WAUMINI SDA WACHANGA FEDHA KUTUNISHA MFUKO WA WATU WENYE ULEMAVU, SARA ORINDO ACHANGA TSH. MILIONI MOJA

Na Mwandishi Wetu, Tarime
WAUMINI wa Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA), wakiwemo wachungaji, wamechangisha fedha kwa ajili ya kutunisha mfuko wa kuwawezesha watu wenye ulemavu wa viungo ndani ya kanisa, ambao utasaidia kutekeleza shughuli mbalimbali zinazowahusu watu wenye uhitaji.
Fedha na misaada mbalimbali, ikiwemo nguo na vifaa wezeshi, vilitolewa Septemba 12, 2026, siku ya jumamosi wakati wa kuhitimisha kambi la watu wenye ulemavu wa viungo Kanisa la Waadventista Wasabato, Jimbo la Mara Kaskazini.
Kambi hilo limefanyika kwa siku saba katika Chuo cha Mwera Vision, ambapo baadhi ya watu wenye ulemavu walikaa kambini kwa muda huo wakijifunza mafundisho ya Biblia, kushiriki vipindi mbalimbali pamoja na uimbaji.
Mgeni rasmi katika harambee hiyo alikuwa Sara Orindo, mkazi wa Kijiji cha Mjini Kati, Nyamongo, Wilaya ya Tarime, ambaye alichangia Shilingi milioni moja.
Sara Orindo, mkazi wa Kijiji cha Mjini Kati, Nyamongo, Wilaya ya Tarime, aliyekuwa mgeni rasmi siku ya Sabato wakati wa kuhitimishwa kambi la watu wenye mahitaji maalum , Jimbo la Mara Kaskazini.
Sara alisema alipata mwaliko kutoka kwa dada yake, Bhoke Orindo, mwenye ulemavu wa macho, ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa kambi hilo, na kusema kuwa familia yao inaendelea kumuunga mkono ndugu yao katika kufanikisha kazi ya Mungu.
"Pamoja na ulemavu wa macho, Bhoke hajawahi kukata tamaa. Nawatia moyo watu wenye ulemavu msikate tamaa. Pia msibweteke kwa sababu tu ni walemavu, bali fanyeni kazi pamoja na kumtumikia Mungu," amesema Sara.
Sara aliungwa mkono na waumini kutoka Nyamongo, akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji cha Kewanja, maarufu kwa jina la Chia, familia ya Orindo, Happenes, Joseph, maarufu kwa jina la Chinga, pamoja na wengine.
Kwaya ya Uinjilisti kutoka Nyamongo ilitoa msaada wa vitu mbalimbali, ikiwemo sabuni na kanga, vyenye thamani ya jumla ya Shilingi milioni moja, kwa ajili ya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa viungo.
Waliosimama mbele wakionesha ishara ni kwaya ya watu wenye ulemavu wa kutosikia wakiimba wimbo. Kulia ni baadhi ya wanakwaya ya Uinjiristi kutoka Nyamongo.
Josephati Mwita, mkazi wa Nyamongo, alitoa vifaa wezeshi, ikiwemo fimbo nyeupe, magongo, mikongojo, baiskeli mbili za magurudumu matatu, kiti mwendo kimoja pamoja na kanga, vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni mbili.
Mwenyekiti wa kambi la watu wenye ulemavu wa viungo , Bhoke Orindo amewashukuru watu wote walioguswa na kutoa michango yao iliyosaidia kufanikisha kambi la watu wenye ulemavu wa viungo.
Mwenyekiti wa kambi la watu wenye ulemavu wa viungo , Bhoke Orindo( kushoto) , kulia ni mdogo wake Sara Orindo aliyekuwa mgeni rasmi katika changizo la kutunisha mfuko idara ya huduma wezeshi.
Mkurugenzi wa Huduma Binafsi, Huduma Wezeshi na Shule ya Sabato wa Jimbo la Mara Kaskazini, Mchungaji Gadiel Mziray, aliwashukuru watu wote walioguswa na kutoa michango yao iliyosaidia kufanikisha kambi pamoja na misaada mbalimbali kwa wahitaji.
Mchungaji Mziray alisema amevutiwa na ushirikiano wa watu wenye ulemavu wa viungo katika kuhakikisha kambi linafanyika na kukamilika vyema.
Mkurugenzi wa Huduma Binafsi, Huduma Wezeshi na Shule ya Sabato wa Jimbo la Mara Kaskazini, Mchungaji Gadiel Mziray( kushoto) akiteta jambo baada ya mmoja mwa wenye ulemavu wa viungo kukabidhiwa baiskeli ya magurudumu matatu.
"Namshukuru Bhoke Orindo kwa kupambana kuwatafuta wadau mbalimbali ambao wamesaidia kambi hii kufanyika. Naishukuru mitaa ya makanisa yetu kwa michango yao, wadau kutoka maeneo mbalimbali pamoja na sapoti kutoka Jimbo letu la Mara Kaskazini."
Pia alimshukuru Mkurugenzi wa Shule na Chuo cha Mwera Vision, Hezbon Mwera, kwa kutoa ukumbi uliowezesha kufanyika kwa kambi hilo la watu wenye ulemavu kwa siku saba.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mwera Vision, Hezbon Mwera, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo Kanda ya Ziwa, aliwatia moyo watu wenye ulemavu wa viungo kutokata tamaa, huku akitoa fursa kwa watu wenye ulemavu kusoma bure fani mbalimbali watakazohitaji.
"Sisi wote ni walemavu watarajiwa. Kuna walemavu wengine walikuwa wazima lakini wakapata ajali na kuwa walemavu. Hapa chuoni kuna vijana tunawasomesha bure, wanajifunza ufundi na watakuwa wataalamu.
"Kwa mwenye ulemavu yeyote, namkaribisha aje chuo kwetu, atasoma bure fani yoyote atakayohitaji. Wasichana waliokatisha masomo tunawakaribisha, watasoma bure kwenye shule yetu ya msingi na sekondari pamoja na chuo," amesema Hezbon.
Mkurugenzi wa Mwera Vision, Hezbon Mwera, akimkabidhi fimbo nyeupe mwenye ulemavu wa macho miongoni mwa vifaa wezeshi vilivyotolewa na Josephati Mwita.

















Post a Comment