MWENYEKITI CCM KATA YA TANGINI ATOA MSAADA KITUO CHA WATOTO YATIMA
Na Gustaphu Haule, Pwani
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Tangini Lazaro Biya amekifikia kituo cha watoto yatima cha Umra( Umra Orphanage Centre) kilichopo Mtaa wa Vikawe Kata ya Pangani na kutoa msaada wa vyakula mbalimbali.
Msaada alioutoa ni pamoja na mchele Kilo 30, Unga wa Sembe kilo 50, mafuta ya ngozi dazeni mbili, Maharage kilo 15, Sabuni kilo 25, vifaa vya shuleni ikiwemo kalamu pamoja na mahitaji mengine mbalimbali yenye thamani ya Sh.500,000.
Biya ametoa msaada huo Oktoba 02,2026 wakati alipofanya ziara maalum ya kuwatembelea watoto wa kituo hicho ikiwa ni sehemu ya kutoa shukrani yake mara baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa Kata ya Tangini katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 01,2026.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Tangini Lazaro Biya( kushoto mwenye shati la kijani) akimkabidhi msaada wa vyakula, sabuni na mahitaji mbalimbali msimamizi wa kituo cha watoto yatima cha Umra Kilichopo Vikawe Kata ya Pangani Lusenene Mzafaru.Katika uchaguzi huo Biya aliibuka mshindi kwa kupata kura 93 dhidi ya mpinzani wake Mfaume Kabuga( Kalanguti) aliyepata kura 37 huku Jenifa Mbawala akipata kura 01 dhidi ya wapiga kura walioshiriki katika uchaguzi huo 131.
Akizungumza wakati akikabidhi msaada huo Biya amesema kuwa amewiwa kuwagusa watoto hao kwakuwa anatambua kundi hilo ni muhimu na linahitaji msaada kutoka kwa jamii.
Amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya shukrani yake baada ya wanaCCM wa Kata ya Tangini kumchagua kuwa mwenyekiti wao na akaona ni vyema kabla ya kuanza kufanya chochote ni vyema akawagusa watoto yatima ili hiwe sehemu ya ibada yake.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Tangini Lazaro Biya akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya watoto yatima wa kituo cha Umra Kilichopo Mtaa wa Vikawe Kata ya Pangani alipokwenda Oktoba 02,2026 kwa ajili ya kuwapelekea msaada wa vitu mbalimbali."Mimi nimewashukuru wanaCCM wa Kata ya Tangini kwa kunichagua lakini nikaona shukrani zangu zisifanyike hivihivi bali nije kuwaunga mkono watoto yatima wa kituo hiki cha Umra kwa kuwaletea kitu kidogo ambacho kitaweza kuwasogeza mbele,"amesema Biya.
Biya amewaomba viongozi na wadau wengine wa maendeleo kujitokeza katika kuwasaidia watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu ili na wao waweze kupata mahitaji yao ya msingi kama ambavyo watoto wengine wanapata.
Msimamizi wa kituo hicho Lusenene Mzafaru amemshukuru mwenyekiti huyo kwa msaada alioutoa huku akisema vyakula hivyo vitakwenda kuwasaidia kupata chakula na hivyo kuzidi kuimarisha afya zao.
Mzafaru, amesema kituo hicho kwasasa kina watoto yatima 49 kati yao Wanaume 24 na Wanawake 25 ambapo baadhi yao wanasoma katika shule ya Msingi na wengine wakisoma katika shule za Sekondari na chuo.
Baadhi ya viongozi wa CCM Kata ya Tangini akiwemo Mwenyekiti wa CCM Lazaro Biya, Mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi Kata ya Tangini Jeremiah Komba na Katibu wa UVCCM Kata ya Tangini Benjamini Lazaro na wadau mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja na watoto yatima wa kituo cha Umra.Amesema changamoto yao kubwa kwasasa ni kupata makazi ya kudumu kwakuwa eneo waliopo sasa hivi limekuwa na mgogoro ambao unawataka wahame ikifika Januari 2027.
Mzafaru ameiomba Serikali, viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuona namna ya kuwasaidia kupata eneo la kudumu la kujenga makazi ya watoto hao ili kuondoa usumbufu ambao kwasasa umejitokeza.
Akizungumza kwa niaba ya watoto wa kituo hicho mmoja wa watoto hao, Husna Yusuf amemshukuru mwenyekiti wa CCM Kata ya Tangini Lazaro Biya kwa kuona umuhimu wa kufika kituoni hapo na kuwapelekea chakula.
Husna, amesema kwao msaada huo ni mkubwa kwakuwa chakula ndio msingi wa maisha yao ambapo amemuomba mwenyekiti huyo kuendelea kujitoa na kuwasaidia bila kuchoka kwakuwa maisha yao yanategemea zaidi misaada kutoka kwa watu mbalimbali na jamii kiujumla.




Post a Comment