HEADER AD

HEADER AD

MEYA KIBAHA ARIDHISHWA NA KASI YA MKANDARASI DIMETOCLASSA REALHOPE LIMITED ANAYEJENGA SOKO LA MNARANI - LOLIONDO


Na Gustaphu Haule, Pwani

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr. Mawazo Nicas amefanya ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa Soko la Kisasa la Mnarani -lililopo eneo la Loliondo Kata ya Tangini na kueleza kuridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikia katika mradi huo.

Mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi Dimetoclassa Real Hope limited kupitia mpango wa Tactic ambapo hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 45 ya utekelezaji wake.

       Mradi wa soko la Mnarani unaojengwa katika Kata ya Tangini kupitia mkandarasi Dimetoclasa Real Hope Limited.

Dr.Nicas amefanya ziara hiyo Oktoba 08,2026 akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali  akiwemo Mwenyekiti wa soko la Loliondo Mohamed Mnembwe na baadhi ya wafanyabiashara wakiwemo mama lishe.

Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo Dr.Nicas amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo huku akisema kukamilika kwa mradi huo ni mkombozi kwa wananchi wa Manispaa ya Kibaha ambao watakuwa na soko la uhakika na sehemu sahihi ya kufanyia biashara.

Dr. Nicas amesema ameridhishwa kwa kazi nzuri inayofanywa na mkandarasi Dimetoclassa Real Hope limited na kwamba kwa kasi hiyo anaimani mradi huo utakamilika kwa wakati kulingana na mkataba.

Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwakuridhia ujenzi wa soko hilo ambalo linaenda kuwa kubwa na la kisasa.

          Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akizungumza na mkandarasi wa ujenzi wa soko la Mnarani pamoja na wafanyabiashara katika ziara yake ya kukagua ujenzi wa soko la Mnarani Oktoba 08/2026.

Amesema kwa maelezo ya Mkandarasi mshauri wa ujenzi wa soko hilo kufikia Februari 2027 mradi huo utakuwa umekamilika na wafanyabiashara ambao kwa sasa wapo katika soko la muda watarejea kwenye maeneo yao ya biashara.

Amemuagiza mkandarasi huyo kuhakikisha wanaongeza spidi na ikiwezekana wajenge usiku na mchana ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa ili kuhakikisha wafanyabiashara wanapata mazingira mazuri na sahihi kwa biashara zao.

"Manispaa ya Kibaha inamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu mkubwa na sisi tunataka ukamilike mapema ili kusudi wafanyabiashara wawe katika mazingira mazuri na wananchi wapate soko la uhakika la kununua mahitaji yao," amesema Dr.Nicas.

Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa soko hilo Emmanuel Mahimbo, amesema wanatakiwa kumaliza kazi kwa wakati na yeye kama mhandisi mshauri watamsimamia mkandarasi ili aweze kumaliza kazi mapema .

       Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas mwenye kofia ngumu (katikati) akizungumza katika mradi wa soko la Mnarani.

Mahimbo amesema kuwa anafahamu sasa hivi wanaelekea katika kipindi cha mvua lakini tayari wameshauri mkandarasi na wamejipanga vizuri kufanyakazi wakati wa mvua bila kusimama ili kazi yote ikabidhiwe kulingana na mkataba unavyotaka Februari 10/2027.

Mahimbo amesema anaishukuru Serikali kwakutoa ushirikiano kwa mkandarasi na Mhandisi Mshauri ambapo pia amemshukuru Rais Samia ambaye ndiye kiongozi wa mradi huo na amekuwa na msaada mkubwa katika kuhakikisha mradi huo unakamilika.

Meneja mradi huo upande wa mkandarasi mhandisi Shabani Kaswaka amesema kuwa wao wamejipanga kukamilisha mradi huo kwa wakati na mpango wao wa sasa ni kufanyakazi usiku na mchana.

Kaswaka amesema kuwa wamepokea maelekezo ya meya wa Manispaa ya Kibaha na watayafanyiakazi ili kuhakikisha lengo la kutekeleza mradi huo linafikiwa kama ambavyo mipango ya Serikali ilivyopangwa.

Mwenyekiti wa soko la Loliondo Mohamed Mnembwe amesema anamshukuru Rais Samia kwa kuwaletea mradi mkubwa wa soko hilo na kwamba wao kama wafanyabiashara soko litakapokamilika litakuja na tija kwa wafanyabiashara.

         Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas mwenye tai nyekundu akikagua barabara ya Tughe-Anglican inayojengwa kwa kiwango cha lami kupitia mkandarasi Dimetoclasa Real Hope Limited.

Ameomba baada ya kukamilika kwa soko hilo wafanyabiashara waliohamishwa kupisha ujenzi huo basi wote wapate eneo la kufanyia biashara zao huku akisema hadi sasa idadi ya wafanyabiashara hao ni 1,550.

Mradi wa TACTIC una thamani ya Tsh. Bilioni 19.83  ukihusisha ujenzi wa Soko la Kisasa la Mnarani, Ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 4.8, bustani ya mapumziko na burudani na ujenzi wa jengo la usimamizi wa mradi.


No comments