MEYA KIBAHA : WAMILIKI WA VIWANDA HAKIKISHENI MNATENGENEZA MIUNDOMBINU YAKUTIRIRISHA MAJI

Na Gustaphu Haule, Pwani
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo nicas amewataka wamiliki wa viwanda kuhakikisha wanatengeneza miundombinu mizuri ya kutiririsha maji yanayotoka katika viwanda hivyo ili yasiweze kuathiri wananchi.
Dr.Nicas ameeleza kufurahishwa na uongozi wa kiwanda cha kutengeneza karatasi cha Fortune Paper kilichopo Mtaa wa Saeni Kata ya Misugusugu kwa kutekeleza agizo lake alilolitoa kiwanda hapo miezi minne iliyopita la kuwataka kujenga miundombinu mizuri ya utiririshaji maji hayo.
Dr, Nicas ametoa kauli hiyo Septemba 24/2026 wakati akiwa katika ziara yake ya kutembelea na kukagua miundombinu ya maji katika kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya kuchukua tahadhari juu ya mvua za El-nino.
Amesema awali alipita katika kiwanda hicho na kukuta maji machafu yanaelekea kwa wananchi na kutoa muda wa siku saba kuhakikisha miundombinu hiyo inaimarishwa lakini amerudi kuhakikisha kama maagizo yake yametekelezwa.
"Kwakweli naupongeza uongozi wa kiwanda hiki kwa kufanya vizuri kwani leo nimekuja hapa nimeona yale maji yaliyokuwa yanatiririka kwa wananchi yamedhibitiwa na miundombinu yake imeimarishwa kwani wasiwasi wangu ulikuwa endapo mvua ya El-nino ikinyesha hali ya wananchi ingekuwaje,"Amesema Dr.Nicas.
Dr.Nicas amesema Rais Dr.Samia Suluhu Hassan ameweka mazingira mazuri kwa wawekezaji na Manispaa ya Kibaha inatekeleza maono ya Rais kwa kuhakikisha wawekezaji hawasumbuliwi lakini lazima wahakikishe pia wananchi wanakuwa salama.
Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akimsisitiza meneja biashara wa kiwanda cha Fortune Paper kilichopo Mtaa wa Saeni Kata ya Misugusugu Colin Yang kuendelea kutunza mazingira hasa katika kuhakikisha wanadhibiti maji yanayotoka kiwandani.Afisa mazingira wa kiwanda hicho Daudi Tito, ameushukuru uongozi wa Halmashauri kwa ushauri na maelekezo waliyoyatoa kuhusu udhibiti wa maji hayo na kwamba wapo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali hususani katika kukabiliana na majanga ya El-nino.
Katika hatua nyingine Dr.Nicas amewahakikishia wawekezaji wa viwanda wa eneo la Zegereni kujenga barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa Kilomita 2 inayojulikana kwa jina la Zegereni Industrial five ambayo inahudumia viwanda tisa kikiwemo kiwanda cha Kinglion.
Amesema Manispaa ya Kibaha kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) tayari wameweka mpango wa kujenga barabara hiyo na muda wowote ujenzi huo utaanza kwani lengo ni kuhakikisha mazingira ya wawekezaji yanaendelea kuboreshwa ili waweze kusafirisha bidhaa zao kwa wakati.
Meneja biashara wa kiwanda cha Fortune Paper Colin Yang (kushoto) akimuelekeza jambo Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas alipokwenda kutembelea miundombinu ya maji katika kiwanda hicho Septemba 24/2026."Nimekuja hapa kuwatembelea na kuwatia moyo kwani natambua hitaji lenu kubwa ni barabara na sisi tayari tumeweka mipango mizuri ya kujenga barabara kwa kiwango cha lami na hapa tunaangalia tuanze kabla ya mvua ya El-nino au baada lakini muda wowote tegemeeni kuona mambo mazuri,"amesema Nicas.
Meneja wa kiwanda cha Kinglion Kelvin Richard amesema kuwa wakati wa mvua wanashindwa kusafirisha bidhaa zao kwakuwa barabara haipitiki ambapo ameiomba Serikali kuharakisha mpango wa ujenzi wa barabara hiyo.
Hata hivyo,Richard amesema kama barabara hiyo itakuwa nzuri na yenye kupitika muda wote ni wazi kuwa uzalishaji wake utaongezeka lakini hata mapato ya Manispaa yataongezeka pia.



Post a Comment