HEADER AD

HEADER AD

MEYA KIBAHA AMWAGIZA MGANGA MFAWIDHI ZAHANATI YA BOKOTIMIZA KUHAKIKISHA DAWA ZA ARV ZINAANZA KUTOLEWA

Na Gustaphu Haule, Pwani

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas amemuagiza  Mganga Mfawidhi wa Zanahati ya Bokotimiza iliyopo Kata ya Tumbi Hangarukwi Idd kuhakikisha dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi(ARV) zinaanza kutolewa katika Zahanati hiyo.

Dr.Nicas ambaye pia ni diwani wa Kata ya Tumbi amesema hakuna sababu ya wagonjwa wanaohitaji dawa hizo kupata usumbufu wa kutumia gharama kubwa ya kusafiri kwa ajili ya kuzifuata dawa hizo wakati uwezekano wa kutolewa katika Zahanati hiyo upo.

       Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akizungumza na Wananchi wa Mtaa wa Bokotimiza na Bokotemboni  Kata ya Tumbi katika mkutano wake uliofanyika Oktoba 11/2026 .

Dr.Nicas ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika mkutano wake na Wananchi wa Mtaa wa Bokotimiza na Bokotemboni uliofanyika Oktoba 11/2026 kwa ajili ya kusoma taarifa ya utekelezaji wa ilani pamoja na kusikiliza kero za Wananchi.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi Kata ya Tumbi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Zahanati hiyo lengo likiwa ni kuwasogezea huduma Wananchi.

Amesema kama Zahanati hiyo ipo hakuna sababu tena ya Wananchi hususani kwa wale wanaoishi na virusi vya Ukimwi kusafiri umbali wa kilomita tano au sita kwa ajili ya kufuata dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi hali upo uwezekano wa kutolewa katika Zahanati hiyo.

       Wananchi wa Mtaa wa Bokotimiza na Bokotemboni wakimsikiliza diwani wa Kata ya Tumbi ambaye ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas.

"Mganga Mfawidhi pokea maelekezo yangu, nataka dawa za kufubaza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi zianze kutolewa katika Zahanati hii ya Bokotimiza, nenda kazungumze na Mganga Mkuu wa Manispaa ili dawa high zipatikane hapa,"amesema Dr.Nicas.

Katika hatua nyingine Dr.Nicas amesema amepokea changamoto ya ukosefu wa mashine ya Ultra- Sound katika Zahanati hiyo na kwamba atalifanyia kazi ndani ya wiki moja ili kuhakikisha Wananchi wanapata huduma stahiki.

Amesema yeye amechaguliwa na Wananchi kwa ajili ya kutatua changamoto zao na kwamba atafanyakazi kuhakikisha ndani ya miaka mitano kila changamoto inapatiwa ufumbuzi ambapo amewaomba Wananchi kuwaunga mkono viongozi waliopo madarakani ili waweze kutimiza matarajio yao.

      Mzee Said Bakari Mkazi wa Mtaa wa Bokotimiza akichangia mada katika mkutano wa Wananchi uliofanyika chini ya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas Oktoba 11/2026.

Changamoto ya ukosefu wa Ultra -sound katika Zahanati hiyo iliibuliwa na mwananchi wa Bokotimiza Ramadhani Ndete  ambaye alisema wajawazito wengi wamekuwa wakisumbuka kupata huduma hiyo.

Ndete amesema wajawazito wamekuwa wakifuata huduma ya Ultra - sound  katika kituo cha afya Mkoani na hospitali ya Rufaa ya Tumbi na kwamba gharama zinazotumika ni kubwa na wakati mwingine huwa wanashindwa kumudu gharama hizo.

Amesema kwa siku mjamzito mmoja anaweza kutumia nauli ya kwenda na kurudi Sh.25000 na wakati huohuo bado gharama za dawa  zinazoandikwa hospitali.

Mganga Mfawidhi wa Zanahati ya Bokotimiza Hangarukwi Idd amesema ni kweli mahitaji ya Ultra- sound  katika Zahanati hiyo ni makubwa kwani kwa siku moja wajawazito 15 hadi 25 wanapata huduma na kwa mwezi ni kati ya wajawazito 140 hadi 160 .

      Wananchi wa Mtaa wa Bokotimiza na Bokotemboni Kata ya Tumbi wakimsikiliza diwani wao Dr.Mawazo Nicas katika mkutano uliofanyika Oktoba 11/2026.

Amesema anamshukuru Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas kwa hatua aliyoichukua katika kuwasaidia wajawazito wanaotibiwa katika hospitali hiyo na kwamba kupatikana kwa mashine itakuwa imerahisisha utendajikazi katika Zahanati hiyo.

No comments