HEADER AD

HEADER AD

MWENYEKITI CCM KIBAHA : HUU MCHEZO HAUTAKI HASIRA

>> Awashihi viongozi wa CCM waliopo madarakani waache kuwanunia wenzao 

Na Gustaphu Haule, Pwani 

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka amesema mchezo wa uchaguzi hautaki hasira kwakuwa kila mtu anahaki ya kugombea nafasi ya chama pale uchaguzi unapotangazwa.

Nyamka amewaomba viongozi waliopo madarakani kuacha kuwanunia wenzao pale wanapoonyesha nia ya kugombea kwakuwa uongozi sio mali ya mtu bali ni mali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

       Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka akizungumza na wanachama wa CCM tawi la Gunewe alipokuwa katika ziara yake.

Nyamka ametoa kauli hiyo Septemba 01/2026 wakati akiwa katika ziara yake Kata ya Tangini katika tawi la Gunewe na tawi la Tangini ikiwa ni sehemu ya kuimarisha Chama na Jumuiya zake pamoja na kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM.

Amesema "Huu mchezo hautaki hasira" akimaanisha hakuna sababu ya kugombana katika suala la uchaguzi kwakuwa kila mwanachama mwenye sifa na uwezo anahaki ya kugombea nafasi yoyote ndani ya CCM ili mradi asivunje Katiba ,kanuni na utaratibu wa chama .

      Wanachama wa CCM pamoja na Wananchi wa Tawi la Gunewe wakimsikiliza mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka ( hayupo pichani) katika mkutano uliofanyika hivi Karibuni.

Amesema kuwa CCM inakwenda katika uchaguzi wa ndani mwaka 2027 lakini kabla ya kufikia katika uchaguzi huo Halmashauri Kuu ya CCM imetoa agizo la kuhakikisha nafasi zote zilizokuwa wazi zinazibwa katika uchaguzi mdogo unaotarajia kufanyika Septemba mwaka huu.

Amesema lengo la kufanya uchaguzi mdogo ni kuhakikisha wanapofika katika uchaguzi mwaka 2027 pasiwepo na viongozi wa kukaimu kwani kunapokuwa na viongozi wa kukaimu kunakuwa na changamoto ya Katibu wa CCM kushindwa kuitisha kikao cha Sekretarieti.

         Wanachama wa CCM na Wananchi wa tawi la Tangini wakiwa katika mkutano wa mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka.

Amesema kuwa wale ambao waliingia mwaka 2022 ukomo wao ni mwaka 2027 ikiwa ni kipindi cha miaka mitano na muda huo ukifika wanaCCM wanaweza kukuambia uendelee au uache.

Nyamka,ameongeza kuwa ukifika wakati wa uchaguzi hakuna mtu wa kusema nafasi yangu kwakuwa nafasi zote ni za CCM na kila mwanachama mwenye vigezo na sifa anaweza kugombea nafasi yoyote anayoitaka.

      Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akizungumza na wazee wa Kata ya Mbwawa alipokwenda Septemba 02/2026 kuzindua Jukwaa la.wazee hao.

Amesema viongozi waliopo madarakani waache nongwa kwani wakisikia mtu anatroti kutaka kugombea utasikia viongozi waliopo madarakani wanaanza kutoa milio kama ya Chura kwa kusema nafasi hizo ni zao jambo ambalo sio sahihi.

"Sisi tuliopo madarakani tusiwanunie wenzetu ambao wameanza kuonyesha nia ya kugombea na wala tusiseme huyu anataka nafasi yangu kwani ndani ya CCM hakuna nafasi ya mtu bali ni nafasi zote ni mali ya CCM na muda ukifika kila mwanaCCM anahaki ya kugombea," amesema  Nyamka .

Amesema kuwa kipindi hiki lazima wachochole chochole ili mradi wasivunje Katiba na kanuni kwasababu muda wa kampeni na muda wa uchaguzi bado kwakuwa hawajapewa ratiba ya uchaguzi japo inafahamika uchaguzi ni mwaka 2027.

Amesema  anawajibu na haki ya kuhamasisha wanachama mwenzake ambaye anaona endapo akishika nafasi ya uongozi anaweza kukisaidia chama lakini sio kuhamasisha kuweka mtu kwa ajili ya maslahi binafsi.

Diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao amesema kuwa Kata ya Tangini ipo salama na wanaendelea na kazi ya utekelezaji wa ilani.

         Diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao akizungumza na wanaCCM katika tawi la Tangini aliposhiriki katika ziara ya Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini.

Milao amesema anatambua Kata ya Tangini inakabiliwa na  changamoto ya miundombinu ya barabara na hususani kipindi cha mvua kushindwa kupitika lakini changamoto hizo zinafanyiwa kazi.

Amesema kwasasa wanasubiri fedha za bajeti ya mwaka 2026/2027 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na upo uwezekano wa fedha hizo kupatikana mapema Septemba na kwamba mara baada ya kupokea fedha hizo zitafanyakazi iliyokusudiwa ikiwemo kujenga vivuko mbalimbali.



Milao amesema mbali na hilo lakini pia Kata ya Tangini imefanikiwa kupata barabara mbili za lami zinazotekelezwa kupitia mradi wa Tactic na barabara hizo ni pamoja Loliondo na kuunganisha barabara ya Pangani pamoja na barabara ya kutoka Shule ya Sekondari Tangini kupitia Muheza.

Milao amewaomba Wananchi wa Kata ya Tangini kuwa wavumilivu katika kipindi hiki ambacho Serikali inaweka mipango madhubuti ya kuhakikisha miundombinu ya barabara ya Kata ya Tangini inaimarishwa ili ziweze kupitika wakati wote.

No comments