Home
/
HABARI KITAIFA
/
SERIKALI PWANI YAWATAKA WENYE MASHIRIKA KUTOTEGEMEA FEDHA ZA UFADHILI BADALA YAKE WAWE WABUNIFU
SERIKALI PWANI YAWATAKA WENYE MASHIRIKA KUTOTEGEMEA FEDHA ZA UFADHILI BADALA YAKE WAWE WABUNIFU

Na Gustaphu Haule,Pwani
SERIKALI Mkoa wa Pwani imewataka waendeshaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali kuacha kutegemea zaidi fedha za ufadhili kutoka nje ya nchi na badala yake wawe wabunifu katika kujitegemea wao wenyewe.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Richard Kayombo wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Mashirika yasiyo ya kiserikali uliofanyika Septemba 18,2026 katika ukumbi wa mikutano uliopo katika jengo la Mkuu wa Mkoa wa Pwani.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Richard Kayombo akifungua mkutano wa mwaka wa Mashirika yasiyo ya kiserikali uliofanyika Septemba 18/2026 .
Kayombo katika mkutano huo alikuwa akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo ambapo amesema lazima kwasasa mashirika hayo yaangalie namna ambavyo yanaweza kujitegemea.
Amesema kuwa Mkoa wa Pwani unafursa nyingi na endapo wakizitumia vizuri upo uwezekano mkubwa wa mashirika hayo kujiendesha yenyewe na hivyo kuacha utegemezi kutoka kwa wafadhili ambao utoaji fedha kwa masharti makubwa.
Kayombo ametaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na Kilimo,Uvuvi,Ufugaji ,utalii,na uzalishaji kupitia viwanda na kwamba fursa hizo bado zinahitaji uwekezaji mkubwa na kama zitatumika vizuri ni wazi kuwa mashirika yatakuwa na uwezo mkubwa wa kujitegemea.
Washiriki wa mkutano wa mwaka wa mashirika yasiyo ya kiserikali uliofanyika Septemba 18/2026 Kibaha Mkoa Pwani.
Amesema Serikali ya Mkoa wa Pwani inatambua na kuthamini mchango wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kazi kubwa wanazofanya hasa katika kupambana na mambo mbalimbali ya kijamii ikiwemo watoto,huduma za kijamii, mazingira.
Amesema Taifa linaendelea kubadilika kwa kasi, idadi ya watu inaongezeka ndio maana kauli mbiu inaeleza kuwa "Fikra mpya kuhusu uendelevu wa Mashirika yasiyo ya kiserikali,ubia,na upatikanaji wa raslimali fedha kupitia vyanzo vya ndani.
Amesema ni muhimu muhimu kila kiongozi wa Shirika kuelewa kauli mbiu hiyo kwani imekuja wakati sahihi kwakuwa Mkoa wa Pwani bado una mahitaji mengi ya kufanya sambamba na kuwaletea Wananchi maendeleo.
Kayombo amesema kuwa anataka kuona mashirika yanajenga uchumi imara katika kuendeleza jamii pamoja na kuona yanashiriki katika dira ya maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050.
Amesema pamoja na Serikali kuweka mazingira wezeshi lakini mashirika yanawajibu wa kuwa waadilifu na uwazi bila kuvunja Sheria na kwamba fedha za miradi sio za mtu binafsi kwani ni lazima fedha hizo zionyeshe uhalisia.
Kayombo ameongeza kuwa anataka mashirika yasiyo ya kiserikali yawe na mahusiano mazuri na Serikali za Mitaa ambapo amewasisitiza wasajili kuacha kuwa na vikwazo vya usajili bali watoe ushauri na namna ya kuyaendesha mashirika hayo.
"Msiendeshe mashirika kwasababu tu ya fedha bali nataka kuona uwajibikaji na uwajibikaji huo maana yake kila Shirika linawajibu wa kuwa wawazi na uadilifu lakini mtambue kuwa fedha za Shirika sio mali za mtu binafsi na hivyo zifanyekazi iliyokusudiwa,",amesema Kayombo.
Hatahivyo,Kayombo ameahidi kutoa ushirikiano mkubwa kwa mashirika hayo kwakuwa anayahitaji katika kusaidia jamii na hatamani kuona Shirika linafungwa kwa sababu ndogo inayoweza kutatulika.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Pwani Grace Tete amesema kuwa lengo la mkutano huo ni kufanya tathmini ya shughuli mbalimbali zilizofanywa na mashirika hayo pamoja na kuangalia changamoto zao.
Tete,amesema wamekuwa wakiona mashirika yanatekeleza shughuli nyingi ikiwemo afya ,elimu, watoto,ukatili wa kijinsia na uwezeshaji Wananchi na kwamba hadi sasa zaidi ya Wananchi 82000 wamefikiwa.
Amesema kutokana na umuhimu huo wameona ni vyema wakaangalia changamoto zinazowakabili ambapo moja ya changamoto ni ukosefu wa fedha ambapo wamekubaliana kila Shirika liende kuangalia kitu gani wanaweza kufanya ili kujipatia fedha za kuendesha shughuli zao.
Baadhi ya viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali wakiwa katika mkutano wa mwaka uliofanyika Kibaha Septemba 18/2026.
Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoa wa Pwani Prisca Ngweshemi amesema kuwa wamekutana kukumbushana na kupeana habari za msingi ambazo wao kama wadau wa maendeleo na mkono wa pili wa Serikali kwamba watafikiaje kutenda kazi pasipo fedha za wafadhili.
Amesema Mkoa wa Pwani ni Mkoa wa kimkakati hivyo ameipongeza Serikali kwakutambua umuhimu wa mashirika hayo na kwamba wapo tayari kushirikiana katika kila jambo ili kusudi waweze kutimiza malengo yao ya kusaidia jamii.
Ngweshemi amesema amefurahi kuona Serikali ikifungua milango kwa taasisi na mashirika binafsi na kwamba hatua hiyo itasaidia Serikali kupata taarifa sahihi za mashirika zikazoingia katika mfumo rasmi.
Hata hivyo, Ngweshemi amekiri kuwa yapo mashirika ambayo taarifa zao hazipatikani katika mfumo ambapo ameomba Serikali kuandaa kikao maalum kwa ajili ya kufundisha namba ya kuingiza taarifa katika mfumo huo.



Post a Comment