HEADER AD

HEADER AD

MEYA KIBAHA AWAASA WAHITIMU DARASA LA SABA KUWA WAZALENDO NA KULINDA AMANI YA TAIFA

Na Gustaphu Haule, Pwani 

MSTAHIKI Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Dr. Mawazo Nicas amewataka wanafunzi waliohitimu darasa la Saba katika Shule ya Msingi Zegereni iliyopo Kata ya Visiga  kuwa wazalendo sambamba na kulinda amani ya Taifa.

Pia Dk. Nicas amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika kujenga miundombinu ya elimu nchini kwahiyo wanafunzi wanapaswa kuitumia miundombinu hiyo kwa ajili ya kupata elimu ambayo itawasaidia katika maisha yao.

Dr.Nicas ametoa kauli hiyo Septemba 16/2026 wakati akizungumza na wanafunzi,walimu ,Wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali na vyama vya Siasa katika  mahafali ya pili ya Shule ya Msingi Zegereni iliyopo Kata ya Visiga.

        Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akizungumza katika mahafali ya pili ya Shule ya Msingi Zegereni yaliyofanyika Septemba 16/2026 Shuleni hapo.

Dr.Nicas amesema, wanafunzi wanatakiwa kuwa wazalendo  pamoja na kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yaliyowekwa na kwamba kwasasa serikali imeweka kiwango cha elimu ya lazima kuwa ni  kidato cha nne. 

"Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan imelenga katika kuona miundo mbinu ya  elimu inaboreshwa zaidi na kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwenye mazingira mazuri na wanapata elimu inayostahili", amesema Dr Nicas.

Amesema, kila  mwanafunzi anawajibika kwa nafasi yake ili aweze kufanya vizuri kwenye masomo yao kwa sababu taifa linawategemea katika kufanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo.

Amesema Taifa linategeme mambo mazuri kutoka kwao pamoja na kufanyakazi kwa bidii ,kuitunza amani ya nchi na kuifanya Tanzania kuwa sehemu nzuri ya kuishi kama ilivyo hivi sasa.

         Wanafunzi wa darasa la Saba katika Shule ya Msingi Zegereni wakiwa katika picha ya pamoja na Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas.

",Mnahitimu leo lakini Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan aliyejenga Shule hii ,akaleta walimu hapa, ataendelea kulipa walimu mishahara na kuhudumia Shule hii hadi leo anatarajia kuwaona tena mkienda Sekondari lakini mkumbuke mnadeni la kuitumikia nchi yenu kizalendo,"amesema Dr.Nicas

Dr.Nicas ameahidi kutatua changamoto ya ujenzi wa ofisi ya walimu katika Shule hiyo ambao kwasasa walimu wote wanatumia chumba kimoja sambamba na kujenga miundombinu ya barabara kutoka barabara kuu ya Morogoro hadi kufika katika Shule hiyo.

Diwani wa Kata ya Visiga Mohamed Mpaki amemshukuru Meya huyo kwa kazi kubwa anayoifanya huku akisema katika kipindi kifupi alichokaa madarakani Kata ya Visiga imepata maendeleo makubwa ikiwemo ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi na Sekondari.

     Diwani wa Kata ya Visiga Mohamed Mpaki akizungumza katika mahafali ya Shule ya Msingi Zegereni yaliyofanyika Septemba 16/2026.

Mpaki ,amesema kuwa Kata ya Visiga Ina Shule ya Sekondari moja tofauti na Shule nyingine ambapo ametumia nafasi hiyo kumuomba Meya huyo kuona uwezekano wa kujenga Shule nyingine ya Sekondari katika Kata hiyo .

Mpaki amesisitiza kwa Meya huyo kuongeza jitihada katika ujenzi wa Shule barabara kutoka Visiga kuelekea kituo cha afya pamoja na kutoka Visiga kuelekea Mbwawa ambazo kwasasa Zina hali mbaya na uenda katika mvua za El-Nino zinaweza zisipitike kabisa.

Mhitimu wa darasa la Saba katika Shule hiyo Hajat Abdul ameomba Meya huyo kuhakikisha anajenga uzio katika Shule hiyo kwani utasaidia kuimarisha ulinzi na usalama wa wanafunzi na walimu na kuzuia utoro  .

Hata hivyo,Abdul  amesema kazi ya kujenga uzio katika Shule hiyo ni kubwa ambapo amewaomba ushirikiano wa viongozi, wadau wa maendeleo na wahisani mbalimbali kujitokeza kushirikiana ili kukamilisha ujenzi huo.

        Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Kata ya Visiga katika mahafali ya Shule ya Msingi Zegereni.


No comments