RC PWANI AWAAGIZA WAKUU WA WILAYA KUCHUKUA TAHADHARI YA EL-NINO

Na Gustaphu Haule, Pwani
MKUU Wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo amewaagiza Wakuu wa Wilaya kuendelea kujiandaa pamoja na kufanya tathmini za mara kwa mara katika kujiweka tayari kupambana na athari zitakazojitokeza kufuatia mvua za El-NINO.
Nyongo amesema Serikali za Wilaya ziwe tayari kupokea misaada,"," mbalimbali ambayo itasaidia kupambana na mafuriko yatakayotokana na mvua za El-nino pamoja na wananchi ambao wataathirika na mvua hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo akizungumza na wadau wa maafa wa Mkoa wa Pwani katika kikao kilichofanyika Septemba 21/2026 Kuhusu mvua za El-nino.Nyongo ametoa kauli hiyo Septemba 21/2026 wakati akizungumza katika kikao cha wadau wa maafa wa Mkoa wa Pwani kilichofanyika kwa ajili ya maandalizi ya kupambana na madhara ya El-NINO endapo yakitokea.
Nyongo amesema kuwa mkoa wa Pwani upo katika hatari kubwa ya kukumbwa na mafuriko ya mvua za El-nino kutokana na kuwepo karibu na Bahari na kwamba Wilaya ambazo zipo katika hatari kubwa ni Rufiji, Kibiti na Mafia.
Amesema kutokana na hali hiyo Mkoa wa Pwani umejipanga vizuri katika kukabiliana na mvua za El-nino na ndio maana hata bajeti ya kupambana na hali hiyo imefikia Sh.bilioni 32 ambapo kati ya hizo Wilaya ya Rufiji pekee zitaelekezwa Tsh.Bilioni 17.
Wadau wa maafa Mkoa wa Pwani wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa Stanslaus Nyongo katika kikao maalum kilichofanyika Septemba 21/2026.Ameongeza kuwa lazima Wakuu wa Wilaya waendelee kujipanga na kuweka mikakati vizuri ikiwemo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali waliopo katika maeneo yao ili hata kunapotokea na mvua hizo madhara yasiwe makubwa.
Amewaomba wadau kujitolea katika kuchangia vifaa mbalimbali yakiwemo magodoro, vyakula, vifaa vya uokozi na vinginevyo lakini suala la kuchangia fedha utaratibu utatolewa kupitia ofisi ya Waziri Mkuu kitengo cha maafa.
Alisema wadau ni muhimu katika jambo mashirikiano ya kupambana na suala la maafa lakini Mkoa wa Pwani ni Mkoa wa viwanda na kwa umoja wao wameweza kujadili nini chakufanya baada ya mvua za El-nino lakini amefurahi kuona wadau wapo tayari kuchangia.
"Nimefurahi kuona wawekezaji wengi wamejitolea na wengine wapo tayari kuchangia vifaa mbalimbali na hii ni kuonyesha namna ambavyo wadau wakishirikishwa vizuri jambo linapata ufumbuzi wa pamoja,"amesema Nyongo.
Nyongo amewatoa wasiwasi wawekezaji hao kuwa Serikali imejipanga vizuri katika kuhakikisha miundombinu ya uwekezaji inakuwa salama kama vile umeme, afya, maji na sekta nyingine zinaendelea kuimarisha ili kuwaondolea usumbufu katika uzalishaji.
Ameitaka TARURA na TANROADS mkoa wa Pwani kufanya utafiti wa kubaini maeneo yenye shida na ikiwezekana yafanyiwe kazi ya haraka kabla ya mvua kuanza ili kusudi kuepusha madhara makubwa hasa ya wananchi kupoteza maisha.
Wadau wa maafa Mkoa wa Pwani wakiwa katika kikao cha kujiandaa na mapambano dhidi ya mvua za El-nino zinazotarajia kunyesha Oktoba 2026.Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Luteni Fredrick Komba amesema kuwa Wilaya ya Rufiji ni Wilaya ambayo mafuriko yanatokea mara kwa mara na kwamba mara ya mwisho mafuriko hayo yalitokea mwaka 2023/2024 na madhara yalikuwa makubwa hususani katika miundombinu.
Komba, amesema kuwa mwaka huu Wilaya imejipanga vizuri kwa kuandaa mpango kazi ambao umeainisha shughuli za kuzuia, kupunguza madhara na majanga yakitokea na namna ya kurejesha hali ya awali.
Amesema tayari hadi sasa wamebainisha maeneo yenye hatari zaidi ambayo ni katika Kata nne ikiwemo Kata ya Umwe, Mbwara, Muhoro na Chumbi na kwamba madhara makubwa katika maeneo hayo huwa ni kuharibika kwa miundombinu ya vivuko na barabara.
Komba, ameongeza kuwa anashukuru Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) ambao wamekuwa wakifanyakazi kubwa na kuchukua hatua ya kurudisha mawasiliano ya miundombinu ya barabara katika Wilaya hiyo.
Amesema mbali na hayo lakini pia yapo maeneo ambayo wameyabainisha ambayo ni salama na yanaweza kutumika kwa dharula katika kuwahifadhi wahanga ambayo ni Ikwiriri, Chumbi na Kipugila na kuhakikisha uwepo wa raslimali na kwamba hadi sasa wanaboti 24 ambapo kati ya hizo za Serikali ni saba na 14 za watu binafsi.
"Kingine tulichoangalia ni eneo la kutolea huduma ya afya, ikiwemo Zahanati na vituo vya afya kwa kuhakikisha kunakuwa na magari ya wagonjwa ambapo hadi sasa yapo magari 12 na mengine ya dharula 18, amesema Komba.
Hata hivyo, Komba amesema kuwa kwasasa wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi, kufanya usafi wa kila siku wa kuzibua mitaro, kufuatilia ubora wa miundombinu ya barabara, umeme, maji na huduma nyingine huku akisema bajeti ya Wilaya ya Rufiji katika kukabiliana na hali hiyo ni sh.milioni 700.



Post a Comment