HEADER AD

HEADER AD

WANACHI KITONGOJI CHA KIHARAKA WAIPONGEZA TARURA BAGAMOYO KUJENGA MITARO

Na Gustaphu Haule ,Pwani

WANANCHI wa Kitongoji cha Kiharaka hususani katika eneo la Minazi Minane lililopo katika Kata ya Mapinga Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani wamesema athari waliyokuwa wanaipata ya kujaa maji katika maeneo yao sasa imekwisha.

Wamesema adha hiyo imekwisha baada ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Bagamoyo kujenga mitaro mikubwa ambayo itakuwa inakusanya maji hayo na  kuyaelekeza Bahati.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiharaka Deus Manjori amesema kuwa mitaro iliyojengwa na TARURA katika Kitongoji chake imekuwa na msaada mkubwa katika kipindi hiki cha kuelekea katika mvua za El-Nino.


      Ukaguzi wa mitaro ya kutolea maji na karavati uliofanyika na Meneja wa Tarura Wilaya ya Bagamoyo Bupe Angetile, Mhandisi wa Tarura Wilaya Wilaya ya Bagamoyo ( katikati) na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiharaka Deus Manjori, ukaguzi huo umefanyika Septemba 11/2026 .

Manjori ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali waliotembelea katika Kitongoji hicho Septemba 11,2026 kwa ajili ya kukagua miradi mbalimbali iliyotekelezwa na TARURA .

Manjori ,amesema kuwa kijiografia Kitongoji chake kipo chini kwa maana hiyo wamekuwa wakipata athari kubwa kipindi cha mvua huku akitolea mfano kuwa mvua zilizopita mwaka huu kaya 85 zilizungukwa na maji.

Amesema baada ya tukio hilo walipata msaada na kwamba anashukuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kupitia Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) wakajenga mitaro mikubwa ya kupitisha maji na kuelekea Baharini .

          Meneja TARURA Wilaya ya Bagamoyo Bupe Angetile akiwa na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiharaka kilichopo Kata ya Mapinga Deus Manjori na Mhandisi Mbaraka Seseme wakikagua mtaro uliojengwa na Tarura katika Kitongoji hicho.

Amesema ujenzi wa mtaro huo ni suluhisho kubwa kwa wakazi wa Kitongoji hicho kwani ujenzi huo ni maandalizi ya mazuri kuondoa athari za mvua za El-Nino zinazotarajia kunyesha kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa .

"Mtaro huu utawanusuru Wananchi wa Kiharaka ambao walikuwa wanatabika na maji ya mvua ambayo kila mwaka yalikuwa yanajaa katika nyumba zao na sasa adha hiyo imekwisha kwakuwa maji yote yatakuwa yanaenda Baharini kupitia mitaro iliyojengwa na Tarura",amesema Manjori.

Manjori amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Serikali yake kwa ujumla kwa kuwezesha ujenzi wa mtaro ambao umesaidia kuwaondolea adha Wananchi wa Kitongoji cha Kiharaka hususani katika eneo la Minazi Minane.

     Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kiharaka kilichopo Kata ya Mapinga Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani akiwaonyesha Waandishi wa habari ( hawapo pichani) namna ambavyo mtaro wa kupitisha maji kwenda Baharini ulivyojengwa.

Pia Manjori amemshukuru meneja wa TARURA Wilaya ya Bagamoyo Mhandisi Bupe Angetile pamoja na meneja wa Tarura Mkoa wa Pwani kwa kufanyakazi kubwa katika eneo ambayo imesaidia Wananchi kuondokana na adha ya miaka mingi ya kujaa maji katika nyumba zao.

     Mitaro na madaraja ya Karavati yaliyojengwa na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Bagamoyo katika Kitongoji cha Kiharaka kilichopo Kata ya Mapinga.

Manjori ametoa wito kwa Wananchi wa Kitongoji hicho kuhakikisha wanaitunza miundombinu ya mtaro huo huku wakizingatia usafi na kuwataka waache kutupa taka katika mtaro ili hata mvua zinapokuwa zinanyesha maji yaweze kupita bila vikwazo.

Nae Pilihilda Swai mwenyekiti wa kanisa Katoliki katika Parokia ya Yuda Thadei ameishukuru TARURA kwa ujenzi wa mitaro hiyo kwani wakati wa mvua waumini wengi walikuwa wanashindwa kwenda Kanisani kutokana na maji kujaa na hivyo kushindwa kupita.

Swai amewaomba TARURA kuendelea kuelekeza nguvu katika kutatua changamoto za Wananchi hususani katika maeneo yenye changamoto mbalimbali za barabara na hata vivuko.

Meneja wa TARURA Wilaya ya Bagamoyo Bupe Angetile amesema kuwa mitaro hiyo imejengwa katika barabara ya Mingoi - Kiembeni yenye urefu wa Kilomita Saba .

    Meneja wa TARURA Wilaya ya Bagamoyo Bupe Angetile akiwa katika ukaguzi wa mradi wa barabara na mitaro ya kupitishia maji katika Kitongoji cha Kiharaka Kata ya Mapinga Bagamoyo Mkoani Pwani ,ziara hiyo ilifanyika Septemba 11/2026.

Angetile amesema kuwa barabara hiyo ilikuwa inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaro ya kutolea maji wakati wa mvua na hivyo kuathiri makazi ya Wananchi hususani wa Minazi Minane.

Amesema baada ya kuona adha wanayoipata Wananchi hao, TARURA Wilaya ya Bagamoyo waliamua kuchukua hatua ya kujenga mitaro hiyo ili Kuzuia maji yasiende katika makazi ya Wananchi na kwamba hadi sasa hali ipo shwari hata katika kipindi cha mvua za El-Nino hali itakuwa vizuri tofauti na awali.


No comments