amenunua kitasa kwa Sh.200,000, jambo ambalo sio sawa na haliwezi kukubalika kwa Takukuru halafu Kibaya mtu huyohuyo akienda kununua kitasa cha nyumbani kwake anaweza kununua hadi chini ya Sh.50,000,"amesema Bulinda.

Bulinda amewaomba wadau kutoa ushirikiano hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akisisitiza wataalam na Wananchi ndani ya Kata washirikiane katika usimamizi wa miradi ya maendeleo na ikiwezekana watoe taarifa juu ya vitendo vinavyoendelea katika miradi ya eneo lao.

Afisa wa TAKUKURU Kitengo cha Elimu Aneth Mwakatobe amesema kuwa lengo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuleta ustawi wa Jamii, kushirikiana katika amani na kutokomeza rushwa.

       Afisa wa TAKUKURU kitengo cha Elimu Aneth Mwakatobe akitoa elimu ya jumla kuhusu mapambano dhidi ya rushwa kwa viongozi wa Kata ya Kibaha , Wananchi na Wajasiriamali katika mafunzo maalum yaliyofanyika Septemba 07/2026.

Mwakatobe,amesema kuwa rushwa uathiri utoaji wa huduma za jamii na kwamba katika bajeti ya Serikali fedha nyingi zinaenda kwenye miradi ya maendeleo na lengo la kufanya hivyo ni kutoa huduma bora kwa Wananchi.

Amesema sasa hivi wapo katika kutekeleza dira ya mwaka 2050 na Serikali inataka  kila mwananchi afikie wastani wa dola 7000 kwahiyo jukumu la Takukuru ni Kupambana na Kuzuia Rushwa ili kuweza kufikia malengo ya Serikali.

Nae afisa mchunguzi wa TAKUKURU Ally Nakapala amesema kuwa TAKUKURU inafanyakazi kwa kutumia vifungu vya kisheria na sheria ya rushwa huwa inabadilika mara kwa mara.

       Afisa uchunguzi wa Takukuru Mkoa wa Pwani Ally Nakapala akitoa elimu kwa viongozi wa Kata ya Kibaha , Wananchi na Wajasiriamali kuhusu Sheria ya TAKUKURU.

Nakapala amesema kuwa Sheria ya TAKUKURU awali ilikuwa na makosa manne lakini kwasasa ina makosa 25 na kwamba lengo la Takukuru inataka rushwa iishe au ipungue kwa asilimia kubwa .

Christina Paulo afisa wa TAKUKURU Mkoa wa Pwani alitoa mada kuhusu Takukuru Rafiki ambapo amesema mwaka 2022 mwishoni ilianzishwa mpango wa Takukuru Rafiki lengo ilikuwa ni kuongeza wadau katika ushiriki wa mapambano dhidi ya rushwa hususani katika huduma na usimamizi wa miradi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwendapole Muhidini Muhidini amesema ameridhishwa na mafunzo ya TAKUKURU kwani amejifunza mengi mazuri hasa katika ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo katika eneo lake.

      Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mwendapole Kata ya Kibaha  Muhidini Muhidini akifungua Mkutano wa mafunzo maalum yaliyokuwa yakitolewa na Takukuru Mkoa wa Pwani Septemba 07/2026

Muhidini amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka na ameahidi kuyafanyikazi lakini ameomba TAKUKURU Mkoa wa Pwani kuendelea kushirikiana kwa karibu kwa kutoa elimu ambayo itawasaidia Wananchi wa eneo hilo.

Nae afisa Maendeleo ya Jamii wa Kata ya Kibaha Regina Lazaro ameipongeza TAKUKURU Mkoa wa Pwani kwa kutoa elimu hiyo ambapo ameomba elimu hiyo itolewe kwa mapana kupitia vikundi mbalimbali kwani wakifanya hivyo elimu itafika mbali zaidi.

       Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kibaha Regina Lazaro akizungumza jambo katika mafunzo ya Takukuru Mkoa wa Pwani yaliyofanyika Septemba 07/2026 katika Mtaa wa Mwendapole.


No comments