CHIFU WANZAGI, JAMES KISIJA LAWAMANI KWA USIRI WA MAPATO BIAGUNGA, MKATABA WA MWEKEZAJI WA KICHINA WAFICHWA
>> Utata wa Sh. bilioni 1 za mwekezaji wa Kichina
>> Vikao vyaendeshwa kwa siri
>> Wanahisa waliotengwa waiomba Serikali kuingilia kati
DIMA Online, Butiama
WANAHISA wa kampuni ya Biagunga Gold Mines Limited iliyopo Kijiji cha Magunga, Kata ya Mirwa wilaya ya Butiama, mkoani Mara, inayojihusisha na shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu, wameibua malalamiko .
Malalamiko hayo yanahusu namna kampuni hiyo inavyoendeshwa, wakidai kuwepo kwa usiri katika masuala ya makusanyo, mapato, matumizi ya fedha na taarifa zinazohusu mwekezaji wa Kichina.
Malalamiko hayo yanawahusisha viongozi wa kampuni, akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Japhet Wanzagi Nyerere, maarufu Chifu Wanzagi na Katibu wa kampuni James Kisija Mholya huku baadhi ya wanahisa wakidai kuwa wamekuwa wakitengwa katika taarifa na maamuzi muhimu yanayohusu kampuni.
Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na DIMA Online, kumekuwepo usiri katika utendaji wa shughuli unaofanywa na Chifu Wanzagi, Katibu James na baadhi ya wanahisa, jambo lililoibua migogoro ndani ya kampuni hiyo.
Miongoni mwa mambo yanayolalamikiwa ni usiri wa makusanyo, mapato na matumizi yatokanayo na wachimbaji wadogo waliowekeza kwenye leseni za Biagunga, madeni yasiyojulikana pamoja na usiri wa fedha zinazodaiwa kutolewa na wawekezaji kwa kampuni.
Utata mwingine unaohusishwa na kampuni hiyo ni kutokuwepo kwa gawio kwa baadhi ya wakurugenzi waanzilishi, vikao kufanyika bila kuwashirikisha baadhi ya wakurugenzi, pamoja na uthamini wa ardhi za wananchi kufanyika bila kuwashirikisha baadhi ya wakurugenzi waanzilishi.
Pia kuna madai kwamba baadhi ya wakurugenzi wananufaika na kampuni huku wengine wakiwekwa kando, na watu wengine wakidaiwa kuingizwa kwenye kampuni bila kuwashirikisha waanzilishi.
Kuanzishwa kampuni ya Biagunga
Kampuni ya Biagunga ni kampuni iliyosajiliwa kwa namba 125554, tarehe 15 Aprili 2016, ikiwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Japhet Wanzagi Nyerere, na Katibu James Kisija Mholya.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa, kampuni hiyo ina wanachama /wakurugenzi wapatao tisa ambao ni Japhet Wanzagi Nyerere, James Kisija Mholya, Sudi Marungu Simba, Elizabeth Peter Nyamboge, John Onaka Obare, Rajabu Ramadhani Bandiliki, Farid Snedy Nassor, Noah Thomas Shaga na Ahmed Mohamed Alawi.
Ahmed Mohamed Alawi anadaiwa kuwa raia wa kigeni ambaye katika kikao cha tarehe 18, Agosti 2026 kilichofanyika Mwitongo, aliondolewa uanachama bila kushirikishwa kwenye kikao hicho.
Inaelezwa kuwa aliondolewa kwa madai ya kutokuwa raia wa Tanzania, licha ya jina lake kuwepo kwenye hati ya uanzishaji wa kampuni.
Ofisi ya biashara ya kampuni hiyo inapatikana NHC House, Jengo la Madini, Samora Avenue, Ilala, Dar es Salaam, ikiwa chini ya usimamizi wa Mkurugenzi Mkuu mteule, Sudi Marungu Simba.
Utata wa hati ya Kampuni
Hati ya Kuanzisha Kampuni, maarufu Memorandum, ni hati inayoweka msingi wa kisheria wa kuanzishwa kwa kampuni, huku Katiba ya Kampuni ikiwa ni mwongozo au kanuni za ndani zinazoeleza namna kampuni itaendeshwa na kusimamiwa.
Hata hivyo, baadhi ya wakurugenzi waanzilishi wanalalamika kuwa hawakushirikishwa katika uandaaji wa hati ya kuanzisha kampuni, bali walikabidhiwa nyaraka tayari na kuambiwa wazisaini.
Wanadai pia kuwa baadhi yao hadi sasa hawajawahi kupewa wala kuiona Katiba ya kampuni ili kufahamu yaliyomo.
Kwa mujibu wa madai hayo, walioandaa na kufuatilia hati ya kampuni ni Chifu Wanzagi na James Kisija, ambao pamoja na wakurugenzi Faridy Snedy, Noah Thomas na Rajabu Ramadhani, wamekuwa wakifanya shughuli za kampuni bila kuwashirikisha wakurugenzi Elizabeth Peter, Sudi Marungu na John Onaka, ikiwemo vikao vya kampuni.
Mchakato wa hati ya kampuni ya mwaka 2016 unadaiwa kutowashirikisha wakurugenzi waanzilishi Elizabeth, John na Rajabu katika kuamua nani apewe hisa ngapi, zaidi ya kupewa hati na kusainishwa.
Hati hiyo inaeleza madhumuni ya kampuni kuwa ni pamoja na kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini ya aina mbalimbali, kutafuta, kufanya utafiti na kuendesha machimbo.
Pia inaonesha mtaji wa kampuni kuwa Tsh. bilioni 10, jumla ya hisa milioni moja na thamani ya hisa moja kuwa sh. 10,000.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa, hati hiyo inaonesha mtaji na thamani ya kila hisa, lakini haielezi sababu iliyofanya Chifu Wanzagi na James kuwa na hisa 150,000 kila mmoja, huku wakurugenzi wengine saba wakiwa na hisa 50,000 kila mmoja.
DIMA ONLINE yafika Butiama
DIMA Online imefika wilayani Butiama kuzungumza na wanachama wa kampuni ya Biagunga ili kufahamu mwenendo wa kampuni hiyo, yakiwemo madai ya kampuni kupokea Tsh. bilioni moja ambazo hazijabainishwa wazi ni fedha za nini, zinazodaiwa kutolewa na mwekezaji mpya wa Kichina ambaye jina la kampuni yake halijafahamika.
DIMA Online pia ilitaka kufahamu kwa nini wawekezaji wa kigeni wanaofika kuwekeza kwenye leseni za Biagunga hushindwa kuendelea na uzalishaji na kuondoka, wakiwemo wawekezaji kutoka India na Urusi, huku sasa kukiwa na mwekezaji wa Kichina.
Mwandishi pia alitaka kufahamu kuhusu usiri wa mikataba ya wawekezaji, ushirikishaji wa wakurugenzi katika zoezi la uthamini wa ardhi, taratibu zilizotumika kuanzisha kampuni na kuwashirikisha wanachama, muundo wa uongozi, haki za umiliki wa hisa, haki za wanachama, utawala wa kampuni, mamlaka ya wakurugenzi pamoja na usiri wa makusanyo, mapato na matumizi ya kampuni.
Baadhi ya wakurugenzi wanaodai kutengwa na kutoshirikishwa kwenye shughuli za kampuni wamefunguka mazito, huku wakurugenzi wengine akiwemo Chifu Wanzagi na James Kisija wakikwepa kuzungumza licha ya kutafutwa mara kadhaa, huku wengine simu zao zikiwa hazipatikani.
Kauli za Wakurugenzi waliotengwa
Elizabeth Peter, John Onaka na Sudi Marungu ni miongoni mwa wakurugenzi wanaodai kutengwa na kutoshirikishwa kwenye vikao vya mipango na maamuzi ya kampuni.
Elizabeth anasema kampuni ya Biagunga ni muunganiko wa wachimbaji wadogo kutoka Kijiji cha Biatika na Kijiji cha Magunga, na kwamba Elizabeth Peter, James Kisija, Rajabu Ramadhani na John Onaka waliungana kwa lengo la kuanzisha kampuni.
“James Kisija alinitafuta mimi, John Onaka, na Rajabu kwamba tuanzishe kampuni. Tulikubaliana tukamtafuta Chifu Wanzagi ili atusaidie kupata leseni na kusajili kampuni.”
“Sisi ndio tuliokuwa tukichanga fedha zetu kuhakikisha Chifu anatusaidia ili tupate leseni ya kampuni. Iwe pesa ya kula, nauli za ndege, chakula na malazi, kuwaleta wajiolojia; sisi waanzilishi ndio tulikuwa tukitoa pesa zetu na kumpatia Chifu Wanzagi kwa ajili ya kufuatilia leseni.”
“Chifu Wanzagi hakuchangia chochote. Alisema yeye anatusaidia tupate leseni, hivyo kila alichosema tulimsikiliza kwa sababu sisi hatujasoma. Kwa hiyo kila kitu alisimamia yeye, kazi yetu ilikuwa tu kutoa fedha kuhakikisha kampuni inasimama,” anasema Elizabeth.
Anaongeza " Hatukushirikishwa kwenye uandaaji wa hati ya kampuni wala mkataba wa kampuni. Nilichokiona ni nyaraka iliyokuwa imeandikwa kwa lugha ya Kiingereza, lugha nisiyoifahamu, ikiwa inaonesha Tsh. 150,000 kwa baadhi ya majina na Tsh. 50,000 kwa majina mengine likiwemo na langu.
“James aliniambia kuwa ule ni mgao wetu wa hisa, akanitaka nisaini. Akasema ana haraka anataka kusafiri, nikasaini. Lakini hakuna kikao chochote tulichowahi kukaa sisi wakurugenzi kujadili au kuandaa Memorandum. Hata hiyo Memorandum hatukutafsiriwa kwa Kiswahili tujue yaliyomo ndani,” anasema Elizabeth.
Elizabeth anasema amekuwa akijiuliza maswali kuhusu uendeshaji wa kampuni lakini kila anapotafuta majibu kwa wakurugenzi wenzake hawampi shirikiano.
“Huwa najiuliza maswali hiyo Memorandum nani aliyeiandaa na kuiandika? Maana sikushirikishwa zaidi ya kuambiwa nisaini, nikasaini. Sikuambiwa kila mmoja angepewa hisa ngapi zaidi ya kuona jina langu limeandikwa hisa 50. Hatukuwa tumeafikiana awali kuhusu mgawanyo gani wa hisa.”
“Hakuna ujumbe, maandishi, mashahidi au ushahidi mwingine unaoonesha makubaliano zaidi ya kuletewa nisaini Memorandum. Kuna majina yaliingizwa kwenye Memorandum ambayo hatukuwahi kukaa kuyajadili zaidi ya wale waanzilishi, mimi, John, Rajabu, James na Chifu Wanzagi tuliyemuingiza kwa lengo la kutusaidia ,” anasema Elizabeth.
Anaongeza " Baada ya kuona majina kwenye Memorandum, watu ambao tulikuwa hatuwafahamu tuliamua kukubali tu tuendelee nao kwa sababu hatukupewa hati yoyote iliyotumika kuwaingiza wanahisa wapya.
“Tuliambiwa eti walisaidia kufanikisha kupata leseni na uandaaji wa Memorandum, japo sisi waanzilishi hatukushirikishwa kwa sababu kila kitu kilikuwa kinafanyika Dar es Salaam na sio makao makuu ya kampuni yaliyoko Butiama.
“Sijawahi kupewa nakala ya Katiba ya kampuni na sijui kama ipo, wala sijawahi kupewa nyaraka zozote za usajili wa kampuni. Sisi tupo tupo tu, bora liende,” anasema Elizabeth.
Wanaoendesha Kampuni
John Onaka anasema " Hii kampuni inaendeshwa na watu wawili, Chifu Wanzagi na James Kisija. Wamejimilikisha kampuni, sisi wengine tumewekwa kando. Mimi kama mkurugenzi mwanzilishi, hatukuwahi kukaa kikao cha kuandaa Memorandum. Chifu Wanzagi na James ndio wanajua nani aliiandaa.
“Mimi nililetewa fomu na James akiniomba nisaini. Nilimuuliza, najaza nini? Kwa nini hamkuniita kwenye kikao na mimi nikae nisikilize na kutoa maoni yangu? Jibu alilonipa ni kwamba tumeenda BRELA kusajili jina la kampuni hivyo natakiwa nisaini Memorandum.
" Nikasaini bila kujua kilichoandikwa ndani kwa kuwa kiliandikwa kwa Kiingereza na mimi sijui Kiingereza,” anasema John.
Mkutano mkuu haufanyiki
Baadhi ya wakurugenzi wanasema kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu Katiba ya kampuni kumewafanya washindwe kufahamu wajibu wao na taratibu za vikao.
Wanadai kuwa tangu kampuni hiyo isajiliwe mwaka 2016 hawajawahi kufanya Mkutano mkuu wa mwaka.
John Onaka anasema " Binafsi tangu kampuni isajiliwe sijawahi kushirikishwa kwenye vikao na hatujawahi kufanya Mkutano mkuu wa mwaka kwa miaka 10 mfululizo tangu kampuni ipate usajili mwaka 2016. Kama kuna nyaraka inaonesha kuwa tulishakaa mkutano wa mwaka au vikao vingine basi TAKUKURU ichunguze saini zetu za mahudhurio; huenda ziligushiwa,” anasema John.
Kwa mujibu wa sheria ya makampuni Na. 12 ya mwaka 2002 , Sura ya 212 , Toleo la marekebisho la 2023 , kifungu cha 133, kampuni ina masharti kuhusu kufanyika kwa mkutano mkuu wa Mwaka. Kifungu hicho pia kinahusisha mambo yanayopaswa kuwasilishwa kwa wanachama katika mkutano huo, yakiwemo hesabu za mwaka na taarifa ya wakurugenzi, kwa mujibu wa masharti ya sheria.
Siri Makusanyo, Mapato, Matumizi
Kampuni ya Biagunga ina vyanzo vya mapato vinavyohusisha wachimbaji wadogo kwenye leseni za Biagunga pamoja na wawekezaji wanaowekeza kwenye leseni hizo.
Hata hivyo, baadhi ya wakurugenzi wanadai kuwa hawajasomewa wala kupewa taarifa za mapato, matumizi na makusanyo yanayopatikana kutoka kwa wachimbaji na wawekezaji tangu kuanzishwa kwa shughuli za kampuni.
Elizabeth anasema " Kampuni ya Biagunga ina uzalishaji ambao ni wachimbaji wadogo wanachimba pale. Hatujawahi kuambiwa mapato na matumizi wala kinachofanywa.
“Tuwekwe wazi kilichokuwa kinavunwa pale, hasara zilizopatikana ziwekwe wazi. Katibu aliingiza watu kwenye kampuni, Ghati John alishatangulia mbele za haki alitoa milioni 15 na Agnes China akatoa milioni 15. Waliambiwa watakuwa wanapata pesa baada ya uzalishaji. Fedha hizo zilifanya nini? Fedha za wawekezaji Mhindi, Mrusi na Mchina zimefanya nini? Maana wamewekeza kwenye leseni za kampuni,” anasema.
Kificho cha mikataba ya Wawekezaji
Kampuni ya Biagunga imekuwa ikiwaleta wawekezaji kufanya shughuli za uchimbaji kwenye leseni za kampuni hiyo, lakini baadhi ya wakurugenzi wanadai kuwa kumekuwepo kificho kuhusu mikataba na majina ya kampuni za wawekezaji.
Tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo mwaka 2016, wawekezaji wa kigeni kutoka India, Urusi na sasa China wamedaiwa kuwekeza kwenye leseni za Biagunga.
Baadhi ya wakurugenzi wanasema hawajui wawekezaji hao wameingia kwa njia gani, hawajui mikataba ya uuzaji au uhamishaji wa hisa, mgawanyo wa hisa kabla na baada ya mwekezaji, majina yao wala majina ya kampuni zao, zaidi ya kuwaona wakifanya shughuli za uzalishaji.
Miongoni mwa maswali yanayoibuliwa ni: Mwekezaji anaingia kwa njia gani? Ananunua hisa za wanahisa waliopo au kampuni inatoa hisa mpya kwake? Anapata hisa ngapi kati ya hisa zote za kampuni? Bei ya kila hisa ni kiasi gani? Mwekezaji analipa kiasi gani? Fedha inaingia kwenye kampuni au inaenda kwa mwanahisa anayemuuzia hisa?
John Onaka anauliza " Sisi wakurugenzi tuliotengwa hatufahamu huyo mwekezaji anafanya uchimbaji kwenye hisa za wanachama au kuna hisa mpya za kampuni? Hatujui kama kuna mabadiliko ya mamlaka ya kampuni na mwekezaji.
“Hatujapewa Mkataba wa uwekezaji ili tuuone. Je, mwekezaji ni miongoni mwa wakurugenzi? Amepewa nafasi kwenye Bodi? Je, ana haki maalumu za kupiga kura na kuwa na uwezo wa kuzuia maamuzi fulani au mamlaka ya kusimamia shughuli za mgodi?” anauliza John.
John anaongeza " Kuna siku nilienda ofisini kwenye kampuni kutaka kujua kuhusu huyo mwekezaji, niliwakuta watu ambao ni Wachina nilipotaka ufafanuzi sikupewa majibu .
“Hatujui mwekezaji huyo anapewa hisa kutoka kwa nani, anapewa asilimia ngapi, analipa kiasi gani, fedha inaenda kwa nani, na baada ya muamala nani atakuwa na udhibiti wa kampuni?” anasema.
" Huwa nasikia kwamba kuna sheria ya makampuni inaweka masharti kuhusu taarifa za mgao wa hisa na kurejesha taarifa kwa Msajili.
“Katika utoaji wa hisa, wanasema kuna sheria ya Makampuni imeweka masharti ya taarifa na kurejesha taarifa kwa Msajili kuhusu mgao wa hisa, ikiwemo idadi ya hisa, majina ya wanaopewa na kiasi kilicholipwa au kinachodaiwa,” anasema John.
John pia anadai " Chifu Wanzagi analeta wawekezaji bila kutushirikisha, anafanya mambo mwenyewe na Katibu. Yeye ndiye ananufaika maana alishawahi kumleta mwekezaji kampuni ya Kihindi ilileta vitendea kazi, Bajaji 4 n.k. ikaanza kufanya uchimbaji.
“Kampuni hiyo ikamnunulia Chifu trekta, wakamjengea na nyumba na kumpatia fedha. Miaka imeenda tukashtukia kwenye leseni zile 10, kati ya hizo leseni mbili kapewa mwanamke mmoja huko Dar ambaye inasemekana ndiye aliyewaleta wawekezaji Wahindi " anasema John.
Elizabeth anasema " Kampuni inatembea na watu wawili ambao ni James na Chifu Wanzagi. Sasa hivi amekuja mwekezaji Mchina, hatujui kaingiaje, kaanzaje? Ilibidi nimtafute Katibu nikamwambia naenda kuwashtaki kwa RMO ili nipate haki zangu. Wakasema basi tutakata kikao cha dharura.
“Tarehe 3/6/2026 tukakaa kikao pale Jirafu, mimi, Faridy, Noah, Rajabu. Wakaniambia hakuna atakayepoteza haki zake. Nikawauliza nitapataje haki yangu wakati Mchina ameingia, sijui mkataba wowote uliosainiwa, sijashirikishwa chochote ?
“Nikawauliza, mnaponiambia siwezi kupoteza chochote, nitajuaje mkataba mlioingia na Mchina? Basi mnipe mkataba niuone. James akasema mkataba nitakutumia kwa njia ya simu.
“Mara tunaambiwa eti tulikuwa mbali, yaani wanakuwa na maneno ya kutishia wakurugenzi wengine ili tukose cha kuongea. Nimwambia James kama mnasema tuko pamoja basi tushirikishwe tujue kinachoendelea planti maana panafanyika uzalishaji pamoja na shughuli zingine za kampuni" anasema Elizabeth.
Anaongeza " Ukipiga simu hakuna anayepokea, wana mizunguko. Ukienda saiti unaambiwa mara wameenda kwenye kesi Dodoma, mara Dar. Hakuna siku utaambiwa kinachoendelea ,unakuwa unapishana tu na watu . Imefika hatua hakuna hata anayetaka salamu." Anasema.
Elizabeth anasema baada ya kukosa ushirikiano kwenye kampuni hiyo yeye, John na Sudi waliamua kupeleka malalamiko yao Ofisi ya Madini Mkoa wa Mara.
“Siku ya kwanza tumekwenda hatukumkuta tukarudi. Kuna siku nimeenda ofisini niongee na hao wanaotutenga, waliponiona wakawasha magari wakaondoka zao. Sudi alikuja kutoka Dar es Salaam tukampigia simu James akasema anapeleka watu wa ardhi Musoma kwamba tusubiri kesho wamalize tathmini ndio twende tukae kikao kwa Chifu." anasema.
Kifungu cha 182 cha Sheria ya Makampuni kinaweka wajibu kwa wakurugenzi kutenda kwa uaminifu na kwa nia njema, kwa maslahi bora ya kampuni. Kifungu cha 185 kinahusu wajibu wa mkurugenzi wa kuwa na uangalifu, ujuzi na bidii inayostahili katika utekelezaji wa majukumu yake.
Aidha, kifungu cha 124 kinahusu marekebisho ya rejesta ya wanachama na wamiliki wanufaika, na kifungu kidogo cha 124(3) kinahusu uwezo wa mahakama kuamua masuala yanayohusiana na haki au umiliki katika mazingira yaliyowekwa na Sheria.
Kwa hiyo, endapo kutathibitika kuwa taarifa za umiliki au wanachama
hazikuakisi hali halisi ya kampuni, suala hilo linaweza kuhitaji kuchunguzwa kwa kuzingatia masharti hayo ya Sheria.
Watinga ofisi ya RMO
Kutoelewana kwa wakurugenzi hao kuliwalazimu baadhi yao kufunga safari hadi Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mara kueleza kero zao.
" Mimi na wenzangu tuliandika barua kwenda kwa RMO. Kisha mimi na John tulienda Ofisi ya RMO lakini hatukumkuta. Zilipopita siku chache RMO alinipigia simu na kututaka twende ofisini. Mimi, John pamoja na wale wakurugenzi wanaotutenga tulihudhuria kikao." anasema Elizabeth.
“Cha ajabu hatukuweza kupewa nafasi ya kujieleza. Ukijaribu kuinua mkono ujieleze, mkurugenzi mwenzako anakwambia kaa, mara unaambiwa wewe ni mjuaji una maneno mengi. Kutokana na picha ambayo RMO aliiona alitushauri twende tukafanye kikao cha maridhiano." anasema.
Wapinga Muhtasari
Wakurugenzi hao wanasema baada ya ushauri wa afisa madini mkazi mkoa wa Mara, Daniel Mapunda wa kuwataka wakurugenzi wa kampuni kukutana na kufanya kikao cha maridhiano, wanahisa hao walikutana na kufanya kikao Mwitongo kilicholenga kuondoa tofauti zao.
Hata hivyo, wakurugenzi hao wanadai kushangazwa na baadhi ya mambo yaliyowekwa kwenye muhtasari wa kikao, wakisema hayakuzungumzwa. Wanasema waliomba yafanyiwe marekebisho lakini haikuwezekana, hivyo muhtasari huo ulipelekwa Ofisi ya Madini Mkoa wa Mara hawakubaliani nao .
Elizabeth anasema " Muhtasari hauna maelezo sahihi ya dhumuni la kikao. Muhtasari haujaweka rekodi ya nini tulitaka yabadilishwe baada ya kukandamizwa kwetu kwa muda mrefu. Hatukuongelea suala la madeni.
“Muhtasari hauelezi tuliyozungumza kuhusu matatizo ya kutengwa kwetu kwa makusudi. Hivyo mimi, John, Sudi tunaukataa huo muhtasari kwa sababu yaliyomo mengi sio tuliyoyazungumzia.”
Elizabeth anasema wanapomuuliza Mwenyekiti Chifu Wanzagi na Katibu James Kisija kwanini muhtasari haujaeleza yale tuliyozungumza, wakwepa na kutowapa majibu.
Wagoma kulipa madeni
Elizabeth na John wanasema wamegoma kulipa madeni ambayo kampuni inadaiwa kwa madai kwamba Chifu Wanzagi, ambaye ni Mwenyekiti, na Katibu James hawajawahi kuwashirikisha katika shughuli za kampuni wala kuwaeleza mapato na matumizi ya kampuni hiyo.
Elizabeth anasema " Tumeshangaa kuona kwenye muhtasari ulioandikwa na Katibu kwamba tuliazimia kwenye kikao cha tarehe 18/8/2016 kwamba sisi tilipe madeni ambayo kampuni inadaiwa, wakati kwenye kikao hatukuwa na hiyo mada.
“Tunaambiwa kampuni ina madeni, hivyo kikao kiliamua kuwa wakurugenzi wenye madeni ambayo hawakutoa pesa kwa ajili ya kulipa leseni ya kila mwaka (pango la ardhi) la eneo la mgodi, magawio yao yatakatwa kulipa madeni ya kampuni. Hatujawahi kushirikishwa kinachopatikana kwenye uzalishaji.”anasema Elizabeth.
Anaongeza " Wakati tunasajili kampuni leseni ya kwanza mimi na Rajabu ndio tulilipia na sijawahi kushirikishwa kwenye uzalishaji wa kampuni. Wao wamechangia kiasi gani? Chifu amewahi kuchangia nini? Wawekezaji wanaingia wanatoa fedha, je fedha hizo zimefanya kazi gani? Leo naambiwa gawio litakapoanza nitakata fedha kwa miaka kumi tangu kampuni ilipoanzia !
“Hatujawahi kunufaika na chochote, nao walete gharama walizotumia kwenye hii kampuni. Ni heri niwe wazi, kama sheria itanitoa Biagunga initoe, maisha yataendelea kwenye shughuli zingine. Kwa sababu siwezi kukubali kuendelea kukandamizwa kwa kitu nilichokishughulikia kwa gharama zangu.
“Kuna wakurugenzi kwenye hii kampuni hawajawahi kuchangia chochote kwenye uanzishaji wa kampuni. Leseni yetu ilikuwa na uzalishaji, wachimbaji wadogo wanachimba, hatujawahi kuambiwa mapato. Kampuni ina planti inazalisha, hatujawahi kuambiwa mapato.
" Wawekezaji wa kigeni wameshawekeza pale, je pesa waliyopewa wamefanya nini? Kuna watu wakiwemo wengine wawili kila mmoja alichangia Tsh. milioni 15, walizifanyia nini?
“Je, hayo mapato yalishindwa kulipa leseni? Je, kampuni imeendesha mradi gani ukapata hasara? Hizo gharama za leseni ni Tsh. ngapi? Je, waliwahi kutueleza hayo madeni hapo awali tukashindwa kuchangia? Mimi kama mkurugenzi ukiniuliza sijui, kwa sababu ukifuatilia hupewi jibu zaidi ya chenga chenga,” anasema Elizabeth.
John Onaka anaongeza " Nashangaa tunaambiwa tulipe madeni ya leseni tangu kampuni iliposajiliwa mwaka 2016. Sisi wakurugenzi waanzilishi ndio tuliogharamika mpaka kampuni kusajiliwa, ni kwa fedha zetu.
“Huyo Chifu anayesema nilipe madeni ya leseni yeye alishachangia nini? Kwa sababu kila kitu sisi wakurugenzi wanzilishi ndio tulikuwa tunatoa fedha. Kila tulipomuhitaji kwa ajili ya kutusaidia kushughulikia leseni ni fedha zetu zilizotumika.
“Nilitumia fedha zangu ambazo nikisema nipige hesabu ni nyingi sana. Elizabeth, James na Rajabu nao walichangia fedha zao. Chifu hakuchangia pesa yoyote zaidi tu ya kutusaidia kwenda kutusajilia kampuni na kupata leseni, na pesa tulitoa sisi wanachama waanzilishi.”anasema John.
John anaongeza " Mimi nilikuwa natoa pesa zangu, Chifu anasafiri kwa ndege mara tatu kwenda na kurudi Dar es Salaam maana ndio usafiri aliouhitaji.
Alipofika Musoma tulikuwa tunamkodishia gari anakuja hadi Buhemba na kurudi Musoma, anapanda ndege anaenda, bado unalipia malazi, chakula na pesa zingine.
“Nilitumia pesa zangu nyingi kusafirisha baadhi ya wakurugenzi na mjiolojia tukaenda Afrika Kusini na Zimbabwe kwa ajili ya kujifunza masuala ya uchimbaji na kununua kifaa. Fedha za malazi, chakula ni mimi niligharamia, halafu wanasema nitakatwa pesa kulipia madeni ! John anashangaa .
“Tangu tusajili kampuni hatujawahi kupewa gawio lolote na mgodi unazalisha. Wananufaika tu wengine ambao hata hawakutumia fedha zao wakati wa mchakato wa uanzishaji wa kampuni. Tulioihangaikia kampuni mpaka ikapata usajili kwa gharama za fedha zetu ndio tumetengwa na wenzetu,” anasema John.
Anaongeza " Mgodi unaomilikiwa na kampuni yetu una maduara zaidi ya 60. Kila duara linatozwa fedha na Serikali na kampuni, mbona kampuni haijawahi kutupatia taarifa ya mapato na matumizi?
Utata wa Tsh. Bilioni moja
John anasema kampuni inapata fedha kupitia wawekezaji lakini kumekuwa na kificho cha fedha zinazotolewa na wawekezaji na matumizi yake.
Anadai kuwa mwekezaji wa Kichina aliyekuja kuwekeza tayari ameipatia kampuni Tsh. bilioni moja.
“Awamu ya kwanza wamepokea milioni 200 na awamu ya pili wamepokea milioni 800. Tunasikia tu taarifa za chini chini lakini hatujawahi kusikia kutoka kwao, hatujui pesa hizo ni za nini.
“Anayenufaika na kampuni ni Chifu Wanzagi na James maana wao ndio wanawaleta wawekezaji, wanafunga nao mikataba, hatujui wanakubaliana nini na faida inayopatikana. Hatupati mgao kama wanahisa, wananufaika wenyewe,” anasema Onaka.
Nani anayefanya uthamini?
John Onaka anasema ana mashaka kwamba huenda tetesi anazozisikia kuhusu mwekezaji wa Kichina kutoa Tsh. bilioni moja kwa ajili ya kuwekeza kwenye leseni za Biagunga zikawa na uhusiano na zoezi la uthamini wa ardhi za wananchi katika Kitongoji cha Kurusiru, Kijiji cha Tarani, na Kitongoji cha Kukitaramanka, Kijiji cha Magunga.
“Hivi karibuni umefanyika uthamini kwenye ardhi za wananchi kwenye vitongoji viwili. Na wanaofanya uthamini ni Wachina kupitia Kampuni ya Biagunga ili kupisha shughuli za uchimbaji.
“Kampuni imefanya uthamini kwenye mashamba ya watu kwamba mwekezaji wa Kichina anakuja kuwekeza. Najiuliza maswali, je, ni nani aliyeomba uthamini ufanyike? Nani aliyeidhinisha? Kwa mamlaka ya nani? Mwekezaji anaitwa nani? Kampuni itapata nini? Je, wanahisa tutapata nini ?
“Je, Katibu alipata wapi mamlaka ya kwenda kitongojini kufanya mchakato wa uthamini kwa niaba ya kampuni? Je, kuna muhtasari wa kikao cha Bodi kilichokaa na kuazimia? Je, alipata barua ya kampuni iliyompa mamlaka?” John anauliza .
Wachimbaji wadogo wahaha
Wachimbaji wadogo kwenye leseni za Biagunga wamebaki njia panda kuhusu watakakoelekea kufanya shughuli za uchimbaji baada ya kampuni hiyo kuwapa taarifa kwamba ifikapo Septemba 14, 2026 wawe wameondoka.
Wachimbaji hao wamezungumza kwa sharti la kutotajwa majina.
Mchimbaji mmoja anasema " Kampuni imetuambia ikifika tarehe 14, mwezi huu wa tisa, tuwe tumeondoka kwenye haya maduara. Tunaondoshwa kienyeji wakati tunalipa kodi serikalini, tunalipa mapato kwenye kampuni lakini wachimbaji hatupewi risiti.
“Halmashauri inachukua Tsh. 300 kwa kila mfuko. Ukiwa na viroba 100 unagawa kwa asilimia 0.7 ambayo ni mrabaha wa Serikali humo humo, bado asilimia 30 inayokwenda kwenye kampuni, bado humo humo inahitajika fedha ya uendeshaji na familia nayo inakutegemea, halafu wanatuondoa kienyeji " anasema.
Anaongeza " Ili uingie kuchimba dhahabu kwenye hizi leseni za Biagunga kiingilio ni kuanzia Tsh. 500,000 na kuendelea kutegemea na upana wa eneo unalotaka kufanyia kazi. Kuna maduara zaidi ya 60 yanazalisha na mengine 40 hayajafikia hatua ya uzalishaji.
Mfanyakazi mmoja wa duara anasema " Tunasikia kuna Mchina anakuja kuwekeza ndio maana wanatutimua. Huwa wanasema Wachina wanafanyisha sana watu kazi na malipo ni kidogo, bora angekuja Mzungu kidogo ana huruma.
“ Wengine tunadai mishahara, sasa wakitufukuza tutapataje malipo yetu? Hii kazi ndio inaendesha maisha yetu na familia. Tutaenda wapi? Tukawe wezi maana tulikuwa tunajipatia kipato hapa ,” anasema.
Mfanyabiashara wa vinywaji anasema " Huu mgodi unatusaidia sisi akina mama wafanyabiashara ndogondogo, tunalisha watoto. Ukija hapa mgodini utauza ndizi, maji, chakula na huduma zingine.”
“Sasa huyo Mchina akija atanunua busara ( Togwa) anywe kweli au atanunua matunda tunayotembeza?
" Kwakweli wangeacha wachimbaji wadogo wafanye kazi, hawa wanasaidia, kunakuwepo na mzunguko wa pesa maana tunaishi nao hapa Buhemba, lakini huyo Mchina atavuna pesa atapeleka kwao,” anasema.
Wasemavyo Wenyeviti wa Vitongoji
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kukitaramanka katika Kijiji cha Magunga, Kata ya Mirwa, Nyamburi Kikare, pamoja na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kirusiri, Kijiji cha Tarani, Lameck Masaka, wanakiri Kampuni ya Biagunga kufika kwenye vitongoji hivyo na kufanya uthamini kwenye mashamba ya wananchi kwa lengo la kupisha shughuli za uchimbaji.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kirusiri, Lameck Masaka, anasema waliofika kwa nia ya kutaka maeneo ni Kampuni ya Biagunga na kikundi cha Mwanga wa Samia.
“Nakumbuka ilikuwa mwezi wa nane mwaka huu walikuja watu wakajitambulisha wanatoka kikundi cha Biagunga wakiwa na mwanasheria kutoka Halmashauri ya Wilaya Butiama aliyekuja kwa ajili ya kutoa elimu.
“Walifuata utaratibu, wakaita wananchi wakawaeleza sera zao. Mwisho wa siku wakawaambia wanataka wawaoneshe mipaka yao ili wajue wenye mashamba ni akina nani. Tukatembea nao kwenye maeneo na kila mtu akapimiwa shamba lake.
“Hao Biagunga ndio waliokuwa wanapima, walikuwa na vipimo vyao. Walipomaliza kupima wakawa wanawapa karatasi ya maelezo kuwa shamba lako ni namba fulani, waliandika walivyovikuta shambani.”anasema Mwenyekiti.
“Baada ya kumaliza zoezi la uthamini walisema watakuja kuwaita. Wananchi wakauliza, mnaweza kurudi kwa muda usio mwafaka, je, tutakaa hadi lini maana mmetuzuia tusilime? Afisa ardhi yeye alikuwa ni mwelimishaji juu ya utaratibu, hakuingilia chochote, kazi yote ilifanywa na hao wa Biagunga.
Mwenyekiti huyo anaongeza " Kundi la pili ni kikundi cha Mwanga wa Samia. Wao sera yao walisema wako tayari kufanya ubia na wananchi. Kama watakubali watakuwa wanachimba kwa pamoja, wanagawana kinachopatikana.
“Sera ya pili ni kumlipa fedha mwananchi kulingana na eneo lake lilivyo. Wananchi wakauliza, kama tukiingia sehemu kwenye shamba langu halafu tuchimbe na isipatikane dhahabu, je, nitalipwa nini?
“Wakasema kama dhahabu itakosekana hautalipwa chochote maana wote tumekosa. Hao Mwanga wa Samia walikuwa ni wanawake sita, walikuja bila afisa ardhi kisha wakaondoka. Siku ya pili wakarudi tena, wananchi wakagoma wakasema hawawaamini maana hata leseni yao hawajaiona.
" Wananchi wakasema mfumo wao hawauelewi, wananchi wakasambaratika wakaondoka. Kikao chao cha kwanza kilifanyika ofisini na kikao cha pili kikafanyika mashambani,” anasema Lameck.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kukitaramanka, Nyambura Kikare, anasema " Walikuja watu wa Biagunga, James akaniambia Mwenyekiti niitie wenye mashamba. Nikawaambia nipelekeni kwanza kwenye mashamba niyaone ili iwe rahisi kutambua eneo hili ni la fulani ili niweze kuwaita kwa urahisi.
“Wakanichukua tukaenda hadi kwenye maeneo, wakanionesha eneo wanalolihitaji. Kwa vile wananchi ni wakazi wangu nikaanza kupita kaya hadi kaya kuwajulisha siku fulani kuna kikao na watoa semina ambao wanataka mashamba yenu.”
Mwenyekiti huyo anasema wenye mashamba walijitokeza lakini kulitokea mvutano " Wananchi walisema kabla hawajapimiwa maeneo yao waelezwe wanalipwa Tsh. ngapi kwa ekari. Wale watu walikataa wakasema hawawezi kuwaambia kwa sababu hawajapima.
“Wananchi wakagoma wakasema hawawezi kwenda kusimama kwenye mashamba hawajajua wanalipwa Sh. ngapi. Wakasema msitupige picha na hatutasaini kokote na majina hatutajiorodhesha.” anasema.
Mwenyekiti anaongeza " Mtoa semina kutoka Idara ya Ardhi Halmashauri akawaelimisha. Akasema basi twendeni kwenye mipaka ili wakipita basi wajue nani wamo. Wakaanza kupima kila mwananchi akiwa amesimama kwenye eneo lake.
“Wakapima kila kilichopo kinaandikwa na jina la mwenye mali. Wakasema baada ya wiki mbili watarudi na kuwaambia kila mwananchi anatakiwa kulipa kiasi gani, yakaishia hapo.
“Tayari zimepita wiki mbili, hii ni wiki ya tatu tunaelekea kumaliza, hawajarudi tunaendelea kuwasubiri waje. Walisema Biagunga ndio imechukua leseni.
“Waliokuja walikuwa ni Watanzania, sikumuona Mchina, wakiongozwa na James. Chifu Wanzagi hakuwepo. Siku ya kwanza James alikuja akanichukua mimi tukazunguka naye kwenye mashamba na huyo James yuko ndani ya Wachina, ila mimi Wachina sikuwaona kwa macho,” anasema Mwenyekiti.
Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa, zaidi ya ekari 200 zinatarajiwa kuchukuliwa kwa ajili ya shughuli za uchimbaji.
Wakwepa kuzungumza
Kutokana na malalamiko ya baadhi ya wakurugenzi kudai kutengwa na wenzao, mwandishi wa DIMA Online alifika hadi ofisi ya Kampuni ya Biagunga iliyopo Kijiji cha Tarani ili kupata majibu ya malalamiko na maswali yaliyoulizwa na wakurugenzi waliotengwa.
Mwandishi akafika getini na kugonga, muda mfupi alifika mlinzi, akajitambulisha na kueleza kuwa alihitaji kuzungumza na Meneja wa Kampuni ya Biagunga, Mchunguzi Kitunzi.
Mlinzi anampigia simu Meneja na kumweleza kuwa kuna Mwandishi wa habari anahitaji kuzungumza nae. Meneja alimwambia mlinzi kwamba ametoka kidogo na mwandishi asubiri.
Mlinzi anaongozana na mwandishi hadi ofisini, anampa kiti aketi na kumuomba asubiri Meneja. Mwandishi anasubiri kwa zaidi ya saa mbili ndipo Meneja anapifika.
Mwandishi anajitambulisha na kueleza sababu ya ujio wake, miongoni mwa maswali aliyohitaji ufafanuzi yalikuwa taratibu zilizotumika kumuingiza mwekezaji wa Kichina kwenye leseni za Biagunga bila kushirikisha baadhi ya wanahisa ambao pia ni wakurugenzi
Sababu za baadhi ya wakurugenzi kutengwa na kutopewa taarifa za shughuli za kampuni, yakiwemo mapato na matumizi, pamoja na taarifa kuhusu mwekezaji wa kigeni.
Maswali mengine yalihusu kiasi cha madeni wanayodaiwa baadhi ya wakurugenzi na chanzo chake, kwa nini baadhi ya wakurugenzi hawakushirikishwa kwenye mchakato wa uthamini, sababu za wanahisa kutopatiwa Katiba ya kampuni na kutoshirikishwa kwenye mikataba ya kampuni na wawekezaji.
Mwandishi pia alitaka ufafanuzi kuhusu Tsh. bilioni moja zinazodaiwa kutolewa na mwekezaji wa Kichina, ambazo baadhi ya wakurugenzi wanasema hawajui ni fedha za nini na kwa ajili ya kazi gani.
Hata hivyo, Meneja Mchunguzi anasema ana mwaka mmoja tangu aajiriwe hivyo mambo ya nyuma hayafahamu.
“Nimeajiriwa nina mwaka mmoja, taarifa hizo ni za nyuma. Sikuwepo, nimekuja 2025 mwishoni. Mimi ni mwajiriwa, ili nijibu mpaka nimuulize bosi wangu hili linaendaje. Chifu Wanzagi hayupo, yuko safarini, labda nimpigie mmoja wapo tuweze kupata jibu sahihi.” anasema.
Meneja huyo akampigia simu Katibu wa kampuni ya Biagunga, James Kisija. James akapokea simu na kuambiwa kuhusu ujio wa mwandishi, kisha akapewa simu kuzungumza na mwandishi.
Baada ya kusalimiana, mwandishi akaeleza sababu ya kufika. James anamwambia mwandishi amsubiri kwa kuwa alikuwa karibu na ndani ya muda wa takribani nusu saa angefika ili azungumze naye, kisha akakata simu.
Mwandishi anamsubiri kwa zaidi ya saa moja bila mafanikio na kumuomba Meneja ampigie tena. Meneja anampigia na James anasema yuko jirani.
Mwandishi anasubiri tena kwa takribani dakika 45 bila mafanikio, anaamua kumuaga Meneja na kuondoka.
Baada ya siku moja, mwandishi anamtafuta tena kwa simu Katibu ili kupata ufafanuzi, lakini kila anapojaribu kupiga simu yake mara kadhaa namba hiyo haikupatikana hewani.
Mwandishi pia akampigia simu Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni, Japhet Wanzagi Nyerere, ili kupata ufafanuzi kuhusu malalamiko hayo, lakini simu yake haikupokelewa.
Baada ya kutuma ujumbe wa maneno na kujitambulisha, dakika 46 baadaye Chifu Wanzagi akapiga simu.
Mwandishi anajitambulisha, lakini Chifu Wanzagi akasema alikuwa anaelekea kwenye msiba Arusha.
“Tumeshakaa kikao, ukiniambia mambo mengine mimi sielewi. Hapa nilipo nataka kuingia kwenye gari naondoka kwenda Arusha. Nimefiwa na mama mkwe wangu, nakwenda kuzika. Nataka nikupe namba za watu ambao tutaongea nao, mimi nina msiba,” anasema Chifu Wanzagi.
Chifu Wanzagi akamtumia mwandishi namba za simu za Katibu wa kampuni ili azungumze naye, ambazo ni zile zile alizokuwa amezipigia awali, lakini simu yake haikupatikana hadi habari hii inaripotiwa DIMA Online.
Mwandishi akampigia simu Sudi Marungu ambaye yeye, John na Elizabeth wanadai kutengwa na kutoshirikishwa kwenye shughuli za kampuni, lakini simu yake haikupatikana licha ya kupigwa mara kadhaa.
Mwandishi pia akawatafuta Faridy Snedy, Noah Thomas na Rajabu Ramadhani ambao wanatajwa kuwa karibu na Chifu Wanzagi na James Kisija ili kupata ufafanuzi kuhusu kwa nini wanawatenga wakurugenzi wenzao na malalamiko yanayotolewa dhidi ya kampuni.
Faridy: Unasemaje?
Mwandishi: Nina jambo naomba kupata ufafanuzi.
Faridy: Jambo gani ?
Mwandishi: Kuhusu Kampuni ya Biagunga.
Faridy: Mimi sihusiki mama.
Kisha anakata simu.
Noah: Unahitaji kuzungumzia nini?
Mwandishi: Naomba ufafanuzi juu ya kile unachokifahamu kuhusu kampuni ya Biagunga juu ya baadhi ya Wakurugenzi kutengwa na kutoshirikishwa kwenye shughuli za kampuni .
Noah ananikatisha mazungumzo na kusema:
“Mwandishi, siko tayari kuliongelea hilo. Suala hilo liko chini ya Bodi. Mimi siwezi kuongea mambo ya majungu, yanisaidie nini? Siwezi kufanya hiyo biashara,” anasema na kukata simu.
Mwandishi akamtafuta Rajabu Ramadhani, ambaye alipokea simu na baada ya kujitambulisha, alisema yuko kikaoni na angepiga baadaye.
Hata hivyo, hakupiga tena simu na mwandishi alimpigia tena bila mafanikio.
Kauli ya Afisa madini
Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mara, Daniel Mapunda, amewaomba wanachama wa Biagunga ambao wanaona makubaliano yamekiukwa kufika Ofisi ya Madini Mkoa wa Mara kueleza changamoto zao, huku akiahidi kufuatilia na kushughulikia changamoto zinazojitokeza katika kampuni hiyo.
“Nilitumia muda mwingi kwenye ofisi yangu, masaa mengi, kutoa mwongozo. Kama kuna mambo ambayo hapo kwenye makubaliano waliyoyafanya, walalamikaji warudi Ofisi za Madini waeleze,” anasema Daniel.
Ombi kwa Serikali
Wakurugenzi wa kampuni wanaodai kutengwa, John Onaka na Elizabeth Peter, wanaiomba Serikali kuingilia kati ili haki itendeke na waweze kupata nakala ya azimio la Bodi ya Wakurugenzi lililoidhinisha mazungumzo au uwekezaji huo.
Wanasema Serikali iwasaidie kupata jina kamili la mwekezaji na jina la kampuni yake, pamoja na nakala ya mkataba uliosainiwa, ili kubaini namna uwekezaji huo ulivyoingia kwenye kampuni.
Pia wanataka kuwepo uwazi kuhusu gawio la hisa au asilimia ya kampuni na ya mwekezaji, pamoja na maelezo ya nani aliyeidhinisha uthamini wa ardhi unaofanywa.
Wanasema wanahitaji pia taarifa za makusanyo, mapato na matumizi ya kampuni tangu kampuni hiyo ianze uzalishaji mwaka 2016 kupitia wachimbaji wadogo na wawekezaji kutoka India, Urusi na China waliowekeza kwenye leseni za Biagunga.
Wanataka kupata daftari la wanachama na taarifa za hisa za kila mmoja, taarifa za vikao vya Bodi pamoja na taarifa za mikutano mikuu ya mwaka iliyojadili masuala mbalimbali ya kampuni na wanachama.
Pia wanataka kufahamu jina na namba ya akaunti ya kampuni ya Biagunga, kiasi cha fedha kilichowekwa benki na kilichotolewa benki pamoja na matumizi ya fedha hizo tangu kuanza kwa uzalishaji mwaka 2016.
Wanasema hatua hiyo itasaidia kubaini kama kampuni ilikuwa inapokea fedha bila kuziweka benki na, endapo kutabainika matumizi mabaya, waliohusika wawajibishwe ili kuinusuru kampuni.
Wameiomba Serikali iwasaidie kupata taarifa rasmi ya kampuni kutoka BRELA ili kuthibitisha wakurugenzi wote waliosajiliwa, tarehe walipoteuliwa, wanahisa waliosajiliwa na taarifa nyingine za kampuni.
Wanasema suala hilo ni muhimu kwa sababu kuna wanachama wapya ambao, kwa mujibu wa madai yao, si waanzilishi na hawajui kikao kilichowapitisha kuwa wanahisa.
Wakurugenzi hao wanaomba Serikali kuingilia kati mgogoro uliopo baina yao na wakurugenzi wenzao, wakisema kwa miaka mingi wamekuwa wakifuatilia kufahamu shughuli zinazoendelea kwenye kampuni lakini hawapati ushirikiano .
Wanasema hali hiyo inawashangaza kwa kuwa wao ndio waliohusika katika kuanzishwa kwa kampuni na walitoa michango mbalimbali kuhakikisha kampuni inapata usajili na leseni, lakini baada ya usajili wanadai walitengwa na wenzao.





Post a Comment