SHAKIL WA FRELIMO AWATAKA WALIOPEWA MAFUNZO KUYATUMIA KUTATUA CHANGAMOTO NA KUBORESHA MAISHA YA WATU
Na Gustaphu Haule, Pwani
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Frelimo cha nchini Msumbiji ambaye pia ni Mjumbe wa bodi ya udhamini ya Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Shakil Aboobacar amewataka washiriki wa mafunzo ya ukufunzi kutoka katika vyama sita vya ukombozi kuhakikisha wanakwenda kutumia mafunzo hayo katika kutatua changamoto za wanachama na kuboresha maisha ya watu wao.
Aboobacar, ametoa kauli hiyo Septemba 19/2026 wakati akifunga mafunzo kwa wakufunzi 37 kutoka vyama sita vya ukombozi mafunzo ambayo yalikuwa yakifanyika katika chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere yaliyodumu kwa muda wa siku 45.
Katibu Mkuu wa Chama Cha FRELIMO cha nchini Msumbiji Shakil Aboobacar akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa katika hafla ya kufunga mafunzo ya wakufunzi kutoka vyama sita vya ukombozi, hafla hiyo ilifanyika Septemba 19/2026.
Aboobacar amesema kupitia mafunzo hayo nchi zao zitakuwa huru kujitegemea lakini pia kutoa nafasi kwa viongozi kufanya vizuri katika nchi zao kupitia vyama vyao vya siasa.
Amesema matokeo ya mafunzo hayo ni kuangalia maslahi ya watu wote na kwamba anaamini siku 45 za mafunzo zinakwenda kubadilisha maisha ya nchi zao.
"Sisi viongozi wa vyama vya siasa mafunzo haya yatasaidia pale tunapoingia katika kampeni za watu hasa katika kuboresha maisha ya watu na nchi zetu na kuleta matarajio ya wananchi,"amesema Aboobacar.
Aboobacar ameongeza kuwa wakufunzi hao waende kufanya kazi zinazokubalika na wananchi japo anajua changamoto ni nyingi lakini ikibidi wawe karibu na wananchi katika kusaidiana kutatua shida na changamoto hizo.
Wakufunzi wa mafunzo ya ukufunzi katika chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere kilichopo Kibaha Mkoa wa Pwani.
Amesema matarajio yake ni kuwa mafunzo hayo yatasaidia kufundisha wanachama wao ili waweze kuelewa mipango ya vyama vyao na hivyo kuzidi kusongambele katika kushika dola.
Amesema wakufunzi na taasisi zao ndio sehemu ya matumaini hasa katika kuwanoa vijana kisiasa na hasa katika ajira hivyo wanakazi kubwa ya kwenda kuwaandaa vijana ili waweze kufanyakazi na kukomesha matatizo ya watu.
"Hatujafanya vizuri sana kwa watu wetu lakini kupitia mafunzo haya vyama vitakuwa vizuri na vitajiimarisha zaidi na watu ambao watataka kuviharibu vyama vyetu watashindwa, hivyo twendeni kuhamasisha umoja wa watu wetu wa vyama kwani kwakufanya hivyo itasaidia katika kuimarisha uchumi wa nchi zetu,"amesema Aboobacar
Aboobacar amempongeza Mkuu wa chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Profesa Chijoriga kwa kazi kubwa na nzuri ya usimamizi wa chuo hicho hasa katika kuyafanya mazingira ya chuo hicho kuwa mazuri wakati wote.
Washiriki wa hafla ya ufungaji wa mafunzo ya ukufunzi kwa vyama sita vya Ukombozi iliyofanyika katika chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Septemba 19/2026.
Amesema amewaeleza wakufunzi hao kuwa Profesa Masselina Chijoriga ataandika barua kwenda katika vyama vyao kuwatambulisha wakufunzi wote walioshiriki mafunzo hayo ili waweze kusambaza elimu waliyoipata katika chuo hicho.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Tanzania Bara Aggrey Mwanry ametumia nafasi hiyo kumshukuru na kumpongeza Katibu Mkuu wa Frelimo kwa kukubali kuungana pamoja katika kufunga mafunzo hayo.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Aggrey Mwanry wa kwanza kulia Akiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Chama Cha FRELIMO Shakil Aboobacar(katikati) pamoja na Mkuu wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Profesa Masselina Chijoriga (kushoto).
Pia Mwanry amempongeza Mkuu wa chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Profesa Masselina Chijoriga kwa kazi nzuri ya usimamizi wa chuo hicho ambapo amemuomba kuendelea katika utekelezaji wa majukumu yake ndani ya chuo hicho.
Amesema muda wa siku 45 wanachama wa vyama sita vya ukombozi kuja kujifunza chuoni hapo ni jambo la kujivunia na kwamba ni hatua ya kimaendeleo katika vyama vyao.
Amesema kuwa muungano huo ni mzuri kwakuwa unakwenda kuleta umoja wa makada na vyama vyao huku akiwaomba washiriki wa mafunzo hayo wakirudi katika nchi zao wakaendelee kujifunza na kuwafundisha watu wao kwa ajili ya kuendeleza vyama vyao.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere Profesa Masselina Chijoriga amesema kuwa mafunzo hayo yalikuwa maalum kwa ajili ya wakufunzi ambao wakifika katika nchi zao watakuwa wanaendelea kuwafundisha watu wa vyama vyao.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere profesa Masselina Chijoriga akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo ya wakufunzi kutoka vyama sita vya ukombozi, hafla hiyo ilifanyika Septemba 19/2026 katika chuo hicho.
Profesa Chijoriga amesema kuwa mafunzo hayo yalianza Agosti mwanzoni na kumaliza Septemba 19/2026 yakiwa yameshirikisha wanachama 37 kutoka vyama sita vya ukombozi ikiwemo FRELIMO, CCM, ZANU PF, SWAPO, ANC na CPC.
Amesema katika kipindi cha mafunzo hayo wakufunzi hao walikuwa wakifundishwa mambo mbalimbali ikiwemo suala la uwajibikaji, uchumi, utawala, maadili, maendeleo na sera zake pamoja na mengine yenye kuimarisha vyama vya siasa katika nchi zao.
Hata hivyo, Chijoriga amewaambia wahitimu wa mafunzo hayo kuwa anatamani kuona matunda ya mafunzo hayo kwani kama yatatumika vizuri anaimani yatasaidia kuimarisha vyama vya siasa katika na nchi husika.
Hafla ya ufungaji mafunzo ya Wakufunzi wa vyama sita vya Ukombozi iliyofanyika Septemba 19/2026 katika chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere.







Post a Comment