RC PWANI AAGIZA WAKUU WA WILAYA KUTENGA MAENEO KWA AJILI YA WATAKAOATHIRIKA NA MVUA ZA EL- NINO

Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo amewaagiza Wakuu wa Wilaya pamoja na viongozi mbalimbali waliopo katika Wilaya hizo kutenga maeneo maalum kwa ajili ya kuwahifadhi wahanga ambao wataathirika kipindi cha mvua za El-Nino.
Nyongo ,ametoa kauli hiyo Septemba 16/2026 wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu namna ambavyo Mkoa ulivyojipanga kukabiliana na majanga mbalimbali katika kipindi cha mvua za El-Nino zinazotarajia kunyesha hivi karibuni kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali Hewa ( TMA).
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo akizungumza na Waandishi wa habari Septemba 16/2026 kuhusu namna Mkoa ulivyojipanga kukabiliana na majanga ya mvua za El-Nino zinazotarajia kunyesha hivi karibuni kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).Amesema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kukabiliana na majanga katika kipindi cha mvua za El-Nino na moja ya mipango ni kuhakikisha inaweka mazingira mazuri kwa Wananchi.
Nyongo amesema hatua ambazo zimechukuliwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi juu ya athari za mvua hizo pamoja na kuwasisitiza Wananchi wanaoishi katika maeneo ya mabondeni kuhama maramoja kwa ajili ya kupisha mvua hiyo.
Amesema pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa lakini pia ni lazima Wakuu wa Wilaya na viongozi wake wahakikishe wanatenga maeneo maalum ili endapo kutatokea na madhara ya kibinadamu basi wapate sehemu sahihi ya kuwahifadhi.
Nyongo,ameongeza kuwa suala la maandalizi ya kukabiliana na mafuriko yanatokana na mvua hizo si tu ya Serikali bali ni jukumu la watu wote ambapo miongoni mwa jukumu hilo ni kuchukua tahadhari ikiwa pamoja na kuhama katika maeneo ya mabondeni.
Amesema mbali na kuhama katika maeneo hayo lakini pia yapo mambo muhimu ya kuzingatia wakati mvua hizo zikinyesha ikiwemo kusafisha mitaro na njia za maji zilizopo katika maeneo ya biashara,kuondoa taka zinazoziba mitaro na kuepusha watoto kuacha kucheza katika mito iliyojaa maji.
Nyongo amesema ,mambo mengine muhimu ni pamoja na kuandaa tochi ,chakula cha kutosha,kulinda afya na Mazingira,pamoja na wamiliki wa mifugo kuchukua tahadhari ya kuhifadhi mifugo yao sehemu zenye usalama.
Ameongeza kuwa hatua nyingine zakuepuka ni pamoja na madereva kuacha kupitisha magari katika mito iliyojaa maji huku akiwataka Wananchi waepuke kuvuka mito iliyojaa maji pamoja na kuacha tabia ya kukaa chini ya miti wakati mvua ikinyesha.
Nyongo pamoja na mambo mengine amewaelekeza viongozi mbalimbali wa Serikali na kidini kuendelea kutoa elimu kwa Wananchi juu ya athari zinazoweza kujitokeza na hatua za kujikinga na mafuriko ya mvua hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Waandishi wa habari wa Mkoa wa Pwani.Amesisitiza TARURA na TANROADS kuendelea kuhakikisha madaraja yote hatarishi yanafanyiwakazi na madaraja yanayojengwa yawekwe katika mazingira mazuri ili yasilete madhara kipindi ambacho mvua hizo zinanyesha.
"Serikali Mkoa wa Pwani imejipanga kukabiliana na mvua za El-Nino kwa kufanya maandalizi ya kuhakikisha miundombinu yote ya maji inakuwa sawa lakini niwaombe na Wananchi wenyewe waanze sasa kuchukua tahadhari ikiwemo wale wanaoishi mabondeni kuhama maramoja", amesema Nyongo.
Kuhusu Wananchi ambao wanaishi katika maeneo ya delta Nyongo amesema kuwa kamati ya afya inayatambua maeneo hayo na Serikali tayari imefanya maandalizi ya kutosha ikiwemo kutoa elimu juu ya madhara yanayoweza kutokea kutokea kufuatia mvua hizo.
Amesema kuhusu suala la maji ya matumizi ya nyumbani tayari Ruwasa na mamlaka zingine za maji zimekusanya dawa za kutosha kwa ajili ya kutibu maji pale yatakapoathiriwa na hata suala la umeme Tanesco imejipanga kubadilisha nguzo zilizochoka na zile zilizodondoka na kuweka nguzo mpya ili kusudi zisisumbue kipindi cha mvua.
Hata hivyo,Nyongo amewaomba Wananchi kuhakikisha wanatoa taarifa sahihi kwa Mamlaka kabla na kipindi cha mvua ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa na hivyo kuokoa maisha ya Wananchi wa eneo husika.


Post a Comment