WAZIRI MKUU AAGIZA WANANCHI PWANI WALIPWE FIDIA

Na Gustaphu Haule, Pwani
WAZIRI Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba amewaelekeza viongozi wanaohusika na Mamlaka ya ardhi katika ngazi ya Taifa,Mkoa na Wilaya kuhakikisha wanalipa fidia kwa wananchi hususani katika maeneo ambayo yamechukuliwa kwa ajili ya uwekezaji na shughuli mbalimbali za maendeleo.
Nchemba amesema sasa hivi tayari Serikali imeweka chanzo mahususi cha kuhakikisha fidia zinalipwa kwa wananchi kabla ya kutwa ardhi yao hasa katika maeneo ambayo yanatambulika kisheria au kwa utaratibu unaoeleweka.
Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani katika mkutano wa hadhara uliofanyika Oktoba 16/2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Majengo.
Dkt.Nchemba ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Oktoba 16/2026 katika viwanja vya shule ya Msingi Majengo vilivyopo Wilayani Bagamoyo Mkoa wa Pwani.
Amesema awali kulikuwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa Halmashauri na Mkoa wakichukua maeneo ya wananchi bila kufuata utaratibu kwa kigezo cha kutaka kuwekezaji na matokeo yake wananchi wengi walikuwa hawapati fidia na hivyo kudhuruhumiwa haki yao.
Amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imekuja na mfumo mzuri wa kuhakikisha kila mwananchi ambaye ardhi yake inataka kuchukuliwa na wawekezaji au Serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ni lazima kwanza wananchi hao walipwe fidia.
Mbunge wa Jimbo la Bagamoyo Subira Mgallu ( kulia) akimkabidhi Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba kikapu cha hoja za migogoro ya ardhi iliyopo katika jimbo hilo.
Dkt.Nchemba amesema kuwa kwakuwa Serikali tayari imeweka misingi mizuri ya kutetea maslahi ya wananchi ni vyema sasa wananchi wasichukie uwekezaji wala wawekezaji bali wachangamkie fursa ili waweze kupata maendeleo.
"Wawekezaji wakichukua eneo la ardhi kwa wananchi lazima walipe fidia kwa wenye ardhi lakini hata Halmashauri kama wanataka kuchukua eneo la mwananchi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo wahakikishe pia mhusika wa eneo analipwa fidia yake,"amesema Dkt.Nchemba
Dkt.Nchemba amewaeleza viongozi na wananchi waliokusanyika katika viwanja hivyo kuwa kwenye eneo la migogoro ya ardhi wala wasitumie nguvu kupambana kwasababu hata wakiuana, wakichukiana, ardhi haiongezeki ila watu ndio wanaongezeka.
Wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo waliojitokeza kumsikiliza Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba katika mkutano uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Majengo Oktoba 16/2026.
Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba amesema kwakuwa ardhi haiongezeki ni lazima sasa wawekeze nguvu katika matumizi bora ya ardhi huku akisema huwa anachukizwa na tabia ya uvunjifu wa sheria kwa makusudi.
Dkt.Nchemba amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo na timu yake kwa kazi kubwa aliyoifanya hasa kwa kuanzisha kliniki ya kusikiliza na utatuzi wa migogoro ya ardhi kwani ardhi ni moja ya mambo ambayo yanatisha.
Amemtaka Mkuu wa mkoa huyo kuendelea na kazi ya utatuzi wa migogoro ya ardhi ndani ya Mkoa wake lakini lazima ahakikishe wananchi wanapata haki zao kwa mujibu wa sheria bila kuonewa mtu huku akimuagiza Kamishna wa ardhi kuweka kambi ya wiki moja Wilayani Bagamoyo kwa ajili ya utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Wananchi Wilaya ya Bagamoyo wakimsikiliza Waziri Mkuu Dkt.Mwigulu Nchemba katika mkutano wa hadhara uliofanyika Oktoba 16/2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Majengo.
Amesema pamoja na mambo mengine lakini lengo ya ziara yake ni kufuatilia shughuli za maendeleo na kuhamasisha shughuli zote za maendeleo ili ziweze kuendelea kufanyika.
Dkt.Nchemba amesema katika kipindi cha miaka mitano chini ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amefanyakazi kubwa kwani amejenga hospitali kila Wilaya na kufikia idadi ya 129 lakini pia amejenga hospitali za mikoa na Rufaa huku vituo vya afya ni 649 na Zahanati zaidi ya 2700.
Amesema sio hivyo tu, lakini mambo makubwa yamefanyika katika barabara, elimu na hata katika sekta nyingine muhimu lakini pamoja na juhudi hizo bado kuna watu wanakwamisha shughuli za Rais kwakufanya mambo ya hovyo.
Amesema kati ya mambo hayo ni pamoja ni kumchangisha mgonjwa fedha ya gari la wagonjwa (Ambulance) jambo ambalo linaongeza chuki kati ya wananchi na Serikali yao huku akitaka jambo hilo liachwe maramoja.
"Hakuna kuchangisha mgonjwa fedha za Ambulance na hospitali itakayofanya hivyo wahusika watafukuzwa maramoja pia namuagiza Waziri wa Tamisemi kushughulikia watu hao na hata wale wanaozuia maiti majina yao tuyapate pia,"amesema Dkt.Nchemba.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo, amempongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwatumikia vyema wananchi wa Tanzania huku akisema Mkoa upo salama na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi na za kijamii.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Oktoba 16/2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Majengo Wilayani Bagamoyo mkutano ambao ulikuwa maalum kwa ajili ya Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba.
Amesema hadi sasa Mkoa umepokea zaidi ya Tsh.Trilioni 1.651 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na katika mwaka 2026/2027 Mkoa umeanza kutekeleza shughuli za maendeleo kwa kuzingatia vipaumbele dira ya Taifa ya mwaka 2050.
Nyongo amesema kuwa lengo ni kuhakikisha maendeleo ya mkoa wa Pwani yanachangia moja kwa moja na kufikia adhma ya Taifa ya kuwa na uchumi shindani, jumuishi na endelevu ifikapo 2050.
Nyongo amesema kuwa katika sekta ya viwanda Mkoa wa Pwani umeendelea kukua toka viwanda 1,387 mwaka 2021/2022 hadi kufikia viwanda 1,768 Septemba 2026 ambapo kati ya hivyo vikubwa ni 503, vidogo 248 na vidogo sana 1,017 huku kongani ya viwanda zikifikia 35 zilizotoa ajira 23,557 na ajira zisizo za moja kwa moja ni zaidi ya 62000.






Post a Comment