HEADER AD

HEADER AD

DIWANI KATA YA TANGINI AZINDUA MPANGO UGAWAJI VIAKISI MWANGA KWA MADEREVA WA PIKIPIKI


Na Gustaphu Haule, Pwani

DIWANI wa Kata ya Tangini katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Anthony Milao amezindua mpango maalum wa kugawa bure viakisi mwanga {Reflector}kwa madereva bodaboda wa kata hiyo ili kuwasaidia kutambulika watakapokuwa katika utekelezaji wa shughuli zao.

Milao amezindua mpango huo Oktoba 24/2026 kwa kugawa viakisi Mwanga kwa zaidi ya maafisa usafirishaji 200 kutoka vijiwe mbalimbali  kikiwemo kijiwe cha TMK, Maduka Matatu, Gill Msikitini, Machinjioni Kijiwe cha Kwa mama Rose , Kijiwe cha Kala Garden na Kijiwe cha Efatha.

        Diwani wa Kata yang Tangani Anthony Milao (CCM) kulia akimkabidhi mmoja wa kiongozi wa kijiwe cha Bodaboda cha Gill Msikitini kiakisi mwanga kwa ajili ya kufanyia shughuli zao.

Akizungumza katika uzinduzi huo Milao amesema kuwa ametoa msaada huo baada ya kupokea maombi kutoka kwa Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa usafirishaji (bodaboda ) Kata yaTangini ambaye aliwasilisha maombi mbalimbaliwasafirishaji viakisi mwanga hivyo.

Milao amesema kuwa mpango wa kugawa viakisi mwanga kwa maafisa hao utakuwa endelevu kwakuwa lengo kubwa ni kutaka kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao ili waweze kutambulika.


       Diwani Kata ya Tangini Anthony Milao(kulia) akimkabidhi kiakisi Mwanga mmoja wa dereva Bodaboda wa kijiwe cha Maduka Matatu Mtaa wa Kilimahewa ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa mpango wa kugawa bure Viakisi Mwanga kwa madereva hao.

Amesema mara nyingi maafisa wasafirishaji hao wamekuwa wakisumbuliwa kwa kukamatwa hovyo kutokana na kuhusishwa na matukio mbalimbali kwakuwa hawana utambulisho lakini kupitia viakisi mwanga hivyo usumbufu utapotea.

Aidha, Milao amewaomba maafisa usafirishaji hao kuhakikisha kila mmoja akiwa kazini anavivaa na kwamba kwa yule ambaye hatovaa akikamatwa hatopata msaada popote na badala yake atakuwa amejumuishwa na kundi la wahalifu.

"Nimekabidhi kulingana na mahitaji ya kila kituo kwa waliokosa tutatafuta wafadhili ili vijana wetu popote wanapoenda watambulike wanatokea wapi na hatawakipata changamoto iwe rahisi taarifa kufika sehemu husika," amesema Milao.

Milao amewasihi maafisa hao kuacha kujiunga kwenye makundi ya uhalifu na badala yake wawe sehemu ya kulinda amani na usalama na ikiwezekana wakiona kuna mwenzao anafanya mambo yasiyofaa ni vyema wakatoa taarifa mapema ili waweze kumdhibiti.

         Diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao wa kwanza kulia juu ya pikipiki akiwa katika picha ya pamoja na madereva Bodaboda wa kijiwe cha Kala Garden mara baada ya kugawa viakisi Mwanga kwa madereva hao Oktoba 24/2026.

Milao amesema Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha inatoa fursa kwa vijana hususani kwa kutoa mikopo ya fedha za asilimia 10 ambapo amewasisitiza vijana kutumia fursa hiyo kwa kujiunga vikundi Biya,imbali ili waweze kunufaika na fursa hiyo.

"Halmashauri yetu inatoa fedha kwa ajili ya kuwawezesha vijana na ninyi kama maafisa usafirishaji mnayo nafasi kubwa ya kupata fedha hizo lakini nawaomba mjiunge katika vikundi na mimi diwani wetu nitakuwa tayari kushirikiana nanyi ili kuona namna ya kuwasaidia kupata mikopo hiyo,"ameongeza Milao.

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Tangini Lazaro Biya, amesema kuwa CCM inathamini mchango wa maafisa usafirishaji na ndio maana kwasasa wapo katika mpango wa kuwasaidia mambo mbalimbali.

Biya amesema anachokifanya diwani ni utekelezaji wa aadi zake alizozitoa wakati wa kampeni na kwamba licha ya kutoa viakisi mwanga hivyo lakini bado diwani atawajengea vibanda ili wakati wa mvua au jua wapate sehemu ya kujistiri.

       Diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao (kushoto) akitoa msaada wa viakisi mwanga kwa madereva Bodaboda wa kijiwe cha TMK Msikitini zoezi ambalo lilifanyika Oktoba 24/2026.

Biya, amewaomba maafisa hao kuendelea kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi ( CCM) pamoja na viongozi wake akiwemo Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka pamoja na diwani wa Kata ya Tangini Anthony Milao.

Pia, Mwenyekiti huyo amewasisitiza vijana hao kulinda amani ya nchi kwakuwa amani ndio tunu ya Taifa kwani ikipotea hakuna kwa kukimbilia huku akitoa wito kuhakikisha wanawatolea taarifa vijana wageni ambao wanajiunga katika vijiwe vyao bila kujua wanapotokea.

Mbali na hayo, lakini pia Biya amewaomba maafisa hao kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia usajili wa kadi za eletroniki zinazotolewa kupitia usajili unaofanywa na vijana wa Tehama wa CCM na kwamba kwa yeyote mwenye Changamoto atoe taarifa ili waweze kumsaidia.

         Polisi Kata wa Kata ya Tangini Inspekta Haruna Msoke akitoa elimu ya kuacha uhalifu kwa vijana wa Bodaboda wa kijiwe cha kwa Mama Rose Mtaa wa Kilimahewa ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa mpango wa kugawa Viakisi Mwanga uliokuwa ukifanywa na diwani wa Kata hiyo Anthony Milao  Oktoba 24/2026.

Katibu wa Maafisa Usafirishaji Kata ya Tangini Issaya Hussein amemshukuru diwani wa Kata hiyo kwa kukubali ombi lao na kuwasaidia huku akimuomba kuendelea kushirikiana na kundi hilo kutatua changamoto zao.

Hussein amesema kuwa kupitia viakisi mwanga hivyo pamoja na ushirikiano wanaohupata kutoka kwa viongozi wa Kata hiyo watakuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanawasimamia wenzao kuvaa viakisi mwanga hivyo na wale wasiovaa watachukuliwa hatua.

Hatahivyo,afisa usafirishaji wa kijiwe cha Maduka matatu kilichopo Mtaa wa Kilimahewa Hassan Hassan amemshukuru diwani huyo kwa msaada huo kwani awali viakisi mwanga ilikuwa Changamoto kwao na sasa wamefurahi kuona diwani amewasaidia.

Hassan, amesema walikuwa wanashindwa kununua viakisi mwanga hivyo kwa kukosa fedha lakini pia wakati mwingine walikamatwa na viongozi wa chama chao na kupewa adhabu kwa kushindwa kuwa na kiakisi mwanga hicho lakini kwasasa usumbufu huo hautakuwepo tena.

No comments