MVIWAKA YATOA MAFUNZO YA USINDIKAJI KWA VIKUNDI VITANO
Na Alodia Dominick, Bukoba
MTANDAO wa vikundi vya wakulima, wavuvi na wafugaji Kagera (MVIWAKA) wamesaidia vikundi vitano kutoka wilaya mbalimbali mkoani hapa kufanya ziara ya mafunzo juu ya usindikaji na ufungashaji katika kiwanda cha kusindika kahawa cha TANICA kilichopo Bukoba mjini mkoani Kagera.
Ziara ya mafunzo imefanyika mwishoni mwa wiki hii ambapo wanufaika wa mafunzo walikuwa ni viongozi wa vikundi vitano vya Tuinuane group cha Kahanga -Muleba ambacho kinajishughulisha na ujasiliamali wa dagaa, Upendo group kilichopo Muleba mjini kinajishughulisha na uchakataji wa senene na lishe.
Vikundi vingine ni Mviwaki kilichopo Kyerwa kinajishughulisha na kilimo, ufugaji na uvuvi wa samaki, kikundi cha Msamalia Fgr kilichopo Bukoba vijijini kinajihusisha na kilimo cha miti na ufugaji wa nyuki na kikundi cha Kaweao kilichopo Muleba kinachojihusisha na uzalishaji wa mvinyo na usindikaji dagaa.
Akitoa mafunzo kwa vikundi hivyo Meneja masoko na kaimu meneja katika kiwanda cha TANICA Zacharia Membo amesema kuwa, wadau wa maendeleo waendelee kutoa elimu kwa wakulima ili waendelee kufuata taratibu za kilimo bora na wahame kwenye kilimo cha mazoea.
"Nyinyi kama viongozi wa vikundi nawaomba muendelee kuwashauri wakulima waendelee kufuata taratibu bora za kilimo kwani tafiti zinaonyesha kwamba mkahawa wa kisasa baada ya kupandwa miaka miwili na nusu unaanza kuvuna na baada ya miaka mitano hapo anaanza kupata mavuno mengi"
"Tuwashauri wakulima wahame kwenye kilimo cha mazoea ambacho hakina tija badala yake walime kilimo cha kisasa ukipanda mbuni ukaipa nafasi inayopaswa ukaweka mbolea, kwa miaka mitano unaweza kukupa hata kilo 10 lakini ukipanda kwa mazoea unakuta mbuni ule ule unakupa kilo mbili" amesema Membo
Ofisa uthibiti ubora katika kiwanda cha TANICA Lilian Emmanuel akitoa elimu kwa vikundi hivyo amesema, katika kuthibiti ubora wanajikita katika usafi na kiwango cha unyevunyevu.
Amesema, TANICA wananunua kahawa iliyokobolewa kutoka kwa wabia wao na wanahakikisha wakati wa usafirishaji magari yanayopakia kahawa ni masafi na hayana harufu ya kitu chochote.
Ofisa programu wa mtandao wa vikundi vya wakulima, wavuvi na wafugaji Mkoa wa Kagera Sylivand Mugere ameeleza kuwa, vikundi hivyo vilivyopata ziara ya mafunzo viliibuka mshindi katika maadhimisho ya wakulima nanenane mwaka huu na kupewa zawadi ya ziara ya mafunzo na kuwa ni kati ya vikundi 20 vilivyoshiriki katika nane nane.
Nao washiriki wa ziara ya mafunzo wameeleza kufurahishwa na mafunzo hayo kwani richa ya kujifunza kwa nadharia pia wametembelea kiwandani na kijionea shughuli mbalimbali za usindikaji katika kiwanda hicho na wamepata uelewa juu ya masoko na usindikaji.
Bertha Andrew katibu wa MVIWAKA amesema, mafunzo hayo yataleta tija kwao kwani elimu waliyoipata imewafungua akili.
Amewaomba TANICA kuanzisha vijiwe vya kahawa kila kata hapa mkoani Kagera ili wananchi watofautishe kahawa nzuri ya TANICA na kahawa ya watu wengine.
Andrew aliwatia moyo wakulima na kuwataka kutokata tamaa badala yake waendelee kulima na kufuga ili walinde ikorojia.





Post a Comment