HEADER AD

HEADER AD

MEYA KIBAHA ATOA SIKU SABA KWA UONGOZI WA KIWANDA CHA CORDY KUHAKIKISHA WANAJENGA MITARO

 


Na Gustaphu Haule, Pwani

MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt. Mawazo Nicas ametoa siku Saba kwa uongozi wa kiwanda cha  Maisha (Cordy) kuhakikisha wanajenga mtaro wa kupitisha maji machafu ya kiwandani ili kuondoa kero inayowakabili Wananchi wanaoishi karibu na kiwanda hicho.

Dkt.Nicas ametoa kauli hiyo Oktoba 07/2026/ aliofanya ziara ya kushtukiza katika kiwanda hicho na kukuta kinatiririsha maji machafu katika makazi  ya wananchi ambayo yanaathiri jamii na viumbe hai ikiwemo mifugo.

      Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas akikagua mitaro ya kupitishia maji machafu katika kiwanda cha Maisha na kulia kwake ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lulanzi Thobias Shilole.

Kufanyika kwa ziara hiyo ilifuatia  malalamiko ya muda mrefu ya wananchi wa Mtaa wa Picha ya Ndege kuhusu harufu kali na maji ya rangi ya nyeusi yanayotiririka mitaani na kuingia kwenye makazi yao na kuleta athari kwa jamii ikiwemo kubabuka pamoja na mifugo kufa inapokunywa maji hayo.

Mara baada ya kufika katika kiwanda hicho, Mstahiki Meya na timu yake kutoka idara ya Mazingira walikuta bomba kubwa la siri pamoja na chemba likiwa limeelekezwa moja kwa moja kwenye mtaro unaopita kwenye makazi ya wananchi.

Dkt. Nicas amesema kiwanda hicho alikitembelea miezi michache iliyopita na kuwapa maelekezo lakini utekelezaji wake mdogo jambo ambalo kwasasa lazima hatua zichukuliwe.

      Ukaguzi wa mitaro ya kupitisha maji machafu uliofanyika Oktoba 07,2026 na Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas katika kiwanda cha Maisha (CORDY) kilichopo katika Kata ya Picha ya Ndege.

"Miezi minne iliyopita nilikuja hapa na nikatoa maelekezo lakini nashangaa hadi leo hawajafanya lolote na leo natoa siku saba kuhakikisha wanajenga mtaro ili kuhakikisha maji machafu hayaendi kwa Wananchi na nitarudi tena kukagua maagizo yangu yametekelezwa,"amesema Nicas.

Amesema kiwanda cha Cordy hakina mfumo wa kuchuja maji taka na sasa amewapa siku saba kuweza kuhakikisha wanajenga mfumo wa maji taka na baada ya hapo mamlaka ya bonde waje kwa ajili ya kupewa kibali cha kutiririsha maji baada ya ya kuyatibu.

Amesema kabla ya kuchukuliwa hatua yoyote ya kisheria anawapatia hadi siku ya Jumapili ya tarehe 12/10/2026 kuweza kusafisha mtaro huo na atafika kwenye eneo hilo kuangalia kama wametekeleza na isipofanyika hivyo watachukuliwa hatua kulingana na sheria ya Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha.

Afisa Mazingira Manispaa ya Kibaha,  Bryson Mpogoza amesema kiwanda hicho kilishapigwa faini na Baraza la Mazingira NEMC na waliahidi watatekeleza yale waliyoelekezwa ila imeonekana wamekuwa wakaidi.

        Diwani wa Kata ya Picha ya Ndege Grace Jungulu (kulia) akiwa na Meya wa Manispaa ya Kibaha Dkt.Mawazo Nicas wakikagua mitaro ya maji machafu katika kiwanda cha Maisha Oktoba 07/2026.

Amesema Manispaa itaangalia ni kwa namna gani wanahakikisha wanasimamia yale yote yaliyosemwa na Mstahiki Meya ikiwemo kusafisha maeneo wanayomwaga majitaka na kujenga mfumo wa uchujaji wa maji taka.

Afisa raslimali watu wa kiwanda hicho Vicent Emmanuel amesema amepokea maelekezo yaliyotolewa na Meya wa Manispaa ya Kibaha na wataanza kufanyiakazi kuanzia Oktoba 08,2026.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lulanzi Thobias Shilole amesema changamoto hiyo ni ya siku nyingi ambapo amemuomba Meya huyo kuhakikisha analisimamia jambo hilo ilikusudi Wananchi wawe katika mazingira yenye usalama.


No comments