RC KAGERA AWATOA HOFU WANANCHI BAADA YA KUTOKEA TETEMEKO LA ARDHI
Na Alodia Babara, Bukoba
BAADHI ya wananchi mkoani Kagera wameeleza kwa hisia na kuonyesha hofu baada ya kutokea tetemeko la ardhi lenye ukumbwa wa 5.0.
Tetemeko hilo la ardhi limetokea Oktoba 09, 2026 kati ya saa 11:20 hadi 11.25 alfajiri na kusababisha hofu na wasiwasi miongoni mwa wansnchi huku wakikumbuka tetemeko la ardhi lililotokea miaka 10 iliyopita na kusababisha madhara makubwa ikiwemo vifo.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali Yahya Kido amewaondoa hofu wamanchi wa mkoa huo huku akiwataka kuwa watulivu.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali Yahya Kido akizumgumza na waandishi wa habari juu ya tetemeko la ardhi lililotokea leo mkoani humo.Kanali Kido ametaja wilaya ambazo zimekumbwa na tetemeko la ardhi kuwa ni wilaya nne kati ya saba za mkoa huo ambazo ni wilaya ya Bukoba, Misenyi, Karagwe na Ngara.
"Hali ya mkoa wa Kagera ni shwari hakuna taarifa zozote za madhara yaliyoripotiwa, timu ya wataalamu wa maafa inaendelea kufanya tathimini katika maeneo yetu ili kupata taarifa za kina na kujua kama kuna madhara yaliyojitokeza" amesema Kanali Yahya.
Esta Kagaruki mkazi wa manispaa ya Bukoba ameeleza kukumbwa na wasiwasi pamoja na hofu lilipotokea tetemeko.
'Kutokana na joto lililokuwepo usiku nililazimika kulala bila kuvaa nguo, lilipotokea tetemeko nimekurupuka na kufungua mlango ili niwahi kutoka nje, bahati nzuri ilikuwa bado usiku na majirani zangu wamekaa ndani hawakutoka tetemeko lilipoisha nikarudi ndani nikatafuta kitenge nikarudi nje ili lisije jingine likanikuta maana wanasemaga huwa yanafuatana mawili" amesema Kagaruki.
Kwa upande wake Alhaji Swalehe Mustapha mkazi wa wilaya ya Misenyi ameeleza kuwa, lilipotokea tetemeko amejawa na hofu na kwamba tetemeko hilo ni ishara kuwa, mwanadamu ambaye hatambui kuwa Mungu yupo ajue yupo na anaweza kufanya chochote na kwa muda wowote.
"Tuendelee kuweka tahadhari linapotokea tetemeko kama hili tutoke ndani ya nyumba tuwe nje na tumuombe sana Mwenyezi Mungu atuepushe na majanga kama haya maana binafsi tetemeko hili limenikumbusha tetemeko lililotokea mwaka 2016"amesema Alhaji Mustapha.
Ikumbukwe kuwa, Septemba 10,2016 lilitokea tetemeko la ardhi mkoani Kagera ambalo lilisababisha watu 17 kupoteza maisha, 253 walijeruhiwa, nyumba za makazi 840 zilianguka na 1,264 zilipata nyufa.


Post a Comment