TARURA YAKAMILISHA UJENZI BARABARA INAYOUNGANISHA KATA YA MAFIZI NA MZENGA
Na Gustaphu Haule, Pwani
SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini ( TARURA) Wilaya ya Kisarawe imekamilisha ujenzi wa daraja kubwa la Mto Kitomondo na kufanikiwa kuwaunganisha wananchi wa Kata ya Mafizi na Kata ya Mzenga ambao kwa muda mrefu walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya mawasiliano hususani wakati wa mvua.
Kaimu Meneja wa TARURA Wilaya ya Kisarawe Japhet Langay , amewaambia Waandishi wa habari waliotembelea mradi huo Septemba 14,2026 kuwa ujenzi wa daraja hilo ulianza Mei 21,2025 na umekamilika Agosti 30,2026 ukiwa chini ya Mkandarasi Neloyt Company Ltd kwa gharama ya Sh.milioni 380.
Kaimu Meneja wa Tarura Wilaya ya Kisarawe Japhet Langay akitoa ufafanuzi kwa Waandishi wa habari kuhusu ujenzi wa daraja la Kwembe linalounganisha Wilaya ya Ubungo na Wilaya ya Kisarawe.
Langay amesema anaishukuru Serikali Kuu kwani mara baada ya kuandika maombi ya fedha za kutekeleza mradi huo zilitolewa kwa haraka na hivyo kuanza ujenzi huo ambao kwasasa umekamilika kwa asilimia 100.
Amesema awali daraja hilo lilikuwa ndogo na kipindi cha mvua lilikuwa likizidiwa kiasi ambacho kilipelekea maji kujaa na hivyo kusababisha Wananchi kushindwa kuvuka na wakati mwingine maji yakijaa magari, bodaboda na Wananchi walikuwa wakisubiri hadi siku tatu ili maji yapungue.
"Awali kulikuwa na hatari kubwa sana kwani mvua ikinyesha mawasiliano yanakatika,magari , bodaboda na waenda kwa miguu walikuwa wakifika hapa wanakwama kuvuka na badala yake ilikuwa ikiwalazimu kusubiri maji yapungue na ndipo wavuke lakini kwasasa hali ni shwari," amesema Langay.
Langay amesema kuwa mbali na ujenzi wa daraja la Kitomondo lakini pia Tarura imekamilisha ujenzi wa daraja la lingine la Kwembe linalounganisha Manispaa ya Ubungo na Wilaya ya Kisarawe.
Kaimu Meneja Tarura Wilaya ya Kisarawe Japhet Langay,akiwa na mafundi wa daraja la Kitomondo pamoja na Waandishi wa habari walipokwenda kutembelea mradi wa ujenzi wa daraja la Kitomondo Septemba 14,2026.
Amesema daraja hilo linaunganisha barabara inayotoka Kisarawe na kuelekea katika hospitali ya Muhimbili iliyopo Mloganzila na lilianza kujengwa Mei 2025 na kukamilika Juni 2026 likiwa limejengwa na mkandarasi Old South Company Limited kwa gharama ya Sh.milioni 360 .
Langay amesema pamoja na ujenzi wa madaraja hayo lakini pia Tarura Wilaya ya Kisarawe inaendelea kuchukua tahadhari dhidi ya mvua za El-Nino zinazotarajia kunyesha hivi karibuni kwa kufanya usafi na kuzibua mitaro yote iliyoziba katika maeneo mbalimbali.
Msimamizi wa kampuni ya ujenzi ya Neloyt Company Ltd Wilson Ponela amesema anaishukuru Serikali ya awamu ya Sita kupitia Tarura kwa kuwaamini na kuweza kuwakabidhi mradi huo.
Daraja la Mto Kitomondo lililojengwa na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Kisarawe kupitia mkandarasi Neloyt Company Ltd.
Ponela amesema walipewa miezi sita kukamilika mradi huo na wamefanikiwa kukamilisha mradi huo kulingana na muda waliopewa japo wakati wa kipindi cha mvua walisimama kwa muda.
Amesema katika kipindi cha utekelezaji wa mradi huo wamekuwa wakishirikina vizuri na Tarura Wilaya ya Kisarawe na hata fedha zilikuwa zinatolewa kwa wakati ndio maana wameweza kutekeleza mradi huo mapema .
Said Marungo dereva wa bodaboda Mkazi wa Kata ya Mafizi ameishukuru Serikali kwa kuwajengea daraja hilo kwakuwa mwanzo walikuwa wanapata shida ya kuvuka upande wa pili kutokana na maji kujaa katika daraja hilo wakati wa mvua.
Baadhi ya Waandishi wa habari wa Mkoa wa Pwani pamoja na Wananchi wakiwa katika daraja la Kitomondo lililojengwa na Tarura Wilaya ya Kisarawe.
Marungo alipokuwa anafika eneo hilo hususani wakati wa mvua alikuwa anashindwa kuvuka hali iliyomlazimu kukaa katika eneo hilo kwa muda wa siku mbili hadi tatu ili kusubiri maji yapungue.
Amesema wakati mwingine mvua zilipokuwa zinaendelea kunyesha akifika katika daraja hilo alikuwa anavushwa yeye na pikipiki yake kwa kubebwa juu na watu ambao walikuwa wanatumia miti kwa gharama ya Sh.5000.
"Kiukweli ujenzi wa daraja hili la Kitomondo ni mkombozi kwetu kwani awali tulikuwa tunakwama hapa hadi siku tatu jambo ambalo lilikuwa linakwamisha shughuli zote za uzalishaji wa uchumi lakini leo tunapita bila shida wala usumbufu wowote", amesema Marungo
Nae Yahaya Hamisi dereva wa pikipiki ya magurudumu matatu( Guta) amesema kuwa daraja hilo kwasasa linakwenda kuinua uchumi kwa Wananchi wa Kata ya Mzenga na Kata ya Mafizi.
Matumizi ya daraja la Mto Kitomondo linalounganisha Kata ya Mafizi na Mzenga Wilayani Kisarawe kama inavyoonekana pichani.
Hamisi amesema Wananchi wa maeneo hayo wanategemea zaidi kilimo na ufugaji na walikuwa wanashindwa kufika sokoni kwa ajili ya kuuza mazao yao lakini kukamilika kwa daraja hilo kumewarahisishia katika kusafirisha mazao na bidhaa zao mbalimbali.
Hata hivyo, Hamisi ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kufanikisha kuwajengea daraja hilo huku akiomba waendelee kuwasaidia Wananchi katika kutatua changamoto zao.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini TARURA Wilaya ya Kisarawe Japhet Langay akikagua vipimo vya ujenzi wa daraja la Kitomondo linalounganisha Kata ya Mzenga na Mafizi na pembeni ni msimamizi wa ujenzi huo kutoka kampuni ya Neloyt Wilson Ponela.







Post a Comment