HEADER AD

HEADER AD

MEYA KIBAHA : WANANCHI PIMENI NA KURASIMISHA MAENEO YENU


Na Gustaphu Haule, Pwani

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dr.Mawazo Nicas amesema Manispaa imeanza kurasimisha na kupatia hati maeneo ya Serikali, ikiwemo maeneo ya shule na zahanati ili kuzuia migogoro ya ardhi.

Amesema wanatarajia ifikapo Februari 2027 maeneo yote ya Serikali yawe yamepimwa na kutambulika kisheria huku akiwataka wananchi pia kupima na kurasimisha maeneo yao ili kulinda mali zao na kuepuka migogoro.

Dr. Nicas ameyasema hayo Septemba 23/2026 wakati akizungumza na wazazi, walimu, wanafunzi na viongozi mbalimbali  wa Serikali katika Mahafali ya tatu ya Shule ya Msingi Kanesa iliyopo Kata ya Kongowe .

       Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu wa darasa la saba katika shule ya Msingi Kanesa.

Amesema kuwa migogoro mingi ya ardhi inatokana na kutokuwepo na umiliki usio wa kisheria hivyo Manispaa ya Kibaha inataka kuondokana na hali hiyo kwa kuhakikisha kila mradi wa serikali ikiwemo Shule na Zahanati zinapata hati.

Amesema Halmashauri imejipanga vizuri si tu katika kupima na kutoa hati katika miradi ya Serikali lakini pia hata kwa wananchi kwakuwa vifaa vimenunuliwa na wataalamu wa kufanyakazi hiyo watatoka katika Manispaa ya Kibaha.

Kuhusu elimu Dr.Nicas amesema Rais Dkt .Samia Suluhu Hassan ameendelea  kuweka sekta ya elimu kuwa kipaumbele kwa kuboresha miundombinu ya shule na kuongeza walimu ambapo Manispaa nayo imejikita katika ujenzi wa ofisi za walimu na inatarajia ifikapo mwisho wa mwaka huu shule za Manispaa zitakuwa na ofisi hizo.

Dr.Nicas amewataka wazazi kushirikiana na Serikali katika ujenzi wa ofisi za walimu pamoja na changamoto ili kuwawezesha walimu kufanya kazi katika mazingira salama na bora.

Amewataka wanafunzi kuzingatia nidhamu na masomo, akisema Taifa linawategemea na wanapaswa kujiandaa kuingia katika ushindani wa soko la dunia ambapo ametaka wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shuleni.

       Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wanaohitimu darasa la saba shule ya Msingi Kanesa , walimu na viongozi mbalimbali katika mahafali yaliyofanyika Septemba 23/2026.

Amesema Manispaa ya Kibaha itawachukulia hatua na kutoa adhabu kali kwa mzazi ambaye atabainika kukaa na mtoto wake nyumbani bila sababu kwakuwa miundombinu imejengwa na serikali kwasababu yao.

"Serikali kupitia Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imejenga miundombinu ya shule nchi nzima ili watoto wasome lakini kizuri zaidi watoto wanasoma bila malipo kwahiyo hakuna sababu kuona mtoto anazurula mtaani na endapo tukabaini mtoto aendi shule tutamchukulia hatua za kinidhamu,"amesema Nicas

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kanesa Jordan Ngailo amesema kuwa shule yake imeanzishwa kutoka katika shule mama ya Kongowe kupitia mradi wa Boost.

Ngailo, amesema changamoto kubwa ya shule hiyo kwasasa ni pamoja na ukosefu wa samani za shule kwani wakati mwingine walimu wanalazimika kusimama kwakuwa viti na meza havitoshi.

        Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akisalimiana na mmoja wa walemavu katika  mahafali ya darasa la saba katika shule ya Msingi Kanesa Kongowe.

Amesema changamoto nyingine ni ukosefu wa uzio hali inayopelekea wananchi kupita shuleni hapo kama njia ya kudumu jambo ambalo linasababisha kuwepo kwa usalama mdogo kwa walimu na wanafunzi wao.

Amesema Kuhusu ujenzi wa uzio tayari walikubaliana na wazazi katika kikao chao cha pamoja kuchangia kila mzazi matofali matano na hadi sasa wamefanikiwa kupata matofali 415 ambayo wataanzia katika ujenzi huo.

Ngailo, amewaomba wazazi, wananchi na wadau mbalimbali kujitokeza katika kusaidia kutatua changamoto za shule hiyo hususani katika samani za walimu na hata katika ujenzi wa uzio wa shule hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya African Company Limited ijayojishughulisha na uundaji na uuzaji wa magari Hafidh Amiri amesema wamekuja shuleni hapo na wamezipokea changamoto za Shule hiyo.

Amiri amesema kuwa kampuni yake ipo tayari kuungana mkono juhudi za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kuboresha elimu hapa nchini ambapo ameahidi kuchangia samani za shule hiyo ikiwemo meza na viti 48 kwa ajili ya walimu.



No comments