MEYA MANISPAA YA KIBAHA ASITISHA SHUGHULI ZA UCHIMBAJI MADINI YA MCHANGA KATIKA BONDE LA MTO MPIJI

>> Ni baada ya kubaini hakuna kibali kilichotolewa kuchimba mchanga eneo hilo
Na Gustaphu Haule, Pwani
MSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas amesitisha shughuli za uchimbaji wa madini ya mchanga katika bonde la Mto Mpiji katika eneo la Mtaa wa Vikawe Bondeni Kata ya Pangani.
Dr.Nicas amefikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwa hakuna kibali kilichotolewa na Manispaa ya Kibaha kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya mchanga katika eneo hilo hali ambayo inapelekea kupoteza mapato ya Manispaa.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akiwaonyesha waandishi wa habari athari za uharibifu wa mazingira zilizotokana na uchimbaji wa mchanga katika Bonde la Mto Mpiji lililopo Mtaa wa Vikawe Bondeni Kata ya Pangani alipofanya ziara ya kukagua machimbo hayo Oktoba 13/2026.Dr.Nicas amesitisha shughuli hizo Oktoba 13/2026 wakati akiwa katika ziara yake ya kutembelea machimbo hayo na kubaini shughuli za uchimbaji zikiwa zinaendelea lakini hakuna kibali cha Manispaa ya Kibaha kilichoruhusu watu wachimbe mchanga katika eneo hilo.
Amesema kwa tishio la mvua za El-nino zilizotangazwa na wataalamu wa hali ya hewa na mazingira ameona hali ilivyo na uharibifu mkubwa wa mazingira na Manispaa haikutoa kibali cha uchimbaji katika eneo hilo.
Amesema ni marufuku kuendelea kuchimba mchanga katika eneo hilo kwasababu linahatarisha usalama wa wananchi pale ambapo mvua za El-nino zitakapoanza kunyesha.
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kutembelea machimbo ya mchanga katika bonde la Mto Mpiji lililopo Mtaa wa Vikawe Bondeni Kata ya Pangani."Kwa niaba ya baraza la madiwani la Manispaa ya Kibaha kuanzia leo nasitisha shughuli za uchimbaji wa mchanga katika bonde hili la mto Mpiji na ni marufuku kumuona mtu wala gari linaingia kuchukua mchanga hapa na tunaweka askari atakayekamatwa sheria zipo,"Amesema Dr.Nicas.
Dr.Nicas amesema kuwa watu wanachimba holela bila kufuata utaratibu na hakuna mapato yanaingia Serikalini huku mazingira yakiharibiwa kwahiyo haiwezekani kukaa kimya kwa kuwaacha watu waharibu mazingira.
Amesema Mto Mpiji unatenganisha Manispaa mbili ikiwemo Ubungo na Kibaha lakini upande wa Ubungo walishapiga marufuku siku nyingi na wameweka askari wa doria na badala yake wakaamua kukimbilia kuchimba Kibaha.
Ukaguzi wa machimbo ya mchanga katika bonde la mto Mpiji Mtaa wa Vikawe Bondeni Kata ya Pangani uliofanywa na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas Oktoba 13/2026.Amesema kwasasa Manispaa ya Kibaha pia inapiga marufuku na muda wote watakuwa askari wakifanya doria na kulinda eneo hilo ili lisiweze kuendelea kuharibiwa ambapo ameomba ushirikiano kwa Halmashauri ya Ubungo ili kuimarisha ulinzi katika pande zote mbili.
Dr.Nicas ameongeza kuwa kwa yeyote atakayekiuka agizo hilo atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria za mazingira na madini.
Afisa mazingira wa Manispaa ya Kibaha Byson Mpogoza amesema Manispaa ya Kibaha haijatoa kibali cha uchimbaji wa madini ya mchanga katika eneo hilo na uchimbaji huo ni uchimbaji holela ambao haujafuata utaratibu.
Afisa Mazingira wa Manispaa ya Kibaha Byson Mpogoza akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu uchambaji holela wa mchanga uliofanywa katika bonde la Mto Mpiji Mtaa wa Vikawe Bondeni Kata ya Pangani.Mpogoza amesema kuwa utaratibu wa kupata kibali unaanzia katika ngazi ya Mtendaji wa Kata husika na baadae taratibu zinaendelea hadi kwa Mkurugenzi wa Manispaa lakini hadi sasa hakuna utaratibu wowote uliochukuliwa.
Amesema kwa mazingira yanavyoonekana katika eneo hilo ni mazingira hatarishi hasa katika kipindi cha mvua za El-nino pale zitakapoanza ambapo ametoa rai kwa Mtendaji wa Kata ya Pangani kuendelea kuwahimiza wananchi kuacha kuchimba kwakuwa ni hatari kwa maisha yao.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Vikawe Bondeni Ally Athumani amesema kuwa mazingira yaliyopo katika machimbo hayo si rafiki kwa wananchi kama ambavyo Serikali imetangaza kuwepo kwa mvua kubwa za El-nino.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Vikawe Bondeni Kata ya Pangani Ally Athumani (kushoto) akifafanua jambo kwa Meya wa Manispaa ya Kibaha Dr.Mawazo Nicas(kulia) wakati alipotembelea machimbo ya Mto Mpiji Oktoba 13/2026.Hata hivyo, Athumani amesema kuwa ni vyema Serikali ikaweka mazingira mazuri ili hata yakija mafuriko kusiwe na athari kubwa kwa wananchi wa Mtaa husika wa Vikawe Bondeni.





Post a Comment